Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA
WATU saba wamefariki dunia mkoani Dodoma kwa kuugua ugonjwa wa Kipindupindu, huku 329 wakiugua ugonjwa huo.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi mjini hapa, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. James Kiologwe alisema takwimu hizo ni kuanzia Oktoba 20, mwaka huu ambapo kwa Wilaya ya Mpwapwa wamefariki watu watatu huku 208 wakiugua.
Dk. Kiologwe alisema katika Wilaya ya Kongwa walifariki wagonjwa wawili huku 18 wakiugua ugonjwa huo, Chamwino 18 wakiugua na wanane kufariki dunia.
“Hizi ni takwimu za Oktoba ugonjwa wa Kipindupindu umetokea wilayani Kilosa kule ni mpakani na Mpwapwa na kulikuwa na bonde ambalo wananchi walikuwa wakijishughulisha na kilimo hivyo walikuwa wakishirikiana katika shughuli za kijamii ndio maana ugonjwa huo ukaingia Mpwapwa,”alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana alikuja na kampeni ya tokomeza Kipindupindu ambayo ilisaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza idadi ya wagonjwa kutokana na kutoa elimu kwa wananchi.
Dk. Kiologwe alisema mpaka sasa wagonjwa waliopo ni nane tu katika Mkoa wa Dodoma kutokana na kampeni hiyo iliyoanzishwa na mkuu wa mkoa.
Mganga Mkuu huyo alitoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kufuata taratibu za usafi katika kipindi hichi cha Sikukuu kwani ugonjwa huo kwa kiasi kikubwa husababishwa na uchafu.