25.7 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

Risasi zarindima ofisi za CUF

Julius Mtatiro
Julius Mtatiro

PATRICIA KIMELEMETA,DAR ES SALAAM

VURUGU kubwa ziliibuka tena jana katika Ofisi za Chama Cha Wananchi (CUF)   Buruguni  Dar es Salaam.

Hali hiyo ilisababisha polisi kuingilia kati kwa kufyatua risasi hewani kuwatanya wafuasi wa chama hicho waliokuwa wakitaka kuzuia kufanyika mkutano wa Kaimu Mwenyekiti wa chama hicho, Julius Mtatiro na vyombo vya habari.

Vurugu hizo ziliibuka baada ya baadhi ya walinzi wa chama hicho maarufu kama ‘Blue Gurd’ kuvamia ofisi hizo.

Walinzi hao waliwataka viongozi waliochaguliwa na Baraza Kuu hivi karibuni kutozungumza na waandishi wa habari kwa madai kuwa hawana mamlaka ya katiba ya kufanya hivyo.

Mkutano huo na waandishi ulipangwa kuanza saa 5.00 asubuhi, mzungumzaji mkuu akiwa Mtatiro, lakini ulichelewa baada ya kutokea vurugu hizo.

Vurugu kama hizo zilizotokea Dar es Salaam Agosti 21 mwaka huu na kusababisha mkutano mkuu maalumu wa chama hicho kuvunjika baada ya baadhi ya wanachama wanaomuunga mkono Profesa Ibrahim Lipumba kutaka arudishwe kwenye   uenyekiti  wa CUF bila masharti.

Hali ilivyokuwa

Walinzi hao walikusanyika kwenye ofisi hizo kuanzia saa 2.00 asubuhi na kuanza kufanya vurugu huku wakiwataka viongozi hao kuondoka kwenye eneo hilo kwa sababu mgogoro uliopo katika chama hicho   haujatatuliwa.

Ilipofika saa 4.00 asubuhi walinzi hao kwa kushirikiana na wanachama wengine ambao wanadaiwa ni wafuasi wa Profesa Lipumba, waliongezeka, hali iliyosababisha polisi kufika kwenye ofisi hizo na kuwaamuru waondoke.

Polisi waliokuwa kwenye gari   namba   PT 3699 walifika na kutoa amri ya kuwataka walinzi hao na wafuasi wengine wa chama hicho kuondoka katika eneo hilo.

Hata hivyo, amri hiyo ilipingwa na wafuasi hao hatua iliyowalazimu polisi kufyatua risasi sita hewani kwa nyakati tofauti ili kuwatawanya.

Licha ya kufyatuliwa   risasi hizo,   wanachama hao waligoma kuondoka na kuanza kuimba nyimbo mbalimbali.

Walisikika wakisema ‘hawana imani na viongozi hao’ kwa madai kuwa wamewekwa kinyume na katiba ya chama, hivyo wanamtaka Profesa Lipumba arudi kwenye nafasi yake  aweze kuendelea na majukumu.

Kutokana na hali hiyo polisi waliongezeka na kuanza kuwatawanya kwa nguvu na kumkamata mwanachama mmoja kabla ya kuachiwa baadaye.

Mtatiro mwenyewe hakuwa tayari kuzungumzia vurugu hizo akidai   nafasi ya mwenyekiti ni taasisi ambayo inaweza kushikwa na mtu yeyote aliyeteuliwa.

“Sijui kama nje kulikuwa na risasi zilizowatawanya wafuasi wanaoitwa wa Lipumba (Profesa) na wala sijui kama kulikuwa na wanachama waliotaka kuzuia mkutano wangu,” alisema Mtatiro bila kufafanua.

Mkutano na waandishi

Ilipofisa saa 11:45 mchana  ndipo Mtatiro alipojitokeza mbele ya waandishi wa habari na kuzungumza nao.

Katika mkutano huo, Mtatiro alizungumzia kauli zilizotolewa na Rais Dk. John Magufuli kwenye ziara ya siku mbili visiwani Unguja na Pemba.

Mtatiro alidai kuwa kauli alizozitoa rais huko Zanzibar zinaweza kuleta mfarakano na kuwagawa Watanzania.

“Rais Magufuli kama kiongozi wa nchi anatoa kauli ambazo zinaweza kupandikiza chuki, uhasama na kuwagawa wananchi jambo ambalo linaweza kuleta migongano na mifarakano.

“Kauli zake zimejaa dhihaka na kebehi, huku akitumia vitisho kwa sababu analindwa na vyombo vya dola,” alisema Mtatiro.

Kaimu huyo mwenyekiti wa CUF  alisema kauli hizo si ngeni kwa kuwa zimekuwa zikitolewa mara kwa mara na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na hivyo zimesababisha kuongezeka  vitendo vya unyanyasaji visiwani humo.

“Hakuna asiyejua kama Dk. Shein hajashinda Zanzibar, bali amewekwa na CCM kwa kutumia mabavu jambo ambalo limechangia kuleta mifarakano kwa wananchi,”alisema Mtatiro.

Haa hivyo alisema CUF kitaendelea na msimamo wa kutomtambua Dk. Shein kama kiongozi kwa kuwa hakushinda kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka jana.

Alisema zaidi ya asilimia 80 ya wananchi walisusa uchaguzi wa marudio ambao aliuita ni haramu na batili, ambao ulifanyika mwanzoni mwa mwaka huu na kwamba hawawezi kuyumbishwa na watu wenye weledi mdogo wa siasa Zanzibar.

Akitoa mfano, alisema wakati wa uongozi wa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamini Mkapa, Januari 2001, serikali ilitumia majeshi na kusababisha zaidi ya Watanzania 658 kujeruhiwa na 135 kupata ulemavu wa kudumu.

Mtatiro alisema Watanzania 4,000 walikimbia nchi na kwenda kuishi Mombasa,   Kenya.

Kuhusu posho ya kustaafu anayopewa Maalim Seif, Mtatiro alisema posho hiyo si msaada bali ni haki yake ya katiba na sheria kulipwa stahiki hizo.

“Maalim Seif ni mstaafu kama walivyo wastaafu wengine, ana kila haki ya kulipwa stahiki hizo kwa mujibu wa sheria kama wanavyopewa viongozi wengine wastaafu nchini.

“Hakuna hisani kwenye mafao ya Maalim Seif bali anapewa kwa mujibu wa Katiba ya nchi, tunashangaa kauli iliyotolewa na Rais Magufuli ambayo ameonyesha wazi kuwa hapendi kiongozi huyo kupewa stahiki zake,”alisema.

Mtatiro alisema   Rais Magufuli amekuwa mstari wa mbele kuhimiza wananchi kulinda amani na utulivu lakini amekuwa mstari wa mbele  kuyashawishi majeshi kutumia nguvu bila  kuzingatia sheria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles