26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

Ripoti: Kupuuza usawa wa kijinsia kunaathiri maendeleo ya Taifa

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Sihaba Nkingia, akikata utepe kuashiria kuzinduliwa kwa Ripoti ya Maendeleo ya Afrika 2016.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Sihaba Nkingia, akikata utepe kuashiria kuzinduliwa kwa Ripoti ya Maendeleo ya Afrika 2016.

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM 

SHIRIKA la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF), hivi karibuni walizindua Ripoti ya Maendeleo ya Binadamu wa Afrika ya mwaka 2016 ambayo pamoja na mambo mengine imezitahadharisha nchi ikiwemo Tanzania kuhusiana na athari za kimaendeleo iwapo zitaendelea kupuuza usawa wa kijinsia.

Ripoti hiyo iliyopewa jina ‘Ripoti ya Maendeleo ya Binadamu Afrika 2016, Kuharakisha usawa wa kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake barani Afrika’, inalenga kuchochea mjadala wa kisera juu ya hatua zinazohitajika katika kutekeleza kikamilifu agenda za kitaifa kuhusiana na masuala ya usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake.

Ripoti hiyo inaonyesha juhudi zinazoendelea kufanywa na nchi za Afrika ili kuharakisha kasi ya uwezeshaji wa wanawake kupitia nyanja zote za kiuchumi, kiafya, kielimu, sehemu za kazi, ushiriki wa kisiasa na uongozi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo, Mkurugenzi Mkazi wa UNDP nchini, Awa Dabo, anasema maendeleo duni kwenye nchi nyingi barani Afrika kwa kiasi kikubwa yanachangiwa na kutokuwepo kwa usawa wa kijinsia na uwezeshwaji wa wanawake.

“Ripoti hii mpya inaonyesha maendeleo ya wanawake wa kiafrika ni asilimia 87 ya maendeleo waliyonayo wanaume katika bara hilo. Hali hiyo kwa kiasi kikubwa inachangiwa na suala la wanawake kutopewa nafasi kwenye fursa za kiuchumi, kielimu pamoja na matatizo ya kiafya,” anasema Dabo.

Kwa mujibu wa Dabo, ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) na Agenda ya Afrika 2063, Bara la Afrika linahitaji kuandaa mazingira ya usawa kwa watu wa jinsia zote ili kutoa fursa kwao kujiendeleza bila vikwazo vya kijinsia.

Hata hivyo aliipongeza serikali kwa jitihada zake katika kupunguza utofauti wa kijinsia hatua ambayo imeanza kuchukuliwa katika suala zima la ujasiriamali na elimu ikiwa ni kuanzia elimu ya msingi.

“Ni faraja kubwa kuona hapa Tanzania suala la elimu bila kujali jinsia limekuwa ni kipaumbele tangu miaka ya 1990. Usajili wa wanafunzi katika ngazi ya elimu ya msingi kwa wastani ni sawa kwa jinsia zote hatua ambayo imekuwa ikileta matokeo mazuri hata katika ngazi ya elimu ya juu,’’ anasema.

Mtazamo wa Dabo unaungwa mkono na Mkurugenzi Mtendaji wa ESRF, Dk. Tausi Kida, ambaye pia alisisitiza umuhimu wa serikali kuzifanyia kazi tafiti mbalimbali kwa kuwa zimekuwa zikionyesha picha halisi kwa wakati husika.

“Kwa kuzingatia umuhimu wa hizi tafiti ESRF tumekuwa tukifanya tafiti ya kitaifa kuhusu maendeleo ya binadamu kila mwaka tangu mwaka 2013 na kwakweli zimekuwa na msaada mkubwa kwa serikali katika kuinua viwango vya maendeleo ya wananchi,’’ anasema.

Anasema ushirikiano uliopo kati ya ESRF, UNDP na serikali umekuwa na tija kubwa  katika maandalizi ya tafiti zenye tija kwa Taifa  huku akitumia mfano wa ripoti ya ESRF ya Maendeleo ya Binadamu ya Tanzania ya mwaka 2014 iliyoitwa mabadiliko ya kiuchumi kwa maendeleo ya binadamu.

Akifafanua zaidi kuhusu ripoti hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinisia, Wazee na Watoto, Sihaba Nkinga, anasema mbali na kuonyesha uhalisia  ripoti imekuja wakati muafaka kwani ni katika kipindi ambacho Tanzania ipo kwenye harakati za kuleta usawa wa kijinsia katika nyanja zote za kijamii, kisiasa na kiuchumi.

“Ripoti kama hizi zimekuwa zikitusaidia sana kwenye masuala ya uandaaji wa sera zetu ndio maana tumekuwa tukuzifuatialia kwa umakini mkubwa.’’  anasema.

Kwa mujibu wa Nkinga, utekelezaji wa ripoti kama hizo ndio umelisaidia Taifa kupiga hatua kubwa katika masuala ya usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake huku akitolea mfano idadi kubwa wa wabunge wanawake kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wale waliopo kwenye Baraza la Mawaziri huku uwepo wa Makamu wa Rais ambaye ni mwanamke nao ukinogesha zaidi hatua hiyo.

Hata hivyo anakiri kuwa pamoja na mafanikio hayo bado Taifa kwa ujumla halijafanikiwa kutumia ipasavyo uwezo wa wanawake katika kujiletea maendeleo zaidi ikilinganishwa na mchango unaoletwa na wanaume licha ya ukweli kuwa kijamii wanawake wameonekana kuwa uti wa mgongo wa familia nyingi hapa nchini

“Jitihada zinazofanyika ni kubwa na zinatia matumaini hasa huko tuendapo ndio maana hadi sasa wanawake ambao ni asilimia 51.3 ya idadi ya watu hapa nchini wameshikilia asilimia 43 ya ujasairiamali na viwanda vidogo vidogo hapa nchini,’’ anasema.

Uzinduzi wa ripoti hiyo umehusisha wadau kadhaa wakiwemo watunga sera ya maendeleo, taasisi za kimaendeleo, wawakilishi kutoka sekta binafsi, taasisi za kiraia, wasomi na wadau wengine husika.

Wakati wa mjadala uliofanyika katika uzinduzi huo, washiriki walikubaliana na masuala muhimu yalioainishwa kwenye ripoti hiyo huku wakikubaliana kuwa mila na desturi kandamizi dhidi ya wanawake zinatakiwa kutazamwa upya kwa kuwa zimekuwa zikirudisha nyuma maendeleo ya jamii kwa ujumla.

Zaidi washiriki walikubaliana kwamba changamoto zinazowakabili wanawake katika kupata ardhi yakiwemo masuala ya mirathi, mila na desturi nazo zimekuwa zikiwakwamisha kila wanapojitahidi kijikwamua kiuchumi na kuboresha maisha yao.

Ripoti hiyo inapendekeza uwepo wa ushirikiano na nguvu ya pamoja baina ya serikali, sekta binafsi, asasi za kiraia na washirika wa maendeleo kuelekea agenda ya pamoja katika kuchukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na uanzishwaji wa Benki ya Uwezaji ya wanawake barani Afrika pamoja kufungua madirisha ya uwekezaji maalum kwa wanawake katika benki za maendeleo ya kitaifa na kikanda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles