22.9 C
Dar es Salaam
Sunday, June 23, 2024

Contact us: [email protected]

Rekodi mrithi wa Makambo Yanga tishio

Mohamed Kassara -Dar es salaam

YANGA imekamilisha usajili wa msimu ujao kwa kumsajili mshambuliaji, David Molinga kutoka FC Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC).

Molinga ambaye mashabiki wa soka wa DRC wanapendelea kumwita Falcao(Radamel), wakimfananisha na mshambuliaji wa zamani wa Atletico Madrid na timu ya Taifa ya Colombia, amechukua nafasi ya kipa  Klaus Kindoki ambaye ameafikiana na Yanga kuvunja mkataba.

Molinga anaelezwa kuwa mrithi wa aliyekuwa mpachika mabao wa Yanga, Herietier Makambo ambaye ameuzwa klabu ya Horoya AC ya Ligi  Kuu ya nchini Guinea.

Akiwa na Lupopo, Molinga ameacha rekodi za maana, katika ufungaji mabao, ambapo msimu uliopita alitupia mara14, katika michezo 16 aliyoshuka dimbani katika mashindano mbalimbali.

Mshambuliaji huyo anatarajiwa kushirikiana na wakali wengine waliojiunga na Yanga kwa ajili ya msimu ujao, akiwemo mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Uganda, Juma Balinya aliyetua Jangwani akitokea Polisi ya nchini humo.

 Molinga ana uzoefu wa kutosha kwani rekodi zinaonyesha, pia amewahi kucheza nje ya DRC katika ligi za Gabon na Angola.

Akiwa Angola, Molinga alizitumikia timu mbili za Clube De Agosto na Recreativo do Libolo, pia amezichezea TP Mazembe, AS Vita na Renaissance za kwao.

Kwa upande wa Ligi Kuu ya DRC pekee, msimu uliopita alimaliza nafasi ya tano katika chati ya wafungaji, baada ya kufunga mabao 11, akiachwa kwa mabao matano na kinara, Jackson Muleka wa TP Mazembe aliyemaliza na 16.

Kanuni za usajili wa wachezaji wa kigeni za Ligi Kuu Tanzania Bara zinaruhusiwa timu kusajili wachezaji 10 wa kimataifa, na hii ndio iliyoilazimisha Yanga kuachana na Kindoki.

Yanga imesajili wachezaji wapya nane wa kigeni, wengine mbali ya Molinga ni kipa Mkenya Farouk Shikalo (Kenya), Issa Bigirimana(Burundi)
, Patrick Sibomana (Rwanda), Mustapha Suleiman (Burundi), Sadney Urikhob (Namibia), Lamine Moro (Ghana), Maybin Kalengo (Zambia) na Balinya.

Wengine wa kigeni waliokuwamo katika kikosi cha Yanga msimu uliopita ni Papy Tshishimbi(DRC).

Hata hivyo ili kuingiza jina la Molinga kwenye usajili wa Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo timu hiyo itaiwakilisha Tanzania kama ilivyo kwa Simba, Yanga italazimika kulipa faini ya Dola 500 (zaidi ya Sh milioni moja)kwa  Shirikisho la Soka Afrika (Caf).

Hatua hiyo inatokana na dirisha la usajili wa michuano ya Caf, ambayo ni Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho kufungwa tangu Julai10 mwaka huu.

Caf iliweka wazi kuwa, baada ya muda huo kupita, kuanzia Julai 11 hadi 20, klabu itakayotaka kusajili mchezaji itatakiwa kulipa faini Dola za Kimarekani 250 (zaidi ya Sh laki tano), lakini pia ile itakayotaka kuingiza jina la mchezaji kuanzia Julai 21 hadi Julai 31 italipa Dola 500, lakini mchezaji atatumika kuanzia raundi ya pili.

Yanga itazindua kampeni za Ligi ya Mabingwa kwa  kuumana na Township Rollers ya Botswana, mchezo wa kwanza wa hatua ya awali utachezwa kati ya Agosti 8 na 11, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kabla ya marudiano kupigwa kati ya Agosti 23 na 25, jjini Gaborone.

Kama itafanikiwa kuruka kiunzi hicho, itatinga raundi ya kwanza na kukutana na mshindi kati ya Green Mamba ya Eswatini na Zesco ya Zambia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles