KIGALI, RWANDA
KATIKA juhudi za kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona, Rwanda imezindua mashine ya kwanza iliyotengenezwa nchini mwake ambayo inawasaidia wagonjwa kupumua maarufu kama ventilator.
Ni mashine iliyotengenezwa na vijana wanane wa Chuo Kikuu cha Rwanda kwa msaada wa wakufunzi wao na lengo likiwa ni kuitua Serikali mzigo wa kuagiza mashine kama hizi kutoka nje.
Kwa kawaida mashine hii inayomsaidia mgonjwa aliyeko mahututi kupumua wenyewe wanasema thamani yake ni Dola 10,000 za Marekani (karibu Sh. milioni 23.1) inaponunuliwa kutoka nchi za nje.
Hata hivyo mabingwa walioitengeneza walisema kwamba kwa sasa kutokana na dunia kukabiliwa na tatizo la Covid-19 bei ya mashine hii imepanda hadi Dola 20,000 za Marekani (karibu Sh. Milioni 46.3).
Mkufunzi katika Chuo Kikuu cha Rwanda, Profesa Stephen Rulisa, alisema licha ya kuongoza mchakato wa kuitengeneza mashine hii ni vijana wake walioitengeneza.
“Sisi tunawapa kazi ya kisayansi, tunawapa mawazo kama haya kisha wao hukaa kwenye maabara kama hapa na tunafurahi kwamba hatimaye wanafanya jambo kama hili,” alisema Profesa Rulisa.
Wahandisi vijana waliotengeneza mashine hiyo walisema haikuwa kazi ndogo lakini iliwezekana na inawezekana kuzitengeneza nyingine nyingi za aina hiyo, lakini hilo litategemea pale tu serikali itakapowajibika zaidi.
“Tunachohitaji ni ushirikiano wa ngazi zote ili tutengeneza mashine nyingi na kuziweka sokoni kwa sababu zinahitajika kwa wingi,” alisema Costa Uwitone, mmoja wa wanafunzi walioshiriki kutengeneza mashine hiyo.
Wakati huo huo, pia viwanda nchini Rwanda vimeanza kutengeneza barakoa ambazo Serikali inasema kutokana na hilo, iko mbioni kumtaka kila mwananchi kuiva popote anapokuwa ili kujikinga dhidi ya virusi vya corona.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya tiba, Dk. Nsanzimana Sabin alisema barakoa zina ubora kama zile zinazoingizwa nchini kutoka nje.
“Tunatambua bei ya barakoa na ubora wake kwa kuzingatia afya zetu kama binadamu, hatupendi kutengeneza vitu vyenye viwango vya chini hapana, ila barakoa zina viwango bora na pia bei ambayo kila mmoja anaweza kumudu,” alisema.
Kwa mara ya kwanza idadi ya wagonjwa wanaopona na kuruhusiwa kutoka nchini Rwanda imepanda kuliko ile ya wagonjwa wanaoendelea kulazwa.