24.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 17, 2021

Hotuba ya kwanza ya upinzani yapenya bungeni

RAMADHANI HASSAN-DODOMA

KAMBI Rasmi ya Upinzani Bungeni, imefanikiwa kuwasilisha hotuba ya kwanza katika mkutano huu wa 19 baada ya tatu kukataliwa kwa madai ya kukiuka taratibu za Bunge.

Hotuba zilizokataliwa ni ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni juu ya bajeti ya Waziri Mkuu, hotuba ya Ofisi ya Makamu wa Rais na ile ya Ofisi ya Rais Utumishi.

Jana msemaji wa kambi hiyo katika Wizara ya Madini, Joseph Haule, alifanikiwa kusoma hotuba yake huku akisema sababu mojawapo ya kushuka kwa thamani ya madini ya Tanzanite ni kuwa na shaka ya uwekezaji na kuondoka kwa wanunuzi wakubwa wa madini hayo.

Akiwasilisha maoni hayo, alisema biashara ya madini ya Tanzanite inadorora na yanaendelea kushuka bei na wachimbaji wengi wanakata tamaa.

“Zipo taarifa kwamba kabla ya corona virus pandemic madini ya Tanzanite yalishashuka bei kwa zaidi ya asilimia 50, lakini sasa madini hayo yameshuka kwa zaidi ya asilimia 70, kitendo hiki kimepelekea hofu iliyotanda kwenye madini ya Tanzanite kuwa kubwa sana.

“Uchimbaji wa madini ya Tanzanite unawezekana tu pale ambapo madini haya yatakuwa na thamani kubwa kwani gharama za uchimbaji ni ghali sana kulinganisha na madini mengine ya vito.

“Ni bahati mbaya kuwa Serikali haitambui kuwa kutotabirika kwa mazingira ya biashara kunaua biashara kuliko hata wingi wa kodi pamoja na ukosefu wa amani kwa wafanyabiashara.

“Mwenendo wa Mkuu wa Mkoa wa Manyara na maofisa madini kuwanyanyasa na kuwatisha wafanyabiashara imeondoa kabisa morali ya biashara hii,” alisema Haule.

Alisema kutokana na mwenendo huo, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuwatambua wafanyabiashara wote nchini wakiwemo wafanyabiashara ya madini kama wadau wakubwa wa biashara nchini.

Aidha, alisema ujengwe utamaduni wa migogoro ya kodi iendeshwe na sheria za kodi tofauti na hali ya sasa ambayo Takukuru na Ofisi ya DPP huichukulia migogoro ya kikodi kama makosa ya utakatishaji fedha na uhujumu uchumi.

MAONI YA KAMATI

Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Nishati na Madini, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dunstan Kitandula, alisema wanaishauri Serikali kupitia Wizara na Tume ya Madini kushirikiana kwa karibu na mamlaka za mikoa ili kuainisha maeneo stahiki yenye mwamko na hadhi za kibiashara ili kutumika kama masoko.

Kitandula alisema kumekuwepo na changamoto mbalimbali zinazokabili masoko ya madini kwa wafanyabiashara wa madini katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Alisema changamoto hizi zimejumuisha masoko kutokuwa kwenye maeneo stahiki ya kibiashara, baadhi ya majengo ikiwemo ya Serikali kuwatoza kodi kubwa wafanyabiashara, gharama kubwa za uendeshaji masoko hayo na mlolongo wa kodi.

“Hivyo basi, Kamati inaishauri Serikali kupitia Wizara na Tume ya Madini kushirikiana kwa karibu na mamlaka za mikoa ili kuainisha maeneo stahiki yenye mwamko na hadhi za kibiashara ili kutumika kama masoko,” alisema Kitandula.

Aidha, kushirikiana na mamlaka nyingine zinazomiliki majengo yanayotumika kama masoko ya madini kupunguza kodi ili kuwaondolea wafanyabiashara wa madini mzigo mkubwa wa gharama za uendeshaji.

“Sambamba na hili, kupunguza changamoto za mlolongo wa kodi kwa wafanyabiashara kutachochea ufanisi wa dhana hii njema ya masoko ya madini na kuondoa kabisa changamoto ya utoroshwaji wa madini,” alisema Kitandula.

MUSUKUMA AMPONGEZA BITEKO

Akichangia mjadala wa bajeti ya wizara hiyo, Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Musukuma (CCM) alimpongeza Waziri Biteko kwa utendaji kazi wake mzuri, huku akidai kwamba ambaye anabeza utendaji kazi wake huyo ni mnafiki.

“Kwa mtu yeyote asipokupongeza waziri huyo ni mnafiki. Mimi naijua vizuri dhahabu, umefanya kazi nzuri wewe pamoja na watendaji wako,” alisema Musukuma.

Pia aliitaka Stamico inunue dhahabu kutokana na kuingia kwa sasa ugonjwa wa corona, hivyo wachimbaji kukutana na changamoto ya anguko la bei.

“Ukienda sokoni kwa sasa dhahabu imeshuka sana bei, tunayo kampuni yetu ya Stamico kila mwaka tunakula hasara, kwanini Stamico isinunue dhahabu katika kipindi hiki cha corona? Niombe sana waziri unapokuja kujibu utueleze,” alisema Musukuma.

NAPE ATAKA BOT IINGILIE KATI

Akichangia hotuba hiyo, Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye (CCM) ameiomba Serikali kupitia Benki Kuu (BoT) inunue dhahabu ili kuwaokoa wachimbaji ambao wamekuwa wakiuza kwa bei ndogo kutokana na uwepo wa ugonjwa wa corona.

Nape alisema kwa sasa madini yamepatikana kwa wingi, lakini kumekuwa na changamoto ya anguko la bei kutokana na ugonjwa wa corona.

Aliiomba Serikali kupitia BoT kununua dhahabu hiyo na kuihifadhi ili pindi ambapo bei itaongezeka waweze kuuza.

AMPONGEZA WAZIRI BITEKO

Vilevile Nape alimpongeza Waziri Biteko kwa kuweza kuisimamia vizuri ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya kuwasimamia wachimbaji wadogo wadogo.

“Niipongeze Serikali ya awamu ya tano kwa kuanzisha wizara inayoshughulikia madini. Uamuzi ni mzuri, uamuzi wa kumteua ndugu Doto Biteko ulikuwa ni uamuzi wa busara, ameituliza wizara hii na ameitendea haki wizara na ninampongeza Doto kwa hili na wapigakura wanalifanyia kazi jambo hili na watawarudisha hapa bungeni.

“Serikali haijakurupuka kuwatambua na kuwarasimisha wachimbaji wadogo kwa miaka hii mine, Serikali imefuta leseni kubwa 514 na hayo maeneo wamepewa wachimbaji wadogo.

“Mimi nadhani eneo hili linatakiwa kupongezwa sana kwani hii imeajiri wafanyakazi zaidi ya 320,000 Doto na wenzako mmeitendea haki wizara,” alisema Nape.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

12,054FansLike
2,941FollowersFollow
18,400SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Latest Articles