Kigali, Rwanda
Urusi na Rwanda zimetuma wanajeshi wao nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati katika kuunga mkono vikosi vya serikali vinavyokabiliana na makundi ya waasi.
Msemaji wa serikali ya mjini Bangui amesema makundi matatu ya wapiganaji yamejaribu kuipindua serikali wiki moja kabla ya uchaguzi wa rais.
Msemaji wa serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, Maxime Kazagui,ameliambia shirika la AFP leo juma tatu kwamba mamia ya wanajeshi wa Urusi wamewasili nchini humo ilikuzima jaribio la mapinduzi.
Kazagui amesema wanajeshi hao wa Urusi ambao wamekuja na silaha nzito, ni kulingana na ushirikiano wa kijeshi baina Jamhuri ya Afrika ya Kati na nchi hiyo. Aliendelea kusema kwamba wanajeshi wengine kutoka Rwanda tayari wamewasili na wameanza kupigana.
Wizara ya ulinzi ya Rwanda ilitangaza kwamba wanajeshi wake ambao wanashiriki katika kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa,walishambuliwa na waasi wa rais wa zamani Francois Bozize.
Na kwa hiyo serikali ya Rwanda iliamua kutuma wanajeshi wa ulinzi nchini humo kulingana na mkataba wa ulinzi kati ya Kigali na Bangui.