30 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

RELI SGR YAJENGWA USIKU NA MCHANA KUFIKIA LENGO MIEZI 30

Na LEONARD MANGOHA

MCHWA pamoja kuwa ni wadudu waharibifu kwa mali za binadamu, lakini wanayo sifa moja kubwa ya kufanya kazi usiku na mchana kwa ufanisi mkubwa.

Utendaji kazi unaoshuhudiwa katika ujenzi wa Reli ya Kati katika kiwango cha SGR Dar hadi Morogoro, inafanana kiutendaji kazi kama vile shughuli ya mchwa ya ujenzi wa usiku na mchana na Kampuni ya Kituruki ya Yapi Merkez, wakitimiza azma ya Rais John Magufuli ya Hapa Kazi Tu.

Ni wakati wa utekelezaji na si maneno marefu na kweli kazi inafanyika na usiku totoro kwa mafanikio na ufanisi mkubwa.

Baada ya kuwapo kwa taarifa za ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa (standard gauge), hatimaye Februari 3 mwaka huu Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (Rahco), ilitiliana saini mkataba wa kuanza ujenzi wa mradi huo na kampuni ya Yapi Merkez ya Uturuki.

Baada ya hapo taratibu za ujenzi zikaanza ukiwamo ujenzi wa kambi zitakazotumika wakati wa ujenzi ikiwamo ile ya Ilala, Dar es Salaam, Soga, Pwani na Ngerengere Morogoro.

Wakati huo pia shughuli ya usanifu wa njia itakayopita reli uliendelea kama mkataba wa ujenzi huo ulivyotaka usanifu na ujenzi vifanyike pamoja, kazi ambayo inaelezwa kukamilika kwa asilimia mia moja.

Meneja Msaidizi wa Mradi huo, Mhandisi Chedi Masambaji, anasema kazi hiyo iliambatana na ile ya upimaji wa udongo wa eneo la njia ya reli ambayo pia imekamilika.

“Kama tulivyoweza kuona kuanzia Pugu hadi hapa Soga zaidi ya kilomita 100 ujenzi unaendelea vizuri na hivi karibuni mkandarasi ataanza kazi ya kupasua miamba,” anasema Mhandisi Masambaji.

Hadi sasa ujenzi huo unaendelea kwa shughuli mbalimbali kutekelezwa, ambapo tayari eneo lenye urefu wa kilomita 107 linaendelea na ujenzi likiwa kimegawanywa katika maeneo 10 ambapo yote hufanya kazi mchana na matano kati yake hufanya kazi usiku na mchana.

Mwishoni mwa wiki tulipata nafasi ya kutembelea mradi huo wakati wa usiku kuona maendeleo ya utekelezaji wake chini ya kampuni hiyo ya Kituruki.

Ni mwendo wa saa nne kutoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam hadi kambi ya Soga kupitia Pugu, ukivuka milima mirefu na mabonde na wakati mwingine kulazimika kupita kwenye mahandaki shughuli mbalimbali zinaendelea kutekelezwa huku baadhi ya wafanyakazi wakilazimika kutumia kambi ndogo zinazohamishika kila baada ya kusogea umbali fulani.

Mradi huu unatekelezwa katika maeneo yaliyopitiwa na reli ya kati iliyojengwa na wakoloni mwaka 1905 na katika mazingira yasiyo na makazi ya watu, huduma za afya, maji wala nishati ya umeme.

Huenda maeneo hayo yana unafuu yakilinganishwa na wakati wa ukoloni kutokana na mabadiliko ya tabianchi, lakini bado mapori yenye vichaka vidogo na miti mirefu michache.

Uwapo wa reli ya kati unaweza kuwa msaada katika ukelekezaji wa mradi huu hata pale mvua zitakapoanza kunyesha kwa mizigo hiyo itasafirishwa kwa treni.

Kwa sababu reli hiyo inajengwa karibu na reli ya kati, hii itarahisisha ubebaji mizigo na ndiyo itakayotumika kupeleka kokoto na mataruma.

Mkurugenzi Mtendaji wa Rahco, Masanja Kadogosa, anasema wameamua mradi huo ujengwe usiku na mchana ili kuhakikisha unakamilika katika muda uliopangwa wa miezi 30 iliyoanzia Mei mwaka huu.

Kadogosa anasema hadi sasa jumla ya kilomita 107 zinaendelea na ujenzi kwa hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na ujenzi wa tuta la reli ambalo limekwishajengwa kwa zaidi ya kilomita 30.

Kadogosa anaeleza kuwa mwezi mmoja uliopita walipotembelea mradi huo Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, alimtaka mkandarasi kuongeza kasi ya ujenzi kwa kujenga usiku na mchana.

“Kama tunavyoona hilo limeanza kutekelezwa, leo tumefika hapa usiku huu tumewakuta mafundi wakiendelea, sasa ili tuweze kwenda haraka zaidi tumeamua kuongeza ‘site’ (maeneo ya ujenzi) kutoka sita hadi kufikia 10.

“Unaposimamia mradi mkubwa kama huu unakuwa na ratibajedwali ya utendaji kazi inayokuongoza kwa siku kadhaa unatakiwa kuwa wapi, tunashukuru kwa sababu kazi inakwenda kama ilivyopangwa, maeneo hayo yote kumi hujengwa mchana na usiku matano kati ya hayo kazi hufanyika mchana na usiku,” anasema Kadogosa.

Kwa sasa kazi zinazoendelea ni zile zinazohusu ujenzi pekee kwa sababu mkandarasi anaendelea na ujenzi wa tuta na baada ya muda ujenzi wa tuta utakwenda sambamba na kazi nyingine ikiwamo ujenzi wa madaraja na karavati.

“Kazi ya ujenzi wa tuta ndiyo ngumu kwa sababu huchukua asilimia 60 ya ujenzi, yenyewe itakamilika kwa miezi 18 ya kwanza, uwekaji mataruma, kokoto, ufungaji wa reli na ujenzi wa mifumo ya umeme na mawasiliano ni asilimia 40 tu ya ujenzi wote na huenda haraka haraka.

Kadogosa anawataka makandarasi wazawa walioajiriwa kwa shughuli mbalimbali katika mradi huo kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa uhakika na haraka na ikiwa hawawezi kufanya hivyo waondoke wenyewe.

Hadi sasa mradi wa ujenzi wa reli hiyo katika kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro chenye urefu wa kilomita 205 za njia kuu na 95 za njia za kupishania treni, utakaogharimu Sh trilioni 2.6 umeajiri zaidi ya watu 800 wakiwamo makandarasi, wafanyakazi, vibarua na watoa huduma mbalimbali.

Kwa mujibu wa Kadogosa ujenzi wa reli hiyo kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza, unatarajiwa kuajiri watu zaidi ya 600,000 hadi utakapokamilika, idadi hiyo inajumuisha wafanyakazi, vibarua na watoa huduma wengine wakiwamo mama lishe na wachuuzi wa vitu mbalimbali.

Anafafanua kuwa ajira hizo zitaendelea kuongezeka kulingana na kazi inavyofanyika, ambapo kwa wakati huu idadi ni ndogo kutokana na kazi inayotekelezwa ni ya ujenzi tu hivyo kazi nyingine zitakapoanza itaongezeka.

“Haiwezekani kuajiri watu wote wanaohitajika kwa wakati mmoja kwa sababu hawatakuwa na kazi ya kufanya, kadiri tunavyoendelea watu wengi zaidi wataajiriwa kadiri ya mahitaji halisi na yaliyoainishwa” anasema Kadogosa.

Meneja mradi wa Rahco, Mhandisi Maizo Magedzi, anasema kwa sasa kuna jumla ya mitambo 189 inayofanya kazi na itaendelea kuongezwa kadiri kazi itakavyoendelea.

Wakati wa mvua kazi haitaweza kuendelea vizuri kuna wakati tutalazimika kusimama kwa sababu mitambo itakuwa inakwama, lakini tutajitahidi kutumia mitambo ambayo matairi yake hayashiki tope, tayari mingine iko bandarini,” anasema Mhandisi Mgedzi.

Meneja Mradi wa Kampuni ya Yapi inayojenga reli hiyo, Abdullah Kilic, anasema hadi sasa wanaendelea vizuri na ujenzi wa reli hiyo inayotakiwa kukamilika katika kipindi cha miezi 30 ili kuhakikisha wanakamilisha katika muda waliokubaliana.

Uwezo wa kampuni hii katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya aina hii si wa kutiliwa shaka kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo uwezo wa Taifa la Uturuki katika masuala ya ujenzi ambayo katika  dunia ni ya nne baada ya Marekani, China na Urusi.

Kwa kiasi kikubwa uchumi wa Uturuki unategemea sekta ya ujenzi ambayo ndiyo inayochangia zaidi katika pato la taifa kila mwaka ikifuatiwa na utalii.

Noman Sigara King ni Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Miundombinu, anasema hana wasiwasi na uwezo wa kampuni ya Yapi katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya reli, kwa kuwa ameshuhudia mradi reli ya kiwango cha kimataifa inayounganisha Bara la Ulaya na Asia iliyojengwa kwa ustadi mkubwa nchini Uturuki.

Silaha nyingine kubwa ambayo kampuni hii inaweza kujivunia katika utekelezaji wa mradi huu ni wingi na ubora wa mitambo wanayotumia katika ujenzi. Kiushindani kampuni hiyo imebeba dhamana ya kuwa mbadala wa kampuni za Kichina ambazo zimehodhi soko la Tanzania na Afrika Mashariki.

Umuhimu wa SGR

Treni itakayotumia reli hiyo itakuwa na uwezo wa kusafirisha mizigo tani milioni 17 kwa mwaka, uzito ambao ni zaidi ya mara tatu ya uzito wa treni inayotumika sasa ambayo husafirisha tani milioni 5 tu kwa mwaka.

Itakuwa na uwezo wa kubeba tani 30 kwa behewa moja. Haya yatakuwa ni mapinduzi makubwa katika sekta ya usafirishaji nchini na hivyo kudai uzalishaji mkubwa zaidi.

Ikumbukwe kuwa treni hiyo itakuwa na uwezo wa kubeba tani 10,000 za mizigo kwa mara moja, uzito amabao ni sawa ule wa mizigo inayoweza kubebwa na malori ya ‘semi trailer’ 500.

Maana yake hapa ni kwamba, barabara zetu zitadumu kwa muda mrefu zaidi tofauti na hivi sasa, ambapo zimekuwa zikilazimika kufanyiwa marekebisho ya mara kwa mara tena muda mfupi tu baada ya kuanza kutumika kutokana kwa kutegemewa katika kusafirisha mizigo mizito zaidi ya uwezo wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles