27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

Ripoti Maalumu – 7: Ballali alifanya kazi akiwa Marekani

Daudi Ballali
Aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Daudi Ballali

Na Waandishi Wetu

KAMA ilivyokuwa hapa nyumbani Tanzania ambako taarifa sahihi za safari ya marehemu Daudi Ballali kwenda nje nchi, kuugua kwake na hata mazishi yake ziligubikwa na utata mkubwa, ilikuwa hivyo hivyo hata Marekani ambako matukio hayo yalimkuta.

Katikati ya mkanganyiko huo, upo pia mkanganyiko mwingine wa sababu hasa ya safari yake nchini Marekani, ambapo taarifa ya Serikali na ile ya wanafamilia zimekuwa zikikinzana.

Kwa upande wa taarifa ya Serikali ambayo ilitoka baada ya shinikizo kubwa la waandishi wa habari, ilieleza kuwa marehemu Ballali alikuwa nchini Marekani kwa ajili ya kuangaliwa afya yake na baadaye angerejea nchini kwa ajili ya kuendelea na majukumu yake.

Taarifa zilizokusanywa na MTANZANIA kwa baadhi ya wanafamilia zinaeleza kuwa Gavana huyo alikwenda Marekani kikazi na habari nyingine kutoka kwa mmoja wa watu waliokuwa karibu naye zinaeleza kuwa aliaga ofisini kwake kuwa anakwenda nje ya nchi kwa muda wa wiki mbili kwa ajili ya shughuli za kikazi.

Akiwa nchini Marekani ambako alifika tarehe za mwishoni mwa mwezi Julai, inaelezwa kuwa alikuwa akiwasiliana na wasaidizi wake kila siku kujua mwenendo wa majukumu ya taasisi yake na wakati mwingine alikuwa akitoa mwongozo wa kazi.

Mmoja wa wanafamilia aliyekuwa naye karibu huko Marekani ambaye alihojiwa na MTANZANIA, alidokeza kuwa marehemu huyo alikuwa akiwasiliana na ofisi yake kila siku pamoja na baadhi ya maofisa katika Wizara ya Fedha na mara chache alikuwa kifanya mawasiliano na maofisa wa Ikulu ya Magogoni.

“Sisi tuliokuwa naye muda mwingi alipokuwa hapa tangu alipofika mwishoni mwa tarehe za mwezi Julai kwanza hatukujua kuwa alikuwa akiumwa, alikuwa akifanya mambo yake vizuri tu na kila siku ilikuwa ni lazima aongee na watu wa ofisini kwake huko Dar es Salaam. Alikuwa akiwasikiliza na wakati mwingine alitoa maelekezo ya kazi.

“Na hata alipoanza kuugua na kulazwa katika hospitali huko Boston, bado aliendelea kufanya kazi. Akiwa kitandani hospitalini alikuwa akiwasiliana na ofisi yake na wakati mwingine alikuwa anawasiliana na maofisa wengine kwenye Wizara ya Fedha. Alikuwa mtu wa shughuli nyingi kwa sababu kuna wakati alikuwa akipiga simu pale Magogoni na kuzungumza maofisa wa hapo mambo yao ya kikazi,” alisema mmoja wa wanafamilia ya marehemu Ballali aliyekuwa naye nchini Marekani, ambaye jina lake tunalihifadhi kwa sababu maalumu.

Alipoulizwa uhusiano wa marehemu Ballali na Serikali ya Tanzania wakati akiugua, alisema mwanzoni ulikuwa mzuri kwa sababu maofisa wa juu walikuwa wakifika kumtembelea katika Hospitali ya Boston alikolazwa awali, lakini baadaye uhusiano huo ulizorota.

“Siku za mwanzo alipoanza kuugua ninafahamu alikuwa na uhusiano mzuri na Serikali. Ni kweli aliyekuwa balozi hapa, Ombeni Sefue sikuwahi kumuona hospitalini, lakini viongozi wakubwa wakubwa, wakiwemo wa Ikulu walifika kumjulia hali na wapo waliokuwa wakimpigia simu kumpa pole na kumtakia afya njema.

“Nakumbuka simu moja aliipokea siku moja hivi ilikuwa mwezi Septemba. Ilipigwa na kigogo mmoja kumjulia hali na nilisikia maongezi yao.

“Lakini kufikia mwisho wa mwaka 2007 uhusiano kati ya Serikali na marehemu ulikuwa umeanza kuzorota. Na hii ni kwa sababu nadhani kuna mambo ambayo yalikuwa hayaendi sawa baina ya makubaliano ya marehemu na baadhi ya viongozi wa Serikali. Na wakati huo mambo yalikuwa ya kuchanganya sana na hata yeye mwenyewe hakuwa kwenye hali nzuri kimawazo, alikuwa kama mtu aliyedanganywa hivi na alikuwa akijuta,” alisema.

Kwa upande mwingine, watu waliokuwa karibu na marehemu Ballali hapa nyumbani, viongozi wa serikali na baadhi ya wanasiasa waliokutana naye Dodoma alikokwenda kuhojiwa kabla hajarejea Dar es Salaam na kuondoka, bado wana maswali tata kichwani ya iwapo gavana huyo aliuawa na watu waliokuwa na lengo la kuficha ukweli wa wizi wa fedha zilizokuwa zimehifadhiwa kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) au aliamua kujiua mwenyewe kutokana na msongo wa mawazo uliosababishwa na kashfa hiyo.

Baadhi ya wanasiasa waliozungumza na MTANZANIA wameeleza kuwa mwenendo wa marehemu Ballali alipokuwa Dodoma unaacha maswali ambayo hayana majibu kuhusu kuugua kwake ghafla na baadaye kukutwa na kifo.

Wanaoeleza haya, wanasema mlolongo wa matukio yaliyojitokeza kwa siku chache alizokuwa Dodoma ambako hakutoa ushirikiano wa kutosha kwa Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi iliyokuwa ikimhoji na hatua yake ya kugoma kuhojiwa na kamati iliyoundwa kuchunguza sakata hilo kwa kile kinachoelezwa kuhofia kuzungumza ukweli na kuwataka waliokuwa wakiusaka ukweli huo kuhoji mamlaka za juu yake, kuna ishara za kukata tamaa ambazo huenda zilimsukuma kufanya jambo lolote.

Lakini ipo imani nyingine kuwa inawezekana kabisa kile ambacho marehemu Ballali alikuwa akiogopa kukisema ikiwa ni pamoja na woga aliouonyesha wa kuwataja wahusika wa kashfa hiyo ndiko kulikomgharimu kwa wahusika hao kuamua kufanya jambo lolote kwake, lengo likiwa kuficha ukweli aliokuwa akiujua kuhusu kashfa hiyo.

Wakati kukiwa na imani kama hiyo hapa nyumbani, aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Ombeni Sefue, aliyeiwakilisha Serikali katika mazishi yake, aliliambia MTANZANIA katika mahojiano maalumu kuwa taarifa za kuugua kwake zilikuwa za ghafla na zilimfikia akiwa nje ya Jiji la Washington, yalipokuwa makazi yake hivyo hakuweza kwenda kumuona na baadaye kidogo alipata taarifa za kifo chake.

Hii ni sehemu ya mahojiano baina ya MTANZANIA na Balozi Sefue

Swali: Wakati Balali akiwa mgonjwa uliweza kumuona?

Jibu: Sikuweza kumuona kwa sababu wakati mimi napata taarifa za ugonjwa wake, yeye tayari alikuwa yupo nje ya Washington. Nilikuja tu baadaye kupigiwa simu kuwa amefariki.

Kwa kuwa nilikuwa Balozi wa Tanzania kule nilikwenda kwenye msiba, nilishiriki kanisani na mpaka tunampeleka kaburini kumpumzisha.

Lakini hata kama nisingekuwa balozi na ule msiba unikute Marekani ningehudhuria kwa sababu nilikuwa namfahamu Ballali, ni mtu niliyefanya naye kazi.

Swali: Ulifanikiwa kuuona mwili wake?

Jibu: Ndiyo niliuona, ndiyo maana nakwambia nilienda kanisani na nilishiriki hatua zote mpaka tulipompumzisha kaburini.

Swali: Ukiwa mwakilishi wa Serikali nchini Marekani wakati huo, uliweza kujua sababu hasa ya marehemu Ballali kuzikwa Marekani?

Jibu: Kwa kweli suala la azikwe wapi na mambo kama hayo mimi sikuwa na uamuzi nayo, hayo ni mambo ya familia.

Swali: Ulifanikiwa kujua ugonjwa uliokuwa ukimsumbua Ballali?

Jibu: Kwa kweli sikujua ni ugonjwa gani uliokuwa unamsumbua. Lakini ninachojua mimi hakuanza kuumwa alipokwenda Marekani, bali tangu akiwa Gavana alikuwa anasumbuliwa na maradhi.

Swali: Mbali na wewe, kuna Watanzania wengine waliohudhuria kwenye huo msiba?

Jibu: Walikuwepo Watanzania wengine, lakini siwezi kuwakumbuka kwa majina. Walikuwepo pia Wamarekani na watu wengine.

Swali: Kwa nini ugonjwa wake na hata kifo chake kilikuwa kimetawaliwa na usiri mkubwa?

Jibu: Kwa kweli maswali mengine mimi siwezi kuyajibu, yupo mjane aliyemuacha yeye ndiye aliyemuuguza tangu mwanzo mpaka mwisho, maswali mengine mnaweza kumuuliza yeye.

Swali: Kuna maelezo kuwa wakati wa mazishi watu walizuiwa kupiga picha, wewe ulishuhudia hali hiyo?

Jibu: Sikumbuki kitu kama hicho.

Kesho usikose kusoma kilichojificha nyuma ya ugonjwa wa Ballali

- Advertisement -

Related Articles

3 COMMENTS

  1. Kuna maelezo kuwa kuna mtu alimwona Balali nchini Marekani na Balali alipojua huyo mtu amemwona Balali alipiga simu Tanzania.Huyo mtu kabla ya kuja TZ alimpigia mtu simu Tanzania kuwa amemwona Balali na aliposhuka uwanja wa ndege alikamatwa na hajulikani alipo hadi leo.BALALI YUPO HAI AU AMEKUFA KWELI!

  2. Inatakiwa sasa ifike mahala hawa viongozi wetu wakuu wa Idara waone Aibu,kutetea mambo ya uovu,madudu,na uozo mbalimbali. Wajue uongo una mwisho,wasije pigwa mawe na hata watoto wao waliowaza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles