CHRISTOPHER MSEKENA
MCHAKATO wa kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), umezua gumzo wiki hii mara baada ya mastaa kibao waliotia nia kuwania ubunge kuondolewa kwa kupigiwa kura chache na wajumbe.
Ni Babu Tale pekee ndio mtu wa burudani aliyefanikiwa kupenya katika mchakato huo kwa kuibuka mshindi baada ya kupata kura za maoni 318 katika Jimbo la Morogoro Vijijini Kusini Mashariki.
Hapa nakupa sababu kadhaa zilizofanya mastaa wengi waangukie pua katika kura hizo za maoni licha ya ukubwa wa majina yao kwenye tasnia ya burudani.
WENGI SIO WENYEJI MAJIMBONI
Itoshe kusema kwamba asilimia kubwa ya wasanii waliotia nia ya kugombea ubunge kwenye majimbo hasa yale yaliyopo nje ya Dar es Salaam sio wenyewe wa maeneo hayo licha ya kuwa kiasili wanatokea huko.
Mastaa wengi wanaishi na kufanya shughuli zao Dar es Salaam, hivyo walipotangaza nia ya kutaka ubunge maeneo hayo mbele ya wajumbe walionekana ni wageni wenye njaa ya uongozi kwenye majimbo yasiyo yao.
Mfano mwigizaji Steve Nyerere, ana asili ya Iringa ila alipoulizwa na wajumbe jimbo la Iringa Mjini lina mitaa mingapi akabaki anajiuma uma, kwa sababu kiukweli ni mgeni wa maeneo hayo licha ya kuwa ana asili ya Mkoa huo.
WAJUMBE WENGI HAWAPO MTANDAONI
Laiti wajumbe wote wangekuwepo mtandaoni na kuona ukubwa wa mastaa waliotangaza nia ya kugombea ubunge kwenye majimbo yao basi wangewapa kura za ndio ila bahati mbaya wajumbe wengi hawapo Instagram na wala sio mashabiki wa hizo filamu na muziki.
Hivyo walichokuwa wanaangalia zaidi ni ubora wa sera na mtu ambaye wanaona kabisa atawavusha salama na sio ukubwa wa majina ndio maana mastaa wengi wakapigwa chini licha ya ustaa wao.
MASTAA WENGI HAWANA ALAMA MAJIMBONI
Kama utakuwa mfuatiliaji mzuri wa harakati za Babu Tale utagundua mara nyingi amekuwa akienda Morogoro Vijijini na kushirikiana na wananchi kwenye mambo mbalimbali.
Katika miaka mitano iliyopita, Babu Tale alikuwa hakauki jimboni kwake, hata kama atakuwa bize na shoo za msanii wake, Diamond, ila atatenga muda wa kwenda Morogoro Vijijini kuacha alama kwa kushirikiana na wananchi kwenye matukio muhimu ndio maana imekuwa rahisi kwake kupata kura nyingi tofauti na mastaa wengine ambao wamerudi majimboni kipindi cha uchaguzi bila kuwa na alama yoyote waliyowahi kuiacha.
KUJIAMINI KUPITA KIASI
Mastaa wengi walichukua fomu wakiamini watapita bila shida kwa kuwa wanafahamika na wana mashabiki wengi ndio maana hakuna aliyedhani kama ataangukia pua.
Walijiamini kupita kiasi, wakasahau kuwa umaarufu si chochote mbele ya wajumbe wanaotaka mbunge wao ajue matatizo na changamoto zikizopo ndani ya Jimbo husika na sio umaarufu ambao haina faida jimboni.