25.3 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

RELI YA KISASA (SGR) TURUFU YA USAFIRISHAJI

Na Mwandishi Wetu,

SERIKALI imezidi kupigia chapuo reli ya kisasa kwa kuifanya kuwa ndiyo kivutio chake mahususi cha kupata wateja wa kutumia bandari ya Dar es Salaam baada ya kuona Kenya inatamba kwa kuwa nayo.

Hayo yalibainishwa katika uwekaji saini mkataba wa mahusiano katika usafirishaji kati ya Serikali ya Uganda na Tanzania.

Serikali ya Tanzania imesema kukamilika ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge kutasaidia kuboresha mfumo wa usafirishaji nchini na kuchochea uchumi wa viwanda kwa kurahisisha na kupunguza gharama za usafirishaji.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alisema hayo wakati wa kutia saini mkataba wa makubaliano wa usafirishaji mizigo kati ya Serikali ya Tanzania na Uganda.

Alisema mfumo huo wa usafirishaji ukikamilika utasaidia bidhaa nyingi kufika kwa wakati na kuongeza idadi ya watumiaji wa sekta ya usafiri nchini.

Alisema kuboresha mfumo huo kutasaidia mizigo itakayotoka Dar es Salaam hadi Kampala, Uganda kuchukua saa 24 tu badala ya siku tatu za sasa (saa 72).

“Kukamilika mfumo huu wa Standard Gauge kutaongeza idadi ya wateja ndani na nje ya nchi wanaotumia bandari yetu na kuleta uwezekano mkubwa wa kupunguza gharama za uendeshaji,” alisema Profesa Mbarawa.

Alisema Tanzania na Uganda zina historia ndefu  katika mambo mengi ya ushirikiano hivyo Serikali ina wajibu wa kuhakikisha Uganda inanufaika na bandari ya Dar es Salaam ambayo kwa sasa imeimarika na itaendelea kuwa bora kwa kuwa na nyezo na miundombinu maridhawa ya kushughulikia mizigo ya kila namna kutokana na uwekezaji unaofanyika.

“Tumesaini mkataba na Uganda kwa lengo la kusafirisha mizigo kupitia bandari ya Dar es Salaam,” alishuhudia Waziri Mbarawa.

Profesa Mbarawa alisema hivyo mradi wa reli ya kisasa ukikamilika mizigo itakayokuwa ikitoka Dar es Salaam kwenda Kampala itachukua saa 24 tu na hivyo aliwataka watumishi wa bandari na reli kuondoa urasimu kwa kuweka mipango mikakati vizuri kuweza kutumia risiti moja ambayo itaondoa usumbufu lakini yenye nembo zote.

Hali hiyo ilirudiwa na Serikali ya Uganda pale waziri wake aliposisitiza uaminifu na uadilifu kwa vitendo.

Waziri wa Usafirishaji wa Uganda, Aggrey Bagiire, alisema uaminifu ndiyo njia bora ya kuimarisha biashara baina ya nchi hizo mbili na kutaka mwenedo mzuri ili kupunguza gharama.

Alisema makubaliano hayo yaliyofikiwa yasipotekelezwa yanaweza kusababisha nchi moja kupata hasara kwa kuhangaika kufanya mawasiliano ambayo yanaweza kuchangia ongezeko la gharama.

“Tutaendelea kushirikiana na Tanzania katika mawasiliano mbalimbali na nafasi hii tuliyoipata ni nzuri, hakika tuna imani tutapata huduma za uhakika,” alisema Bagiire.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Deusdedit Kakoko, alisema ni wajibu wa nchi hizo kushirikiana kwa sababu zina historia ndefu.

Alisema njia ya Dar es Salaam – Mwanza –Kampala, Uganda itanufaisha nchi kwa sababu itachukua muda mfupi wa saa 24 tu.

Tanzania iko mbioni kuboresha Bandari ya Dar na mfumo wake wa reli kuwa wa SGR ili kuongeza mwendo, ukubwa wa mizigo na upungufu wa gharama kwa wote wanaotumia huduma zake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles