Paris, Ufaransa
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema kuwa atazuru Rwanda mwisho wa mwezi Mei kufungua “Ukurusa mpya wa uhusiano” kati ya nchi hizo mbili.
Ziara yake itakuwa ya pili kwa rais wa Ufaransa tangu kutokea kwa mauaji ya halaiki nchini Rwanda mwaka 1994 – baada ya Rais Nicolas Sarkozy mwaka 2010.
Akizungumza mwisho wa mkutano wa Paris ulioangazia kufadhili Afrika, Bwana Macron alisema kuwa ziara yake itakuwa kwa ajili ya “ukumbusho, siasa, uchumi …na hatma yao.
“Pia tumekubaliana na Rais Kagame kufungua ukurasa mpya wa uhusiano wetu na kuendeleza miradi kadhaa…,” amesema Macron amesema.
Rais Paul Kagame, Jumatatu alikiambia chombo cha habari cha Ufaransa cha France 24, kuwa, “hatua kubwa imepigwa..pengine bila kusahau yaliyopita na wameweza kusonga mbele”.
Uhusiano kati ya nchi hizo mbili ulizorota kuanzia mwaka 2006 hadi 2009, baada ya majaji wa Ufaransa kutoa kibali cha kukamatwa kwa washirika wa karibu wa Bwana Kagame.
Hilo lilitokana na kudunguliwa kwa ndege iliyokuwa imewabeba marais wa Rwanda na Burundi Aprili mwaka 1994 – tukio ambalo lilisababisha mauaji ya halaiki.
Serikali ya Rwanda imekuwa ikishutumu mamlaka ya Ufaransa kwa jukumu lake ililotekeleza kwenye mauaji ya mwaka 1994 na kuwahifadhi waliotekeleza mauaji hayo.