24.7 C
Dar es Salaam
Saturday, April 13, 2024

Contact us: [email protected]

GIZA MIKOPO ELIMU YA JUU

*Ni 15,000 pekee walioomba ipasavyo

Na NORA DAMIAN -DAR ES SALAAM

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imesema kati ya wanafunzi 49,282 walioomba mikopo kujiunga na mwaka wa kwanza wa masomo katika taasisi mbalimbali za elimu ya juu nchini, 15,473 pekee ndio waliokamilisha taratibu zote, huku wengine 33,809 wakiwa bado.

Kutokana na hali hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul – Razaq Badru, alisema wamelazimika kuongeza muda wa maombi kutoka Septemba 4 hadi 11.

Katika mwaka ujao wa masomo,  HESLB inatarajia kutumia Sh bilioni 427 kutoa mikopo kwa wanafunzi 30,000 wa mwaka wa kwanza na 93,252 wanaoendelea na masomo yao kuanzia mwaka wa pili na kuendelea.

Akizungumza Dar es Salaam jana na waandishi wa habari, Badru alisema idadi hiyo ya wanafunzi walioomba mikopo ni ya hadi Agosti 29.

Akifafanua kasoro zilizo kwenye maombi ya wanafunzi 33,809, alisema baadhi yao nyaraka zao ikiwa ni pamoja na vyeti vya kuzaliwa, hazijathibitishwa na Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) na hazijagongwa mihuri na viongozi wa Serikali za mitaa kama inavyotakiwa.

Alisema wengine vyeti vyao vya taaluma vinatakiwa kuthibitishwa kwa kugongwa muhuri na sahihi za kamishna wa viapo, ama hakimu au wakili, jambo ambalo hawajafanya.

Badru alisema wengine ambao wamesoma kupitia wafadhili, wanatakiwa waambatanishe barua kutoka taasisi iliyowafadhili.

“Tunasisitiza kwa kila mwombaji kuambatanisha nyaraka muhimu zinazohitajika, zikiwamo zile zinazotakiwa kusainiwa na kamishna wa viapo na RITA,” alisema Badru.

Aidha, Badru amewasisitiza waombaji wa mikopo kuzingatia mwongozo uliotolewa na bodi, unaowataka kuambatanisha nyaraka zote zilizothibitishwa na RITA, makamishna wa viapo, mawakili na Serikali za mtaa na kuziwasilisha kwenye mtandao wa bodi.

Akifafanua zaidi juu ya waombaji hao 33,809, Msemaji wa bodi hiyo, Dk. Cosmas Mwaisoba, alisema wako baadhi ya wanafunzi ambao hawakuingiza taarifa zote kama inavyotakiwa.

“Unakuta mwingine amefanya ‘registration’ (usajili)’ akatoka, mwingine ameingiza taarifa zote akatoka, mwingine labla ame–‘attach’ (ameambatanisha) cheti cha kidato cha nne tu bado cha kuzaliwa.

“Kwahiyo hawajafikia hatua ya mwisho ya ku–‘submit’ (kukabidhi maombi yao), ndio hao tunasema wako katika hatua mbalimbali za kukamilisha maombi yao,” alisema Mwaisoba.

Akizungumzia namna mfumo huo unavyofanya kazi, alisema unamuhusisha mwombaji pekee na kuna maelekezo kwenye kila hatua.

“Sisi hatuongei na mwanafunzi ni yeye na ‘system’ (mfumo), yaani ukiingia ukimaliza hatua hii inakwambia hatua inayofuata ni hii, hadi utakapofika mwisho itakwambia.

“Na kwenye kila hatua akijisikia kutoka kuna sehemu ya kutokea, atakapoamua kurudi anaanzia alipoishia na kuendelea,” alisema.

Kaimu Mkurugenzi wa Utoaji Mikopo, Dk. Veronica Nyahende, alisema waombaji wengi hawasomi miongozo kama inavyopaswa, hivyo wanashindwa kuambatanisha viambatanisho muhimu.

“Kila mwombaji anatakiwa awe makini, asome kwa uangalifu na kurekebisha makosa yaliyojitokeza awali,” alisema.

MWAKA WA MASOMO 2016/17

Katika mwaka wa masomo 2016/17, wanafunzi waliodahiliwa walikuwa 58,000 na kati yao waliokidhi vigezo na kupatiwa mikopo walikuwa 25,717.

Kiasi cha fedha zilizoidhinishwa kwa ukopeshaji kilikuwa Sh bilioni 483 ambazo zilitarajiwa kunufaisha wanafunzi 119,012 ambao mbali na wa mwaka wa kwanza, wanafunzi 93,295 walikuwa ni wale wanaoendelea na masomo.

Katika mwaka huo, idadi kubwa ya wanafunzi walishindwa kuendelea na usajili vyuoni kutokana na kukosa mikopo, huku wanufaika wachache waliopatiwa mikopo wakilalamikia kuambulia kiasi kidogo kisichokidhi mahitaji muhimu ya wanafunzi vyuoni.

SIFA 10 ZA MWOMBAJI WA MKOPO

  • Awe Mtanzania
  • Awe ameomba kudahiliwa na chuo kikuu au taasisi ya elimu ya juu inayotambuliwa na Serikali
  • Asiwe mwanafunzi wa masomo ya jioni (part time student)
  • Asiwe na udhamini/ufadhili/msaada wa kifedha kutoka katika vyanzo vingine
  • Awe ameomba mkopo kupitia mfumo wa mtandao (OLAMS)
  • Awe amefaulu mitihani ya mwisho wa mwaka (wanaoendelea na masomo) na matokeo yake kuwasilishwa Bodi ya Mikopo na chuo chake
  • Awe amemaliza kidato cha sita au awe na sifa linganishi (kama diploma n.k) ndani ya miaka mitatu (2015/2016 – 2017/2018)
  • Awe na umri usiozidi miaka 30 wakati wa kufanya maombi
  • Ambao wazazi wao ni wakurugenzi au mameneja waandamizi katika kampuni binafsi zinazotambuliwa na mamlaka za mapato na usajili, hawatarajiwi kuomba mkopo
  • Ambao wazazi wao ni viongozi wa umma au kisiasa, wanaotajwa na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, hawatarajiwi kuomba mkopo.
- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles