24.4 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

TADB KUSISIMUA MAENDELEO YA SEKTA YA KILIMO

Na LEONARD MANG’OHA

KATIKA juhudi za kuinua ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini nchini, Serikali imechukua hatua mbalimbali kuharakisha  mapinduzi katika Sekta ya Kilimo, ambayo inaajiri zaidi ya asilimia 75 ya wananchi na kuchangia  asilimia 65 ya malighafi za viwanda vya ndani.

Pamoja na umuhimu wa sekta ya kilimo, bado ukuaji wake umekuwa ukikabiliwa na changamoto mbalimbali, kama vile kiwango kidogo cha uzalishaji, matumizi madogo ya teknolojia za kisasa, kiasi kidogo cha kilimo cha umwagiliaji maji, ukosefu wa mtaji na upatikanaji wa mikopo kwa wakulima.

Pia yako matatizo kama vile ukosefu wa masoko ya mazao, bei duni za mazao ya kilimo, miundombinu mibovu ya usafirishaji, ukosefu wa maghala ya kuhifadhi mazao, ukosefu wa nishati ya umeme wa uhakika, hususan katika maeneo ya vijijini, kutokuwapo kwa ongezeko la thamani kwa mazao ya kilimo, mabadiliko ya hali ya hewa, sambamba na changamoto nyingine lukuki. Kwa kifupi changamoto ni nyingi sana.

Kwa mujibu wa taarifa ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa gazeti la MTANZANIA, inaeleza kuwa, miongoni mwa matatizo yanayoikabili sekta ya kilimo ni ufinyu wa upatikanaji wa fedha za mikopo ya maendeleo ya kilimo nchini, unaochangiwa kwa kiasi kikubwa na mikopo mingi kutoka taasisi za fedha kuelekezwa zaidi kwenye upande wa biashara za bidhaa na si katika shughuli za kilimo.

Pia riba kubwa kwenye mikopo ya kilimo, mikopo ni ya muda mfupi, masharti magumu ya kukopa bila kuzingatia hali halisi ya sekta ya kilimo ni miongoni mwa vikwazo katika sekta hii.

Uanzishwaji wa TADB

Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ilianzishwa mwaka 2015, ili kusaidia kukabiliana na mapungufu yanayoikabili sekta hii ikiwa ni pamoja na kuhuisha upatikanaji wa mikopo katika sekta ya kilimo ili kuleta mapinduzi katika  kilimo nchini na kuhamasisha taasisi nyingine za fedha zinatoa mikopo zaidi kwa wakulima.

TADB imeanzishwa kwa madhumuni makuu mawili, ambayo ni kusaidia upatikanaji wa utoshelezi na usalama wa chakula ambao ni endelevu, pili ni kuchagiza na kusaidia mapinduzi ya kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara, ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa, kutokana na azma hiyo TADB imedhamiria na kujizatiti kuhakikisha inachangia kwa kiasi kikubwa katika  kuleta mapinduzi yenye tija katika kilimo kwa kusaidia upatikanaji na utoaji wa fedha, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa sera nzuri zitakazosaidia maendeleo ya sekta hiyo.

Malengo mkakati ya benki

Wanafafanua kuwa TADB imejiwekea malengo mkakati ambayo ni pamoja na kuinua uzalishaji wenye tija katika kilimo kwa kuendeleza miundombinu muhimu, mathalani, skimu za umwagiliaji, usafirishaji, hifadhi ya mazao, usindikaji na masoko, kuwa benki kiongozi  ya maendeleo ya kilimo, pamoja na kuhamasisha mabenki na taasisi nyingine za kifedha kutoa fedha kwenye mnyororo mzima wa thamani wa kilimo.

Pia benki inaweka mkazo katika kuhamasisha upatikanaji wa fedha zenye masharti nafuu na endelevu, ili kuinua ushiriki wa wakulima wadogo katika mfumo wa kifedha, kuhamasisha kilimo cha kisasa na cha kibiashara kwa wakulima wadogo wadogo.

Kushirikiana na Serikali, wabia wa kimkakati na wadau wengine katika kuendeleza sekta ya kilimo, hasa kuboresha na kutekeleza juhudi na sera zinazohusu kuhuisha ushiriki wa wananchi kwenye mifumo ya kifedha.

Matarajio ya benki

Taarifa hiyo inaongeza kuwa, katika kuhakikisha inaharakisha maendeleo katika kilimo, inatarajia kuongoza jukumu la utoaji mikopo ya maendeleo, ya uongezaji wa thamani katika shughuli za kilimo, kuwezesha na kusimamia upatikanaji wa sera za utoaji wa mikopo ya kilimo, kusaidia kufanya ubunifu wa bidhaa na huduma kwa kutumia teknolojia za kisasa.

Inaendelea kueleza kuwa, TADB inalenga kuwa jukwaa la utafiti na maendeleo katika upatikanaji fedha kwenye kilimo, kuongoza katika utoaji fedha na huduma saidizi, kusaidia uboreshaji wa miundombinu ya vijijini ili kuongeza ukuaji wa kilimo.

Pia inatarajiwa kuziimarisha taasisi za utoaji mikopo kwa kuchochea taasisi za fedha na wadau wengine kushiriki katika maendeleo ya kilimo.

Kuanzishwa kwa TADB kumesaidia kuboreshwa kwa upatikanaji wa mikopo na huduma za kifedha kwenye miradi ya maendeleo ya kilimo kwa riba nafuu zilizo chini ya viwango vya kibiashara kwenye soko, kuweka mfumo mahususi wa uratibu wa upatikanaji wa fedha katika kuongeza thamani kwa mazao ya Kilimo na kusaidia kuwaunganisha wakulima na masoko;

Pia imesaidia upatikanaji wa huduma zisizo za kifedha kwa wakulima, kama vile kujengewa uwezo juu ya uandaaji wa andiko la miradi ya kilimo, upatikanaji wa taarifa za masoko, usimamizi wa biashara, mafunzo ya miradi ya kilimo na mbinu za majadiliano ya mikataba.

Imesaidia kuratibu taarifa za utafiti na maendeleo ya kilimo, hali ya hewa, udongo, na hatua nyingine za kuhuisha maendeleo ya kilimo, kutoa ushauri wa kisera na kujadiliana na Serikali na wadau wa kilimo ili kuboresha mazingira ya uwekezaji na uendelezaji wa sekta ya kilimo;

TADB inaeleza kuwa, tangu kuanzishwa kwake imefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 6.5, fedha ambazo zilielekezwa kwa wakulima wadogo wadogo na Wakala wa Mbegu za Kilimo.

Tangu kuanzishwa kwa benki hii jumla ya ekari 4,969 zimekopeshwa au kunufaika na mikopo.

Maeneo yaliyokopeshwa fedha kwa kipindi chote cha uhai wa TADB ni pamoja na mahindi, mpunga, mbogamboga, nyanya, miwa, sambamba na uendelezaji wa mbegu za kilimo.

Hivi karibuni Wizara ya Fedha na Mipango iliipatia TADB Sh bilioni 209.5 kuiongezea mtaji ili kuiwezesha kutoa mikopo ya muda wa kati na mrefu kwa gharama nafuu kwa wakulima wadogo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles