29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Robo tatu wanakijiji Bukundi hawajui kusoma, kuandika

Na Derick Milton, Meatu

WANANCHI wa kijiji cha Lukale Kata ya Bukundi,wilayani Meatu, Simiyu,  wamemuomba Mkuu wa Mkoa huo David Kafulila, vituo vitatu vya elimu ya watu wazima pamoja na walimu kutokana na robo tatu ya wakazi  wa Kijiji hicho hawajui kusoma na kuandika.

Kijiji hicho ambacho kipo umbali wa zaidi ya kilometa 80 kutoka makao makuu ya wilaya hiyo, wananchi wake wanajishughulisha na kazi za uchimbaji madini ya chumvi, ufugaji na kilimo.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi hao jana wakati wa mkutano wa hadhara na mkuu wa mkoa huo, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Dumanang kilichopo, Girahuda Gisura, amemweleza mkuu huyo wa mkoa kuwa zaidi ya robo tatu ya wananchi wa kijiji hicho hawajui kusoma na kuandika.

“Robo tatu ya wananchi wa kijiji cha Lukale wote hawajui kusoma na kuandika, ni kwa nini serikali isitupatie angalau vituo vitatu vya Memkwa, wananchi wakanufaika angalau kujua kusoma na kuandika,” alisema Gisura.

Kwa upande wake  Salum Said ambaye ni  mmoja wa wachimbaji madini ya chunvi amesema  kwa muda mrefu wananchi wa kijiji hicho elimu kwao siyo kipaumbele, bali jambo muhimu ni ufugaji, uchimbaji pamoja na kilimo.

“ Wananchi wengi hapa ni kabila la Wamang’ati na Wataturu, wengi wao hawana elimu, hawajui kusoma na kuandika kweli kama wao walivyosema, hata sisi ambao tumekuja katika kijiji hiki tunapata shida kufanya nao kazi,” amesema Said.

Naye Mtendaji wa kijiji hicho Michael Kilatu,amekiri kuwepo kwa idadi kubwa ya wananchi wake ambao hawajui kusoma na kuandika, huku akieleza kuwa kijiji hicho kina wananchi 1,699.

“Ni kweli wengi hawajui kusoma na kuandika lakini katika kuchangia maendeleo wana mwitikio mkubwa, ambao wamesoma ni wachache sana ndani ya kijiji hiki, hivyo kituo cha elimu ya watu wazima ni muhimu sana,” amesema Kitalu.

Kutokana na ombi hilo, Kafulila aliwashukuru  kwa kuweka wazi changamoto hiyo na kumwagiza  Mkurugenzi wa halmashauri hiyo pna Ofisa Elimu Msingi kuhakikisha wanaleta walimu na kuanzisha kituo cha elimu ya watu wazima ndani ya kijiji hicho.

“ Niwapongeze kwa ombi hilo, mmeongea jambo la muhimu sana, elimu ni haki yenu, mkurugenzi na ofisa elimu fanyeni utaratibu wa kuleta walimu na kuanzisha kituo cha Memkwa hapa mara moja,” amesema Kafulila.

Katika hatua nyingine  wananchi hao wameiomba Serikali kukamilisha ujenzi wa zahanati yao ambayo wameijenga kwa miaka 10, kwani wamekuwa wakihangaika  kutembea kilometa 90 kufuata huduma za afya makao makuu ya kata.

Mbali na Zahanati wananchi hao wameomba huduma ya maji safi na salama kwa kuchimbiwa kisima wanayotumia si salama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles