31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

SABABU ZA KUSITISHWA BOMOABOMOA NYUMBA 300 DAR

Na MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

RAIS Dk John Magufuli amezuia ubomoaji wa nyumba zaidi ya 300 zilizojengwa kwenye eneo tengefu la Bonde la Makamba Kata ya Toangoma wilayani Temeke,  Dar es Salaam.

Tamko hilo lilitolewa jana na Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda   kwa niaba ya Rais Magufuli, alipotembelea eneo hilo.

Makonda alisema Rais Magufuli  alimwagiza awatangazie wananchi hao kuwa amesitisha hatua hiyo kwa sababu halikufuata utaratibu wa Serikali.

Tamko hilo limetolewa ikiwa ni siku chache baada ya Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaviva kuwataka wananchi waliojenga kwenye eneo hilo kuondoka kabla ubomoaji huo haujaanza.

Siku hiyo, DC  aliitisha kikao na wananchi na kubaini aliyehusika kuwauzia viwanja katika maeneo hayo ambayo si salama kwa makazi, ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Masaki Kata ya Toangoma, Hassan Bakari.

Makonda alisema ingawa tamko la kubomolewa nyumba hizo za Toangoma lilitolewa na wakurugenzi wa manispaa,  lazima taratibu za  maandishi zifuatwe kwa kuijulisha ofisi ya mkuu wa mkoa.

“Hata kama tamko hilo limetolewa na watumishi wa mkoa, mfano wakurugenzi wa manispaa au wakuu wa wilaya, lazima Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ipate taarifa na iridhie bomoabomoa hiyo.

“Na hata kama taarifa zimetoka wizarani inapaswa taratibu za  maandishi zifuatwe kwa kujulisha ofisi ya mkoa.  Haiwezekani mtu atoe tamko la kuvunja nyumba bila mkoa kujua, hilo haliwezekani.

“Nimezungumza na Rais Dk. Magufuli akaniuliza endapo nina taarifa ya   ubomoaji wa nyumba hizo nikamweleza sina taarifa hizo zaidi ya ubomoaji wa nyumba zilizo kwenye hifadhi ya barabara ya kuanzia Ubungo kwenda Kimara na Mbezi ambao unafanywa kwa ajili ya upanuzi wa barabara ya Morogoro,” alisema Makonda.

Alisema baada ya kumweleza Rais kuwa hana taarifa hizo, alimwagiza awaeleze wananchi hao kuwa hatua hiyo  imesitishwa.

“Pia ametaka wananchi wanaoishi katika maeneo halali waachwe kwa sababu amepata taarifa kuwa huenda hatua hiyo ingekwenda mbali zaidi mpaka kwa wananchi wasiohusika,” alisema na kuongeza:

“Rais amenieleeza niwaambie kwamba hamkumchagua ili awabomolee nyumba, mlimchaguali awaletee maendeleo ambayo ni pamoja na kuwa na makazi ya kudumu na mlimchagua aboreshe makazi yenu. Akaniambia niwafikishie ujumbe wana Toangoma”.

Vilevile, mkuu huyo wa mkoa alipiga marufuku hatua yoyote ya kubomoa nyumba bila ofisi yake kupewa taarifa na kuridhia.

Aliwataka wananchi na wakazi wote wa Dar es Salaam kuzingatia sheria na kutovamia maeneo au kuuziwa viwanja na matapeli.

Maeneo mengine

Hivi karibuni Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi ya Mazingira (NEMC) lilitangaza kubomoa nyumba zaidi ya 17,000 zilizojengwa katika hifadhi ya Bonde la Mto Msimbazi wilayani Ilala, Dar es Salaam.

Ofisa Mipango Miji wa   NEMC, Dk. Charles Mkalawa aliwaambia waandishi wa habari wiki iliyopita kuwa nyumba hizo ni miongoni mwa zilizowekewa alama ya X katika bomoa bomoa iliyositishwa mwaka jana.

Nyumba 300 za wakazi wa Kimara, Mbezi hadi Kibamba Dar es Salaam, zinaendelea kubomolewa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kupisha upanuzi wa barabara ya Morogoro.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles