LONDON, UINGEREZA
HESHIMA ya Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair kwa mara nyingine iliingia doa jana baada ya ripoti kuhusu Vita ya Irak kuzidi kumumbua.
Mbali ya madudu aliyofanya kushinikiza vita hiyo, barua 29 za siri alizomwandikia aliyekuwa Rais wa Marekani George W. Bush zilichapishwa kwa mara ya kwanza jana zikionesha alivyokuwa akijipendekeza kwa kiongozi mwenzake huyo.
Barua hizo ni pamoja na ya Julai 2002, miezi saba kabla ya wabunge wa Uingereza kupiga kura kuunga mkono au kukataa uvamizi wa Irak, ambapo Blair anamtoa wasiwasi Bush kuwa atakuwa pamoja naye bila kujali matokeo yoyote ya kura hiyo.
Katika barua nyingine ya siri alimwambia Bush kuwa wanapaswa wachukue hatua, ikiwa ni miaka miwili kabla ya vita ya Irak mwaka 2003.
Nyingine anasifu hotuba ya Bush kuhusu vita hiyo kwamba ni nzuri na ya kimkakati huku barua nyingine ikihimiza wakutane ili pamoja na mambo mengine waimarishe uhusiano wao binafsi.
Ripoti hiyo inaonesha Blair akipindisha taarifa za kijasusi kuhusu tishio linaloletwa na Kiongozi wa zamani wa Irak Saddam Hussein ili kuhalalisha vita hiyo iliyosababisha vifo vya askari 179 wa Uingereza.
Baada ya miaka saba ya uchunguzi ripoti hiyo iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa Uingereza imesema vita hivyo vilianzishwa bila sababu na hakukutumika njia zote za utafutaji suluhu ya mzozo huo kwa amani.
Akiwasilisha matokeo ya uchunguzi huo, Mwenyekiti wa Tume iliyochunguza vita hivyo, Sir John Chilcot amesema ni wazi sera kuhusu Irak iliongozwa na taarifa za ujasusi na tathimini zisizo sahihi, ambazo zilipaswa kupingwa.
Lakini pia Chilcot amesema Irak haikuwa tishio na uamuzi kuhusu uwepo wa silaha za maangamizi makubwa uliwasilishwa kwa lengo la kuhalalisha vita.
Amesema matokeo ya uvamizi huo ulioongozwa na Marekani yalipuuzwa na kuwa maandalizi ya matokeo ya baada ya vita hayakuzingatiwa.
Akijibu ripoti hiyo, Blair alisema: “Siamini kuondolewa madarakani kwa Saddam Hussein ndiyo kulikosababisha ugaidi tunaoshuhudia sasa Mashariki ya Kati na kwingineko.”
Blair pia amesema uamuzi wake wa kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Saddam ulichukuliwa kwa nia njema na kwa maslahi ya taifa.
Blair alidai ripoti inaonesha hakuongopa popote au kutumia vibaya baraza la mawaziri na kuwa hakuwa na dhamira yoyote iliyojificha kuhusu vita hiyo.
Familia za askari na wanawake waliokufa nchini 179, zilisema inapanga kumfikisha mahakamani na zimemuita Blair ‘gaidi mbaya zaidi duniani’.