24.2 C
Dar es Salaam
Sunday, April 14, 2024

Contact us: [email protected]

MRITHI WA MUGABE ATUA IKULU

HARARE, ZIMBABWE


SIKU moja baada ya Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, kujiuzulu muda mfupi kabla ya Bunge kuanza kujadili hoja ya kumtoa madarakani kwa nguvu na kumshtaki, Emmerson Mnangagwa, anayetarajiwa kurithi nafasi yake, amewasili Harare na kwenda moja kwa moja Ikulu.

Msemaji wa wa Chama cha ZANU-PF, Larry Mavhima, jana alisema: “Awali alikuwa awasili kwenye Uwanja wa Jeshi la Anga Manyame mjini Harare saa 10 jioni, lakini akawasili saa 8.30 za jioni.”

Mnangagwa (75), anayefahamika kwa jina la utani kama Mamba, ataapishwa kesho, siku tatu baada ya Mugabe (93) kujiuzulu wadhifa wake, ikiwa ameongoza Zimbabwe kwa miaka 37.

“Amekutana na Kamati Kuu ya ZANU-PF katika Uwanja wa Jeshi la Anga Manyame. Ameondoka kuelekea Ikulu ambako anapewa taarifa zaidi. Sherehe za kumwapisha ni Ijumaa,” alisema Mavhima.

 

SPIKA AELEZA UTARATIBU KIKATIBA

Mapema jana, Spika wa Bunge, Wakili Jacob Mudenda, alizungumza na waandishi wa habari na kueleza namna ambavyo mrithi wa Mugabe anapaswa kupatikana kwa mujibu wa Katiba.

Mudenda alisema Chama cha ZANU-PF kimemjulisha rasmi kwa mujibu wa Katiba kuwa, kimemteua Mnangagwa kuchukua nafasi ya Mugabe ya Rais wa Zimbabwe.

Alisema Bunge pia limemjulisha Katibu Mkuu Kiongozi wa Ofisi ya Rais na Baraza la Mawaziri, Dk. Misheck Sibanda, kuhusu uteuzi wa Mnangagwa ili aandae mchakato wa kumwapisha kama rais wa Zimbabwe.

Spika Mudenda alisema kuwa Dk. Sibanda anafanya kila linalowezekana ili hafla ya kumwapisha Mnangagwa ifanyike kesho kwa mujibu wa Katiba.

Katiba ya Zimbabwe inataka rais mpya aapishwe saa 48 tangu kujiuzulu kwa mtangulizi wake.

Makamu huyo wa rais wa zamani, alikuwa akitarajia kurudi nyumbani jana. Maelfu ya wafuasi wake walikuwa wakisubiri kwa hamu katika Uwanja wa Jeshi la Anga Manyame mjini Harare.

 

ZUMA AMPONGEZA MNANGAGWA

Akiwa nchini Afrika Kusini alikokimbilia baada ya kuvuliwa wadhifa wake wa Makamu wa Rais, Mnangagwa alikutana na Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, ambaye alimpongeza.

Zuma amekuwa kiongozi wa kwanza kumpongeza uso kwa uso Mnangagwa kwa kumrithi Mugabe. Viongozi hao walikutana katika Ikulu ya Afrika Kusini.

Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Zimbabwe (ZBC), baada ya kukutana na Zuma mjini Pretoria jana, Mnangagwa alielekea Uwanja wa Ndege wa Lanseria jijini Johannesburg tayari kupanda ndege kuelekea Harare.

 

KUONGOZA HADI SEPTEMBA 2018

Kwa mujibu wa ZBC, Mnangagwa ataapishwa kesho kuwa rais wa mpito wa Zimbabwe hadi Uchaguzi Mkuu utakapofanyika Septemba mwakani.

Jumapili iliyopita, Mnangagwa aliteuliwa kuwa Rais wa ZANU-PF baada ya chama hicho tawala kumfukuza Mugabe.

Juzi jioni, Mugabe alitangaza kujiuzulu nafasi yake ya urais, hatua iliyohitimisha utawala wake wa miaka 37, baada ya jeshi kuchukua udhibiti wa madaraka kwa siku kadhaa, bila ya kumwaga damu.

Mugabe, ambaye awali alipuuza miito ya kumtaka ajiuzulu, alichukua hatua hiyo baada ya fedheha ya mawaziri wake 17 kumsusa kikaoni na kushuhudia wabunge wa chama tawala na upinzani wakijitokeza kwa wingi bungeni ili kumng’oa.

Hatua ya Mugabe kujiuzulu ilipokewa kwa shangwe kubwa na nderemo bungeni, huku Wazimbabwe wakiimba na kucheza katika mitaa mbalimbali ya nchi hiyo.

Spika Mudenda, ndiye aliyesoma barua ya Mugabe kujizulu urais, wakati wa kikao maalumu cha Bunge ambacho kilikuwa kimeanza mchakato wa kisheria kumwondoa madarakani.

Mnangagwa alifukuzwa kazi mapema mwezi huu baada ya kutuhumiwa kwa kutokuwa mwaminifu na utovu wa nidhamu.

Hata hivyo, hatua hiyo iliyolikasirisha jeshi, ilichukuliwa kama njia ya kumwezesha mke wa Mugabe, Grace, kuwa mrithi wa kiti cha urais.

 

JESHI KUMSHTAKI GRACE?

Wakati hayo yakitokea, hatima ya kiongozi huyo mkongwe na mkewe Grace, ambao wamejichimbia katika hekalu lao la kifahari, haijajulikana.

Baadhi ya wanafamilia na walinzi wa Mugabe, waliuambia mtandao wa MailOnline kuwa jeshi limejiandaa kumwachia Mugabe aondoke nchini bila kumgusa, lakini lina mtazamo tofauti kuhusu mkewe.

Kwa mujibu wa watu hao wa karibu na Mugabe, majenerali wa jeshi wanasisitiza kumsamehe Mugabe, lakini si Grace. Wanataka akabiliwe na mashtaka.

Mmoja wa walinzi alisema: “Suala la Grace ndilo zito zaidi. Msimamo wa majenerali wa jeshi ni kumfungulia mashtaka kwa uhalifu wake, ikiwamo utakasishaji wa fedha, kujitwalia mali za umma na kuingilia shughuli za Serikali.”

 

MUGABE ADHOOFIKA

Mugabe anasemekana amekumbwa na msongo kiasi cha kushindwa kuinua miguu wakati akitazama kwenye televisheni Wazimbabwe kuanzia bungeni hadi mitaani wakishangilia hatua yake ya kujiuzulu.

Mmoja wa walinzi wa Mugabe aliyeomba kuhifadhiwa jina alisema: “Amezama kwenye msongo kiasi kuwa anashindwa kutembea. Anaburuza miguu.

“Kuhusu Grace, amegoma kutoka nje kupunga upepo. Wote wanafahamu wamefikia mwisho wa enzi na wamejikuta katika msongo. Wasiwasi wao mkubwa ni nini kitawakumba wao na familia zao.”

Mmoja wa wanafamilia wa Mugabe alisema: “Bob amekuwa katika maombi mazito na Padri Mukonori na familia. Anajisikia kuchanganyikiwa kwa kuona taifa zima linashangilia kujiuzulu kwake.”

Padri Fidelis Mukonori, ndiye aliyekuwa mtu wa kati wakati wa mazungumzo baina ya Mugabe na jeshi na ndiye aliyemshawishi aache mgomo wa kula, kuoga na kuzungumza mwishoni mwa wiki iliyopita.

Juzi, Mukonori, ambaye amekuwa baba wa kiroho wa Mugabe tangu miaka ya 1970, alienda kumfariji mshirika wake huyo wakati akichukua uamuzi wa kujiuzulu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles