25.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Rungwe: Nitaunda Serikali ya mseto

RungweNA DEBORA SANJA, DODOMA

 

MGOMBEA urais wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMA), Hashim Rungwe amesema endapo akishinda nafasi hiyo, ataunda Serikali  ya mseto itakayoshirikisha vyama vyote vilivyoshiriki uchaguzi.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Rungwe alisema Katiba haikatazi kuundwa kwa Serikali ya aina hiyo.

“Nitachagua watu wenye akili kutoka vyama vyote vilivyoshiriki uchaguzi kwa ajili ya kuunda Serikali, nitapunguza pia ukubwa wa Serikali ili fedha hizo zifanye maendeleo ya wananchi,” alisema.

Alisema hii ni mara ya kwanza kwa chama chake kushiriki uchaguzi, hivyo wagombea wake wote ni wasafi hawana madoa yoyote.

“Wagombea wetu wengi wapya, hawana madoa tofauti na wenzetu kutoka vyama vingine kwa kuwa wengi ni walewale, hali inayowalazimu  kipindi hiki cha kampeni kujibu maswali ya wananchi kabla ya kuwaomba kura,” alisema.

Alisema anashangaa kuona baadhi ya wagombea kujisifu kwamba wameleta maendeleo, ikiwamo kujenga barabara wakati walitumia fedha za wananchi.

“Mtu anabaki kujisifu, nimejenga hiki nimejenga kile kwani alitumia fedha za baba yake, aliona nani ambaye alipewa kazi akashindwa, hakufanya kwa kuwa hakupewa nafasi ya kufanya,” alisema.

Akizungumzia sekta ya kilimo, Rungwe alisema iwapo atakuwa rais atatengeneza ndege kubwa kwa ajili ya kumwagilia maji kwenye mashamba ya wananchi.

“Suala hilo linawezekana, waarabu wanauwezo wa kuhamisha ardhi na kuipeleka jangwani kwa ajili ya kilimo, tatizo la nchi hii si mali, bali ni uongozi mbovu,” alisema.

Kuhusu utafiti wa taasisi za Synovate na Twaweza, alisema yale yalikuwa ni maoni yao sawa na utabiri na  kwamba vipimo halisi vitatangazwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva.

“Siwezi kutoa maoni yoyote kuhusu utafiti wao, wale wanatoa utabiri wao kama waganga wa kienyeji , sipingi wala sina ugomvi nao…vipimo halisi vitaonekana Oktoba 25,mwaka huu,” alisema.

Alisema hadi sasa kwenye kampeni zake, ametembelea mikoa 12 na kila sehemu wanayopita mapokezi yanaridhisha kutokana na wananchi kujitokeza kwa wingi.

“Kwa watu waliowahi kuwa serikalini muda mrefu, baadhi ya wananchi hawakuwahi kuwa karibu yao… wakati huu wa kampeni wananchi wanavutika kwenye mikutano yao ili kuwaona, haina maana watampigia kura,”alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles