Bibi wa miaka 68 ajifungua mapacha Nigeria

0
1091

 ABUJA, NIGERIA

MWANAMKE mwenye miaka 68 nchini Nigeria amejifungua watoto pacha kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Lagos na kuwaacha wengi na mshangao.

Akitoa tangazo hilo Jumapili iliyopita, Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la chuo hicho, Profesa Wasiu Adeyemo, alisema mwanamke huyo alijifungua kwa njia ya “upasuaji baada ya wiki 37 za ujauzito”.

Mume wa mwanamke huyo, Noah Adenuga aliiambia BBC kuwa iliwachukua miaka 43 kutafuta mtoto na kwamba waliwahi hata kutumia njia ya kuanguliwa kwa mayai yake ya uzazi nje ya mfuko wa uzazi na baadae kuchanganywa na mbegu za kiume na kisha kupandikizwa ndani ya mfuko wake wa uzazi ama IVF kwa lugha ya kitaalamu mara kadhaa bila mafanikio. Hata safari hii pia mafaniko yao yamepitia njia hiyo ya IVF.

Mama na watoto wake wachanga wanaendelea vema na kwa sasa wameruhusiwa kuondoka hospitalini.

Adenuga alisema safari yao ya kutafuta watoto iliwapeleka hadi nchini Uingereza na kuwarejesha tena Nigeria na imani yao iliwafanya waendelea kuishi pamoja kwa miaka mingi bila watoto. Adenuga (70) pia alisema kuwa alipokea jumbe kutoka kwa kikundi cha madaktari wa uzazi ambao walisema matendo yake ni kijinga.

Daktari aliyemuhudumia mama huyo, Adeyemi Okunowo alitaja kuzaliwa kwa watoto hao ‘muujiza’ lakini pia alisema mume huyo na mke wake walijiweka hatarini kwa kuamua kusaka mtoto katika umri wao mkubwa.

Utawala wa hospitali ulisema kuwa usingewapatia huduma ya IVF katika umri wa miaka 68 lakini waliamua kumlaza tu kwa sababu ulikua ni wajibu wao wa kimatibabu.

Hii si mara ya kwanza kwa mwanamke kikongwe kujifungua duniani.

Mwanamke mwingine nchini India, Mangayamma Yaramati alijifungua watoto pacha Septemba mwaka jana pia akiwa na umri wa miaka 73, huko katika jimbo la Kusini la Andhra Pradesh. Bibi huyo pia alitungishwa mimba kupitia njia ya IVF.

Mangayamma Yaramati alisema kuwa yeye na mumewe ambaye alikua na umri wa miaka 82, walikuwa wakati wote wakitaka kuwa na watoto lakini hawakuwahi kupata mtoto hadi walipotumia njia ya IVF.

“Tulijaribu mara nyingi kupata watoto na tukawatembelea madaktari wengi, kwa hiyo hiki ni kipindi cha furaha zaidi maishani mwangu,” alisema Yaramati. Aliongeza kuwa alihisi kutengwa na jamii na wanakijiji wenzake na mara kwa mara amekuwa akitengwa katika mikusanyiko kwasababu yeye hakuwa mama.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here