27.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, June 12, 2024

Contact us: [email protected]

Ngeleja amtumia Zitto kujitetea Escrow

willium NgelejaNA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM
MBUNGE wa Sengerema, William Ngeleja (CCM), ameishangaa hatua ya Baraza la Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kumtaka ajibu mashtaka ya kukiuka maadili ya umma.
Ngeleja pia aliishangaa sekretarieti hiyo kwa kile alichosema ‘limemuacha Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema)’ aliyedaiwa kufanya kosa linalofanana na lake kwa kupewa zaidi ya Sh milioni 30 kutoka Kampuni ya Pan African Solution Ltd (PAP).
Alitoa shutuma hizo Dar es Salaam jana alipozungumza mbele ya Baraza hilo huku akiwasilisha kielelezo chake cha pili juu ya madai ya ukiukwaji wa maadili yanayomkabili.
Ngeleja alisema kielelezo hicho hakitofautiani na tuhuma dhidi ya Zitto zilizotolewa na Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM) kwamba mbunge huyo wa Chadema alipokea fedha hizo kutoka PAP iliyohusishwa na suala la uchotwaji wa fedha za Akaunti ya Escrow.
Katika maelezo yake aliyoyatoa jana asubuhi kwa saa 4:14, Ngeleja alisema Zitto alituhumiwa kuchukua fedha hizo kwa awamu nne na kwamba alifanya hivyo wakati akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
“Pamoja na Lusinde kuzungumzia tuhuma hizo na kutoa ushahidi mbele ya Bunge kisha Zitto akataka achunguzwe na kufikishwa mbele ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, jambo hilo halikufanyika.
“Nashangaa katika suala hili, PAC haikunipa muda wa kujitetea wakati nilikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala kabla sijavuliwa wadhifa huo kutokana na tuhuma hizi.
“Pamoja na hatua nilizochukuliwa, Zitto amebaki na nafasi yake na wala hajaitwa kwenye sekretarieti, hali hii inanifanya nijiulize kwa nini sheria inachagua.
“Hata wakati wa kusomwa hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo ya mwaka 2014/15, Lusinde alitaka kujua uhalali wa Zitto kupokea msaada kutoka kwa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF).
“Pamoja na kutolewa ushahidi, Bunge halikumuadhibu Zitto wakati likijua Zitto kama mwenyekiti wa kamati anahusika kuyakagua mashirika hayo.
“Kwa hiyo natoa ushahidi kama kiambatanisho cha utetezi wangu,” alisema.
Akijibu hoja ya kupewa Sh milioni 40.4 kutoka Kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited iliyokuwa na hisa ya asilimia 30 na Kampuni ya Kufua Umeme (IPTL), alisema amekuwa akiomba misaada ya kumsaidia kutatua matatizo kutoka kwa wafadhili mbalimbali.
Kuhusu shtaka la kuingiziwa fedha katika akaunti ya namba 0011010265260 iliyoko Benki ya Mkombozi, Tawi la St. Joseph, Dar es Salaam, Ngeleja alikana kuitambua akaunti hiyo na kusema akaunti yake ni 00110102652601.
Baada ya kuwasilisha namba ya akaunti hiyo, Mwenyekiti wa Baraza la Sekretarieti hiyo, Jaji mstaafu, Hamis Msumi, aliomba iangaliwe kama jina lililotajwa kwenye hati ya mashtaka lilikuwa la mlalamikiwa na ilithibitika lilikuwapo jina la Ngeleja.
Kuhusu shtaka la kujiingiza katika mgongano wa kaslahi kwa kukubali kuchukua kiasi hicho cha fedha wakati akijua VIP ilikuwa na hisa asilimia 30 kwenye Kampuni ya IPTL, alisema hakuwahi kupokea fedha kutoka kampuni hiyo na badala yake alipokea fedha kwa VIP TZS Trustee.
“Msaada niliopokea hausababishi mgongano wa maslahi kama inavyoelezwa katika sheria ya maadili kifungu cha 6 (e) na ndiyo maana hata nilipotakiwa na TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) kulipa kodi ya asilimia 30, nililipa Shi milioni 13, tena bila kuhoji kama Rugemalila alikuwa ameshazilipia,” alijitetea Ngeleja.
Baada ya kumaliza kujitetea, Wakili wa Sekretarieti hiyo, Hassan Mayunga, alianza kumhoji na mahojiano yao yalikuwa hivi.
Wakili: Unataka kutueleza kwamba wanasiasa mnaishi kwa kuombaomba?
Ngeleja: Ndiyo, wanasiasa tunaishi kwa kuombaomba kwa sababu hata nchi yetu inaombaomba kwa kuwa bajeti haitoshelezi.
Wakili: Fedha ulizopewa ni za umma au binafsi?
Ngeleja: Fedha zile nilipewa kwa ajili ya kusaidia Watanzania katika shida ambazo haziingizwi kwenye bajeti kama vile ujenzi wa makanisa na misikiti.
Kuhusu shtaka la kutuhumiwa kutumia wadhifa wake kwa kujipatia manufaa ya fedha kinyume na kifungu cha 12 (1) (e) cha Sheria za Maadili, mbunge huyo alisema wakati anazipokea, nafasi yake ya uwaziri ilikuwa imeshakoma tangu Mei 4, 2012.
“Nikiwa Naibu Waziri, sikuwahi kulalamikiwa au kupatwa na tuhuma kutoka Kamati ya Bunge, kwamba nimewahi kuhusika katika kuipendelea Kampuni ya VIP,” alisema.
Aliliomba baraza hilo kutoa mwongozo kwa wabunge wote ili wazuiwe kuomba misaada kama haistahili katika sheria kwa kuwa wabunge wote hutumia njia hiyo.
“Naomba kama suala hilo ni kosa, rungu lisianzie kwangu kwa sababu utaratibu wa kuomba misaada si wangu peke yangu, huu ni wa wabunge wote akiwamo Zitto.
“Hivyo, sijatenda jambo hilo kwa nia mbaya bali ni taratibu zilizozoeleka na sasa najiweka mikononi mwa baraza kusubiri uamuzi kwa sababu fedha nilizopewa zilikuwa za kusaidia Watanzania,” alisema.
Baada ya mahojiano hayo, alilishukuru baraza hilo kwa kumpa kwa mara ya kwanza nafasi ya kujitetea kuhusu mashtaka aliyotuhumiwa.
Jaji Msumi alisema Baraza litapitia jalada hilo na kulipeleka katika mamlaka husika kwa ajili ya kutoa uamuzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles