29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

Sababu uhaba wa saruji zatajwa

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Ludovick Nduhiye amesema baadhi ya viwanda vinavyozalisha saruji nchini vilisimamisha au kupunguza viwango vya uzalishaji katika kipindi cha Oktoba na Novemba mwaka huu, hali iliyosababisha uhaba wa bidhaa hiyo.

Nduhiye alisema hayo baada ya kufanya ziara katika viwanda vinavyozalisha saruji, mawakala na wasambazaji nchini, ili kubaini hali halisi ya uzalishaji, usambazaji na mwenendo wa bei ya bidhaa hiyo.

Alisema katika ziara yake hiyo aliyoambatana na maofisa waandamizi toka Wizara ya Viwanda na Biashara, amebaini kati ya viwanda tisa vinavyozalisha saruji nchini kwa sasa, baadhi yake vilisimamisha au kupunguza viwango vya uzalishaji katika kipindi hicho ili kufanya matengenezo ya mitambo ya uzalishaji ‘clinker’ na saruji.

Nduhiye alifanya ziara hiyo ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alilolitoa jijini Dodoma baada ya kuapishwa na Rais Dk. John Magufuli kushika tena wadhifa huo.

Katika ziara yake, alitembelea Kiwanda cha Tanzania Portland Cement PLC kinachozalisha saruji ya Twiga, Lake kinachozalisha saruji chapa Nyati vilivyopo Dar es Salaam, Dangote kilichopo Mtwara na Kiwanda cha Saruji Mbeya kinachozalisha saruji ya Tembo. 

Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha Tanzania Portland Cement PLC, Alfonso Velez alisema wameendelea na uzalishaji wa saruji na kuisambaza kwa wateja wake kwa bei ile ile ya Sh 13,500 kwa mfuko wa saruji aina ya 32.5R na Sh 13,800 kwa saruji aina ya 42.5R.

Mkurugenzi huyo alieleza kuwa kwa sasa kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha wastani wa tani 160,000 kwa mwezi na takribani tani milioni 2.0 kwa mwaka. 

Wakala kutoka Kiwanda cha Portland Tanzania, Dipak Manilal Lal alisema mahitaji yameongezeka nchini na kuwa yeye anauza saruji yote anayoipata kwa siku kwa wateja wake.

Mkuu wa Idara ya Mikakati ya Kibiashara wa Kiwanda cha Lake  Ipn  Pathall alisema kuwa  uhaba wa saruji nchini ni dalili nzuri ya maendeleo ya kiuchumi yanayosababishwa na ongezeko kubwa la mahitaji ya bidhaa hiyo kuliko uzalishaji linalotoa changamoto kwa viwanda kuongeza uzalishaji ili kukidhi mahitaji ya soko.

Alisema kiwanda chake hakikusitisha uzalishaji na wala hakikupandisha bei ya saruji bali kimeendelea na uzalishaji ili kuendana na mahitaji ya wateja wake pamoja na miradi mikubwa yanayoongezeka kila siku.

Pathall alisema bei ya mfuko wa saruji imeendelea kuuzwa kwa Sh 12,710 kwa saruji aina ya 32.5R na Sh 13,500 kwa saruji aina ya 42.5R.

Mtendaji Mkuu wa Uzalishaji wa Kiwanda hicho, Biswajeet Mallik alisema  kwa sasa wanazalisha tani 50,000 kwa mwezi na 600,000 kwa mwaka na wanajipanga kuongeza uzalishaji ili kukidhi mahitaji ya soko linalokua kila siku.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, Alphayo Kidata alisema kuwa bei ya saruji kwa mfuko mmoja ilipanda kutoka Sh 13,500 hadi Sh 23,000. 

Alisema bei hiyo kwa sasa imeanza kushuka hadi Sh 14,000 na 15,000 kwa mfuko.

Waziri Mkuu Majaliwa aliamuru wakuu wote wa mikoa kukagua viwanda vyote vya saruji na kuwashtaki wamiliki watakaobainika wameficha bidhaa hiyo.

Akizungumza na wakuu hao katika mkutano wa video, Majaliwa alisema ukaguzi huo unapaswa pia kuhusisha mawakala wa uuzaji wa saruji na wauzaji wa bidhaa hiyo kote nchini.

Majaliwa alisema ripoti zilizowasilishwa kwake kutoka kwa wakuu wa mikoa zimeonyesha kuwa kulikuwa na uhaba wa saruji na ilikuwa ikiuzwa kwa bei ya juu.

Akizungumza muda mfupi baada ya kuapishwa na Rais Magufuli katika Ikulu ndogo ya Chamwino katika mji mkuu wa Dodoma, Majaliwa alisema; “kazi yangu ya kwanza kama Waziri Mkuu ni kuchunguza sababu ambazo zimesababisha kupanda kwa bei ya saruji.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles