33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Watu 17 kortini kwa ugaidi

watuhumiwa ugaidi
Watuhumiwa wa ugaidi wakiwa chini ya ulinzi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam jana. Picha ndogo kulia ni kinara wa mtandao huo, Jihad Gaiboni Swalehe. Picha na Humphrey Shao

Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam

WATUHUMIWA 17 wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashtaka ya kula njama za kuwaingiza watu nchini kushiriki vitendo vya ugaidi, kusaidia, kuwezesha kupata malighafi, fedha na ujuzi kwa nia ya kuweka mabomu nchini na nchi jirani ya Kenya.

Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani jana mbele ya Hakimu Mkazi, Hellen Riwa na kusomewa mashtaka na Mawakili wa Serikali, George Barasa, Mwanaamina Kombakono na Brenda Nick.

Mshtakiwa Jihad Swalehe, mkazi wa Kitunda Mbondole, ni mmoja wa washitakiwa waliofikishwa mahakamani hapo jana saa 7.20 mchana, chini ya ulinzi mkali wa Polisi. Alisomewa mashtaka peke yake ya kula njama za kusaidia na kuwezesha kufanyika vitendo vya kigaidi nchini Kenya.

Washitakiwa wengine 16 wanaohusika na mashtaka ya kula njama za kuwaingiza watu nchini na kushiriki vitendo vya kigaidi ni Nassoro Abdallah, Hassan Suleimani, Anthari Ahmed, Mohamed Yusuph, Abdallah Hassani au Jibaba, Hussein Ally, Juma Sadala na Said Ally.

Wengine ni Hamis Salum, Abubakar Mngodo, Salum Ali, Salum Amour, Alawi Amir, Rashid Nyange au Mapala na Amir Juma.

Washtakiwa wote 17 wakiwa chini ya ulinzi mkali wa Polisi, waliingizwa katika chumba cha mahakama, mbele ya Hakimu Mkazi, Riwa.

Akiwasomea mashtaka washtakiwa hao, Barasa, akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Prosper Mwangamila, alidai katika tarehe tofauti kati ya Januari 2013 na Juni 2014, maeneo tofauti nchini, walikula njama ya kutenda kosa kinyume cha Sheria ya Ugaidi ya mwaka 2002, kwa kuwaingiza watu ili wafanye makosa ya ugaidi.

“Mheshimiwa Hakimu, shtaka la pili, washitakiwa wote wanadaiwa kipindi hicho na maeneo tofauti nchini, wakijua, kwa pamoja walikubaliana kuwaingiza Sadick Absaloum na Farah Omary ili kushiriki kutenda makosa ya ugaidi,” alidai Barasa.

Kutokana na tuhuma hizo dhidi yao, washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Mwangamila alidai upelelezi haujakamilika, hivyo aliiomba mahakama kuahirisha kesi hiyo hadi Jumatano ijayo ili waweze kuwasilisha maombi maalumu.

Hakimu Hellen aliahirisha kesi hiyo hadi tarehe hiyo na kuamuru washitakiwa kurudishwe rumande. Baada ya washitakiwa hao kumaliza kusomewa mashtaka, alipandishwa kizimbani Swalehe na kusomewa mashtaka na Wakili Brenda.

Akisoma shtaka dhidi ya Swalehe, Wakili Brenda alidai tarehe tofauti kati ya Machi 21, 2013 na Juni 2, mwaka huu, eneo lisilofahamika Dar es Salaam, mshitakiwa alikula njama na watu wengine ya kutenda kosa la kusaidia kutenda vitendo vya ugaidi.

Alidai katika kipindi hicho, mshtakiwa kwa kujua na kutumia mawasiliano ya Facebook waliwasiliana na Nero Saraiva na watu wengine kwa ajili ya kupata malighafi, fedha na ujuzi kwa nia ya kuweka mabomu sehemu tofauti katika Jamhuri ya Kenya ili kusababisha majeraha na hofu kwa Wakenya.

Mshitakiwa huyo hakutakiwa kujibu chochote ambapo upande wa Jamhuri ulidai upelelezi haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa. Hakimu Hellen aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 31 mwaka huu, kwa ajili ya kutajwa.

Washitakiwa hao waliletwa mahakamani hapo mchana wakiwa ndani ya mabasi mawili ya kubebea mahabusu, huku yakisindikizwa na magari mawili ya Kikosi cha Kuzuia na Kutuliza Ghasia (FFU) na mengine matatu yaliyokuwa na askari wakiwa wamevalia kiraia.

Baada ya kusomewa mashtaka, washtakiwa waliondolewa mahakamani hapo kwa kutumia basi ndogo la magereza, wakisindikizwa na magari manne ya FFU.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles