SAFARI ya Miss Tanzania 2014, Lilian Kamazima, anayetarajiwa kuagwa leo ipo tayari kwa ajili ya kwenda kushiriki mashindano ya Dunia (Miss World) ambayo fainali zake zitafanyika ukumbi wa Beauty Crown Grand Theatre, nchini China.
Shindano hilo la dunia linatarajiwa kufanyika Desemba 19, mwaka huu, likijumuisha washiriki kutoka nchi zaidi ya 120 wakiwania taji linaloshikiliwa na Rolene Strauss kutoka nchini Afrika Kusini, aliyeibuka kidedea mwaka jana jijini London, England.
Ofisa Uhusiano wa Lino International Agency ambao ni waandaaji wa mashindano ya urembo nchini, Haidari Ricco, alisema wakiwa nhini China, Lilian pamoja na warembo wengine watakuwa katika Hotel ya Beauty Crown Sanya kuanzia Novemba 21 hadi siku ya fainali hizo.
Ricco alisema washiriki wote wamehamasishwa kutumia mitandao ya kijamii ili kujitangaza na kutangaza utalii wa China pamoja na shindano hilo kwa kuwa mitandao hiyo itatoa alama kwa washiriki wote watakaoitumia vizuri.