24.9 C
Dar es Salaam
Sunday, April 21, 2024

Contact us: [email protected]

SAFARI YA KAFULILA, CHADEMA – NCCR – CHADEMA – ‘CCM’

Na ESTHER MBUSSI-DAR ES SALAAM


MBUNGE wa zamani wa Kigoma Kusini, David Kafulila, ametengeneza historia nyingine kisiasa, hasa baada ya kutangaza kuhama Chadema.

Hatua hiyo inatajwa kama historia ya aina yake kwa mwanasiasa huyo, ambaye ametumikia vyama viwili tofauti katika kipindi cha miaka 10, huku akitarajiwa wakati wowote kujiunga na chama kingine hivi karibuni.

Kafulila alitangaza uamuzi wa kujivua uanachama wa Chadema jana katika taarifa yake, huku akidai kwamba hana imani tena na upinzani katika kupambana na ufisadi.

Hii ni mara ya pili kwa Kafulila kutoka Chadema baada ya mwaka 2009 alipoondoka na kujiunga na NCCR-Mageuzi.

Hatua ya mwanasiasa huyo kijana, imekuja siku moja baada ya juzi Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), kuridhia kupokewa kwa waliokuwa wanachama wa Chadema; aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrance Masha na Mwenyekiti wa Bavicha, Patrobas Katambi.

Katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari, Kafulila, alidai kwamba kwa sasa bado anatafakari na hivi karibuni atatangaza jukwaa jipya, akimaanisha chama atakachohamia ili kuendeleza harakati zake dhidi ya ufisadi.

Akielezea sababu za kuhama Chadema ikiwa ni miezi 11 tu tangu ahamie akitokea NCCR-Mageuzi, alisema ni upinzani kukosa ajenda ya ufisadi.

Kafulila, alisema hiyo inatokana na Rais Dk. John Magufuli kushughulikia kwa vitendo ajenda ya ufisadi, hasa baada ya watuhumiwa na wahusika wa rushwa kubwa kufikishwa mahakamani.

“Nikiwa mmoja wa wanasiasa vijana, nilibahatika kutumikia Bunge la 10, siku zote nimejipambanua na kujitoa mhanga kupambana na ufisadi kupitia jukwaa la Bunge, vyama vya siasa na shughuli mbalimbali za kijamii kwa ujumla.

“Hata hivyo, katika siku za hivi karibuni na hasa tangu harakati za uchaguzi mwaka 2015, vyama vya upinzani nchini vinaonekana kupigwa ganzi na kupooza katika juhudi zake za kupambana na ufisadi.

“Tangu Rais Magufuli achaguliwe na kukabidhiwa jukumu la kuongoza nchi, vita ya miaka mingi dhidi ya ufisadi imechukua sura mpya.

“Ghafla ufisadi siyo tena ajenda kuu ya upinzani nchini kwa sababu ni wazi kuwa upinzani siyo tena jukwaa la kuendesha vita dhidi ya ufisadi,” alisema Kafulila katika taarifa yake.

Aidha, Kafulila alisema matokeo ya tafiti za hivi karibuni zilizofanywa na mashirika huru ya ndani na nje ya nchi zinaonyesha kiwango cha rushwa nchini kimeporomoka.

 

TAARIFA ZA KUZUIWA NA MKEWE KUJIUNGA CCM

Hata hivyo, MTANZANIA ilipomtafuta Kafulila, ili kujua uwepo wa taarifa ya kushindwa kujiunga na CCM juzi akidaiwa kuzuiwa na mkewe Jesca Kishoa ambaye ni mbunge wa viti maalumu Chadema, alizikanusha.

“Hakuna mwenye uhusiano wa mapenzi na siasa, ni tofauti, nilikuwa NCCR akiwa Chadema. Kwahiyo hakuna uhusiano wowote ule, hii ni nafasi yangu,” alisema.

Alipoulizwa wakati akiwa Chadema walikuwa pamoja na mkewe, alisema: “Siasa ni kile unachoamini, yaani unaamini katika nini… Dk. Slaa alikuwa Chadema mke wake alikuwa CCM, nini tatizo?

“Na alikuwa anaonyesha kupambana na rushwa kuliko mwanasiasa yeyote. Na ukisema alikuwa anamwibia siri mumewe si kweli, yaani diwani anaweza akajua siri za chama kikubwa kama CCM? Hata kwa akili ya kawaida tu diwani anaweza akajua siri za ngazi ya taifa?”

Alipoulizwa kuhusu hatima ya mke wake kama naye ataamua kuondoka Chadema au la, alisema atafutwe mwenyewe kwani naye ana msimamo wake wa kisiasa.

 

ALIVYOKUWA CHADEMA

Kafulila ambaye aliwahi kuwa Ofisa Habari wa Chadema kabla hajatimkia NCCR-Mageuzi mwaka 2009, baada ya kuhama mwaka huo, aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, alidai kuondoka kwake hakukuwa na athari yoyote kwani alikuwa sisimizi tu ndani ya chama hicho.

Hatua hiyo aliichukua baada ya kuwatuhumu Mwenyekiti Freeman Mbowe na Dk. Slaa kuwa wanaendesha chama hicho kibabe na kwamba katika uongozi wao mbovu, wamekuwa na matumizi mabaya ya fedha za ruzuku.

Kutokana na hali hiyo, kulikuwa na tetesi kwamba kama angeendelea kuwa ndani ya Chadema, basi jina lake lisingepitishwa kwani alitaka kugombea ubunge katika Jimbo la Kigoma Kusini, mwaka 2010.

Kwa mujibu wa Kafulila kwa wakati huo, alidai kwamba chuki ya Mbowe na Dk. Slaa ndiyo ilimwondoa Chadema baada ya kuhoji matumizi ya fedha za chama, zikiwamo Sh milioni 35 za ruzuku ambazo wakati huo haikujulikana zilipo.

 

NCCR-MAGEUZI

Akiwa katika chama cha NCCR-Mageuzi, Kafulila alifanikiwa kushinda ubunge Jimbo la Kigoma Kusini hadi mwaka 2015.

Katika harakati zake ilidaiwa Kafulila na wenzake walijaribu kupanga mkakati kumpindua Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia wakimtaka kujieleza kuhusu kukidhoofisha chama na kuwa kibaraka wa CCM.

Hata hivyo, jaribio hilo lilifeli na kuishia kuvuliwa wadhifa wa Katibu Mwenezi wa chama hicho, huku akifukuzwa uanachama na alikimbilia mahakamani kupinga uamuzi huo.

 

MAPAMBANO BUNGENI

Akiwa bungeni, Kafulila alijizolea umaarufu, hasa baada ya kuibua sakata la uchotwaji wa fedha kwenye akaunti maalumu ya Tegeta Escrow, lililosababisha mvutano mkali baina yake na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema.

Werema alimfananisha Kafulila na ‘tumbili’, akidai kuwa hakuwa anajua anachokisema.

Katika majibizano hayo bungeni, yaliyosababisha Bunge kusimama kwa muda, Kafulila alijibu mapigo kwa kumwita Jaji Werema ‘mwizi’, huku akitaka uchunguzi ufanyike ili ifahamike nani ni tumbili na nani ni mwizi.

Aidha, Kafulila aliwalipua kwa kuwataja kwa majina baadhi ya viongozi wa dini na Serikali, akidai walipokea mgawo wa fedha hizo za Escrow.

 

AREJA CHADEMA

Desemba mwaka jana, Kafulila alitangaza kuhama NCCR-Mageuzi na kuhamia Chadema kwa madai kuwa chama hicho hakina mwelekeo wa kuleta mabadiliko na kwamba anahamia katika chama kinachojipambanua kimkakati na mipango kuleta mabadiliko ya kweli.

Hata hivyo, Kafulila alidaiwa kuhama NCCR-Mageuzi baada ya kushindwa kutetea ubunge wake wa Kigoma Kasini mwaka 2015 licha ya kupambana mahakamani kudai haki yake.

Juzi Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (Bavicha), Patrobas Katambi na Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Lawrance Masha walitangaza kujiunga na CCM.

Kutoka ACT-Wazalendo waliojunga na CCM ni aliyekuwa mshauri wa chama hicho ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo, aliyekuwa Katibu Mkuu Samson Mwigamba, Mshauri wa Sheria, Albert Msando na aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu, Edna Sunga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles