NA RAMASHANI HASSAN, DODOMA
SERIKALI imesema upungufu wa watumishi ulisababisha kufungwa vyuo vitano vya ufundi kwa ajili ya watu wenye ulemavu.
Kauli hiyo iliitoa bungeni Dodoma jana na NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Vijana, Antony Mavunde wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Dk. Elly Macha.
Dk. Macha alihoji: ‘’Ni sababu gani zilizosababisha vyuo hivyo vitano vifungwe wakati kuna mahitaji makubwa ya watu wenye ulemavu kupata mafunzo ya ufundi.’’
“Je, serikali ina mpango gani wa kufungua haraka vyuo vilivyofungwa ili viendelee kutoa mafunzo ya ufundi kwa watu wenye ulemavu … serikali ina mkakati gani wa kujumuisha watu wenye ulemavu kwenye vyuo vyake vya VETA na FDC?”
Akijibu, Mavunde alizitaja sababu hizo kuwa ni upungufu wa watumishi na baadhi yao kustaafu na wengine kufariki dunia.
Alisema serikali ina nia ya dhati ya kuhakikisha watu wenye ulemavu nchini wanapata mafunzo siyo tu ya ufundi, bali ya aina nyingine yatakayokidhi mahitaji ya ajira na kuondoa utegemezi kwa watu wenye ulemavu.
Pia alisema serikali imewasilisha maombi maalum Hazina ya kuomba fedha za maendeleo kwa mwaka wa fedha 2017/18 ambazo zitatumika kufanya ukarabati na kuboresha miundombinu ya vyuo mbalimbali nchini.
“Vilevile, wizara imewasilisha IKAMA ya watumishi utaratibu wa kuajiri watumishi ufanyike mapema kuziba nafasi zilizo wazi,”alisema Mavunde
Naibu waziri alisema mkakati wa serikali ni kuwa na walimu wenye mbinu za kufundisha watu wenye ulemavu katika kozi ya ualimu MVTTC ambayo ipo Monduli inayohusu mbinu za kufundisha watu wenye ulemavu.
Alisema pia lengo la Serikali ni kukarabati miundombinu ya njia za kutembelea na majengo kuwapa fursa watu hao kushiriki katika mafunzo ya ufundi bila kikwazo.