KUILENGA saratani ya tezi dume kwa tiba ya mionzi ya nishati ya mwanga kutoka chombo mfano wa tochi kijulikanacho kama (laser) kunaweza kuondoa vivimbe kwa maelfu ya wanaume, utafiti umebainisha.
Njia hiyo, ambayo mwanga maalumu wenye kemikali inayopenya ukichagizwa na laser huzifikia seli za saratani na huweza kuokoa wagonjwa wengi dhidi ya maumivu yatokanayo na upasuaji au tiba mionzi.
Karibu nusu ya wanaume waliokuwa katika hatua za awali za saratani ya tezi dume walishuhudia ikitokomezwa moja kwa moja kwa njia hiyo wakati wa majaribio.
Kwa sababu mkondo mzima wa damu haujazwi na dawa, athari zilizozoelekeza katika tiba za kawaida hupunguzwa kwa kiasi kikubwa na tishu zenye afya haziharibiwi.
Pia tiba hii ina nafuu zaidi ya zile nyingine zilizozoeleka, ambazo zinahusisha pamoja na upasuaji wa kuondoa tezi au tiba mionzi (radiotherapy) ambayo hubomoa na kuja na vihatarishi ikiwamo ugumba au kushuka kwa uwezo wa tendo la ndoa.
Matokeo ya utafiti huo yaliyohusisha wagonjwa zaidi ya 400 wa saratani ya tezi dume chini ya wataalamu wa Chuo Kikuu cha London na kuchapishwa katika jarida la Sayansi la Lancet.
Nusu ya wanaume walipatiwa tiba mpya na asilimia hiyo 49 haikuonesha dalili za maradhi miaka miwili baadaye – kulinganisha na asilimia 13.5 tu ya wagonjwa waliopona miaka miwili baada ya kupata tiba zilizozoeleka.
Mtafiti kiongozi Professa Mark Emberton katika Chuo Kikuu cha Hospitali ya London, alisema: “Matokeo haya ni habari njema kwa wanaume wenye maradhi ya saratani yaliyo katika hatua za awali. Watapata matibabu yanayoweza kuua saratani bila kuondoa au kuharibu tezi.
“Hii kwa kweli ni hatua kubwa iliyopigwa kwa matibabu ya saratani ya tezi dume, ambayo ilikuwa ikiburuza miongo kadhaa iliyopita nyuma ya saratani kama ya ile ya matiti,” anasema.
Matibabu hayo yajulikanayo kama tiba inayolenga mishipa ya damu kupitia nishati au jina la kibiashara Tookad – inaweza kupatikana katika Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Tiba (NHS) ndani ya miaka miwili au mitatu ijayo.
Wanasayansi katika Taasisi ya Sayansi ya Weizmann nchini Israel walitengeneza njia hiyo miaka kadhaa iliyopita baada ya kugundua baktaria wenye kuhisi mwanga chini ya bahari.
Ili kuishi katika mwanga mdogo mno wa jua, baktaria walipitia kubadili mwanga kuwa nishati yenye ufanisi mkubwa.
Wanasayansi wa Israeli waliiga maajabu hayo ya asili kwa kutengeneza mchanganyiko ujulikanao WST11, ambao hutoa molekuli zinazoharibu uvimbe wakati vinapowezeshwa na mwanga wa laser.
Walienda kufanya kazi kwa kushirikiana na timu ya Chuo Kikuu cha London, ambacho kwa miongo kadhaa iliyopita imekuwa ikifanyia majaribio tiba kupitia mlolongo wa majaribio ya kimaabara.
Dawa hiyo WST11 inaingizwa katika mkondo wa damu kwa dakika 10 na kisha laser kufanya kazi yake kwa dakika 20 kupitia upenyo mdogo mwembamba unaoelekezwa katika ngozi, ambapo hupenya hadi mahali palipoathirika.
Kwa sasa kampuni ya dawa hiyo Steba Biotech inatarajia kukutana na Wakala wa Tiba wa Ulaya Aprili mwaka ujao kujadili uombaji wa kibali cha usalama.
Wanaume 30,000 hukabiliwa na maradhi haya nchini Uingereza kila mwaka.
Gerald Capon (68), alikutwa nayo mwaka 2011 na alipatiwa tiba hii ya nishati, ambayo ilionesha mafanikio kamili.
Mwanasheria na babu yake huyo wa wajukuu wanne kutoka Grinstead Mashariki, Sussex, alisema: “Matibabu niliyopokea yalibadili maisha yangu.”
Saratani ya tezi dume
Hii ni tezi (kokwa) ambayo inapatikana katika mfumo wa uzazi wa mwanamume katika shingo ya kibofu cha mkojo.
Kazi yake kubwa ni kutengeneza maji maji ya uzazi kwa mwanamume, ambayo husaidia kurutubisha mbegu za kiume zilizotengenezwa kutoka kwenye korodani na husaidia kusafirisha mbegu za kiume na kuzifanya zibaki hai kwa muda unaostahili.
Tezi hii huwa inaongezeka uzito au ukubwa kadri umri wako unavyozidi kukua ikiwa katika shingo ya kibofu cha mkojo na hivyo basi ukuaji wake unaweza kuathiri mfumo mzima wa utoaji mkojo kwenye kibofu.
Saratani ya tezi dume inashika nafasi ya tatu kwa kusababisha vifo vinavyotokana na saratani kwa wanaume duniani.
Ugonjwa huu ni chanzo kikuu cha vifo vinavyosababishwa na saratani kwa wanaume wenye umri wa miaka 70 na kuendelea.
Hata hivyo, satarani ya tezi dume kwa sasa inawapata zaidi wanaume kuanzia miaka 25.
Kwa ufahamisho tu ni kwamba neno saratani ni jina la ugonjwa ambalo hutokea wakati chembechembe za uhai au seli katika sehemu fulani ya mwili zinapoanza kukua bila kufuata utaratibu wa mfumo wa mwili na kutengeneza vijiuvimbe vidogo vidogo. Kwa kawaida seli huwa zinajigawa na baadaye kupevuka.