26.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

RELI YA KISASA DAR – MWANZA KUKAMILIKA 2021

Na LEONARD MANGOHA – DAR ES SALAAM


UJENZI wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa (standard gauge) kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza, unatarajia kukamilika mwaka 2021 na utagharimu Sh trilioni 7.6.

Awamu ya kwanza ya ujenzi huo itakayohusisha kipande cha kilomita 300 kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, inatarajiwa kuanza mwezi huu na itagharimu dola za Marekani bilioni 1.21 (Sh trilioni 2.6).

Kwa maana hiyo, kipande cha kilomita 711 kutoka Morogoro hadi Mwanza kitagharimu Sh trilioni tano.

Akizungumza Februri 3 wakati wa kutia saini mkataba, kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alisema awamu hiyo ya kwanza inagharimu kiasi kikubwa cha fedha kutokana na jiografia ya eneo hilo kuwa na milima mingi.

Akizungumza na MTANZANIA jana ofisini kwake Dar es Salaam, Ofisa Uhusiano kwa Jamii wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (RAHCO), Catherine Moshi, alisema ujenzi wa reli hiyo yenye urefu wa kilomita 1,011 (Dar es Salaam – Mwanza) ambayo ujenzi wake umegawanyika katika awamu tano, unatarajiwa kuanza mapema mwezi huu kwa kipande cha kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, chenye urefu wa kilomita 205 za njia kuu na 95 za kupishania treni.

Moshi alisema ujenzi huo utakamilika mwaka 2021 kutokana na mfumo wanaoutumia wa kutoa zabuni kwa vipande vipande badala ya kutoa zabuni yote kwa kampuni moja.

Alisema mfumo huo unapunguza muda wa ujenzi kutokana na kampuni nyingi kufanya kazi hiyo kwa wakati mmoja, lakini ikitokea kampuni inayojenga ikaomba tenda na kushinda na ikabainika kuwa na uwezo wa kufanya shughuli hiyo kwa wakati, itapewa zabuni.

“Tunaamini tutakamilisha ujenzi huu mwaka 2021 kwa kutumia mfumo huu na kwa kuzingatia vipande vya kuanzia Makutupora (Dodoma) hadi Mwanza ni vifupi na havina milima mingi kama Dar es Salaam hadi Makutupora,” alisema Moshi.

Akizungumzia kuhusu eneo korofi kati ya stesheni ya Kilosa na Gulwe mkoani Morogoro, alisema miongoni mwa mambo waliyokubaliana kuyapa uzito wakati wa ujenzi ni pamoja na wazabuni kukwepa maeneo ya mito kama vile Magole na kupitia milimani ili kuepusha reli kuharibiwa ma mafuriko.

Kwa mujibu wa Moshi, zabuni za ujenzi wa vipande vya kutoka Morogoro hadi Mwanza zinatarajiwa kufunguliwa mwezi ujao, ambapo vipande vitakavyohusika ni kile cha Morogoro hadi Makutupora kilomita 336, Makutupora-Tabora (km 294), Tabora-Isaka (km 133) na Isaka-Mwanza (km 248).

Akizungumzia ujenzi wa reli ya kiwango kama hicho kutoka bandari ya Mtwara hadi Mbambabay na Mchuchuma na Liganga, alisema tayari upembuzi yakinifu umekemilika na sasa wako kwenye mchakato wa kumtafuta mshauri wa fedha ili kufahamu kiasi kitakachotumika kujenga mradi huo.

Alisema reli hiyo yenye urefu wa kilomita 1,000 pia itakuwa ya kiwango cha kimataifa (standard gauge) na kwamba kukamilika kwake kutarahisisha usafirishaji wa mizigo kutoka bandari ya Mtwara kwenda nchi jirani za Zambia na Malawi.

Akizungumzia uondoaji nyumba katika maeneo ya hifadhi ya reli nchini ambao kwa baadhi ya maeneo umeibua maswali miongoni mwa waliowekewa alama, alisema kuwa pamoja na sheria kueleza kuwa eneo la hifadhi ni mita 15 kwa maeneo ya mijini na 30 kwa maeneo ya vijijini, lakini kwa maeneo ya stesheni ya treni sheria inasema ni kati ya mita 75 na 100.

Moshi alisema hiyo ni kwa sababu kuna njia nyingi za kupishania na kushushia na kwamba maeneo ya makutano ya barabara na reli ni mita 100 kila upande ili kumwezesha dereva kuona kwa urahisi kama kuna gari linakaribia.

Hivi karibuni baadhi ya wakazi wa Kichangani mkoani Morogoro walilalamikia kutakiwa kubomoa nyumba zao ndani ya siku 30, wakisema kuwa sheria inaeleza eneo la hifadhi ya reli kwa maeneo ya mjini ni mita 15, hivyo hawaafiki hatua iliyochukuliwa dhidi yao.

“Mbona sheria hapa imeeleza wazi kuwa ni mita 15 mjini, wao wanatutaka vipi kuvunja nyumba zetu, kwahiyo wao na sheria ni kipi kinachosema ukweli?” alisema mmoja wa wananchi hao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles