30.5 C
Dar es Salaam
Thursday, May 26, 2022

Wanamichezo wamlilia Mkapa

WINFRIDA MTOI-DAR ES SALAAM

TANZANIA imepata pigo zito! Ni baada ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa kufariki usiku wa kuamkia jana jijini Dar es Salaam.

Hayati Mkapa, aliyezaliwa mwaka 1938, atakumbuka na Watanzania na mataifa mbalimbali ulimwenguni kutokana na kuwahi kushika wadhifa wa urais wa Tanzania, pia mwanadiplomasia aliyekuwa na mahusiano mazuri na viongozi wengi duniani.

Tofauti na siasa, Mkapa hakuwa nyuma katika harakati za kuendeleza michezo na  ameacha alama kubwa hapo nchini ikiwemo kujenga ya uwanja wa kisasa wa soka ambao ndio uwanja wa Taifa na  uliobeba jina lake.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, mwili wa Rais huyo mstaafu utaaagwa Julai 29, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kutokana na mchango wake katika michezo, kifo chake kimewaguza wanamichezo wengi nchini, wakiwamo wachezaji, viongozi wa klabu na mashirikisho.

TFF

Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania(TFF), Wallace Karia, amepokea taarifa za msiba huo kwa masikitiko makubwa na kusema kuwa watamkumbuka kwa kujenga Uwanja wa Taifa.

 “Katika soka Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Mh. Benjamin William Mkapa, ataendelea kukumbukwa siku zote kwa kujenga uwanja unaojulikana kwa jina la Benjamin Mkapa, unaotufanya kutembea kifua mbele katika Ukanda wa Afrika Mashariki,” alisema Karia.

Yanga

Uongozi wa Klabu ya Yanga nao umetuma salamu za rambirambi kwa Watanzania na familia ya Hayati Mkapa, kutokana na msiba huo.

“Tutamkumbuka kwa mengi, Uwanja wa Taifa aliotujengea lakini pia kwetu Yanga alikuwa shabiki wetu ambaye mara zote alikuwa akitoa ushauri kila anapohitajika,”alisema Mwenyekiti wa Yanga Dk. Mshindo Msolla.

Simba

“Uongozi wa Klabu ya Simba umepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Rais wa Awamu ya Tatu, Mhe. Benjamin William Mkapa, tunatoa pole kwa familia, ndugu, marafiki na Watanzania wote kwa msiba huu mkubwa kwa Taifa letu,” ilisema taarifa ya Simba iliyowekwa katika mtandao wao.

Mdau wa masumbwi, Emmanueli Mlundwa

Alisema kifo cha Mkapa, kimemgusa kwa kiasi kikubwa kwa sababu kuna mambo mengi amemsapoti katika maisha yake ya ngumi za kulipwa.

Anasema mchezo ngumi hasa za kulipwa una deni kuwa la kumuenzi Mkapa kwakua alikuwa kiongozi mkubwa wa kwanza kuusapoti wakati huo akiwa Waziri wa Mambo ya Nje.

“Pambano la kwanza la ngumi za kulipwa nchini, lilichezwa mwaka 1981 na Mheshimiwa Mkapa ndiye alikuwa mgeni rasmi, nilicheza mimi na Ally Mohammed.

“Nilikuwa bondia wa kwanza kuingia katika ngumi za kulipwa na kipindi hicho nilikuwa naonekana tofauti, niliambiwa nimeingiza mchezo wa kibepari nchini, lakini Mzee Mkapa aliwashawishi Watanzania kuona ngumi hizo ni burudani na starehe kama nyingine.

“Hata nilipostaafu ndiye aliyeidhinisha mimi nikaenda kusoma shahada ya ‘Computer Science’ nchini Uingereza mwaka 1994 baada ya kumuomba kuwa nina vigezo vyote,” alifichua Mlundwa.

Japhet Kaseba

Bondia Kaseba alisema Mkapa alikuwa na mchango mkubwa katika kuutambulisha mchezo wa ngumi za kulipwa nchini.

“Ni mtu pekee aliyeshawishi mchezo wa ngumi za kulipwa kuchezwa nchini kipindi akiwa Waziri wa Mambo ya Nje, kwa sababu zamani ngumi za kulipwa zilikuwa zinajulikana kama mchezo wa kibepari.

“Mwaka 1981, alikuwa mgeni rasmi katika pambano la ngumi za kulipwa kati ya Emmanuel Mlundwa na Ally Mohammed lililofanyika ukumbi wa Diamond Jubilee, kuanzia hapo watu wakaupokea mchezo huo na hadi sasa unaendelea kupeperusha vizuri bendera ya Tanzania,” alisema Kaseba.

TAVA

Chama cha Mpira wa Wavu Tanzania(TAVA), kupitia Katibu Mkuu wake, Alfred Serengia alisema  watamkumbuka Mkapa kwakua kiongozi aliyekuwa na  mtazamo  tofauti na mchango wake katika sekta ya michezo.

“Kitu kikubwa alichokiacha ni Uwanja wa Taifa uliojengwa katika kipindi chake na hautaishia hapo kwa sababu  unatakiwa kuendelea kwa awamu  hadi kufikia ujenzi wa uwanja wa michezo ya ndani ambao tutatumia sisi wachezaji wa mpira wa wavu.

“Ili kumuenzi ni kuhakikisha ujenzi wa viwanja vyote vyote vilivyopo katika ramani ya kuanzia uwanja wa Taifa, vinakamilika kujengwa,”alisema Selengia.

Namungo

Katibu Mkuu wa Klabu ya Namungo, Ally Seleman alisema wamepokea msiba huo kama Watanzania wote, lakini wao umewagusa zaidi kwa sababu unahusu familia ya watu wa mikoa ya Kusini ambao timu yao inapatikana.

“Pamoja na mambo mengi ya michezo Mzee Mkapa aliyofanya, sisi Namungo tumesikitika zaidi kumpoteza mwenzetu wa Kusini, tunamuombea Mwenyezi Mungu amuweke mahali pema peponi,” alisema Seleman.

AS Roma

Klabu ya soka ya AS Roma ya Italia nayo imeguswa na kifo hicho baada ya kuandika katika ukurasa wao wa waTwitter wa Kiswahili kuwa: “Tumepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu wa Tanzania, Mhe. Benjamin William Mkapa. ASRoma inatoa pole kwa familia yake, ndugu zake, marafiki na Taifa la Tanzania kwa ujumla. 

Wachezaji

Katika mitandao yao ya kijamii, wachezaji wa soka wa Kitanzania, wameweka picha ya rais huyo kama ishara ya maombolezo na kuandika jumbe mbalimbali.

Mingoni mwa wachezaji hayo ni Mbwana Samatta anayechezea Aston Villa ya England aliyeandika: “Pumzika kwa amani mzee Mkapa.”

 Simon Msuva anayezea Difaa El Jadida, amendika ‘Rest In Peace’.

Mnyarwanda Haruna Niyonzima aliandika: “Inalilah wa inailah lajiuni, Rest in Paradise baba, pole pia kwa Watanzania wote.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
192,358FollowersFollow
541,000SubscribersSubscribe

Latest Articles