ZAINAB IDDY-DAR ES SALAAM
WAWAKILISHI wa Tanzania katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba, leo watajitupa kwenye Uwanja wa Mazembe mjini Lubumbashi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na TP Mazembe.
Mchezo huo wa marudiano katika hatua ya robo fainali, unaonekana ni mgumu kwa Simba baada ya kutoka suluhu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Jumamosi iliyopita.
Mshindi wa jumla katika mchezo huo atakutana na mbabe kati ya Constatine ya Algeria na mabingwa watetezi wa michuano hiyo, Esperance ya Tunisia katika hatua ya nusu fainali.
Kwenye mchezo uliopita Simba ilicheza vizuri mno na kuihimili TP Mazembe, mabingwa mara nne wa Ligi ya Mabingwa Afrika kiasi cha kukaribia kushinda mchezo huo ambapo nahodha wake, John Bocco, alikosa penalti.
Matokeo haya yameonekana kuwaumiza mashabiki wa Simba, hasa pale wanapokumbuka rekodi yao ya mwisho walipokutana na Mazembe miaka nane iliyopita.
Mwaka 2011 katika mchezo wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa, Simba waliambulia kipigo cha mabao 3-1 mjini Lubumbashi, kabla ya kuchapwa tena mabao 3-2, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, hivyo kujikuta wakitolewa kwa jumla ya mabao 6-3, hili pekee linawakatisha tamaa mabingwa hao wa Tanzania Bara.
Simba inahitaji kushinda au kupata sare ya idadi yoyote ya mabao katika mchezo wa leo ili iweze kusonga mbele.
Lakini ukiutupia jicho la tatu mchezo wa Mazembe na Simba, wawakilishi hao wa Tanzania, bado wana nafasi ya kusonga mbele kutokana na historia kuonyesha Mazembe wamekuwa wakitolewa mara kwa mara baada ya kucheza kwao.
Rekodi za Mazembe nyumbani
Rekodi mbalimbali zinaonyesha Mazembe wameshindwa kufanya vizuri katika michezo yao ya nyumbani na kutolewa kwenye mashindano kadhaa.
Historia inaonyesha miamba hiyo ya soka ya Congo tangu mwaka 1969 hadi hivi sasa hawana rekodi nzuri katika michezo ya kimataifa wakiwa nyumbani kwani mwaka huo walitolewa na Ismailiy kwa kufungwa mabao 5-3 ambapo mchezo wao wa kwanza wakiwa Congo walitoka sare ya mabao 2-2 kabla ya kuchapwa mabao 3-1 mchezo wa marudiano.
Hali iliendelea kuwa hivyo mwaka 1970 pale walipoondolewa na Asante Kotoko waliyokutana kwenye fainali na kuchapwa mabao 2-1 kabla ya hapo walishatoka sare ya bao 1-1 wakiwa nyumbani.
Mwaka 2013 walipokutana na CS Sfaxiem, waliondolewa mapema kwenye ligi ya mabingwa baada ya kufungwa mabao 3-2 nyumbani kwao, lakini pia mwaka 2017 waliondolewa mapema katika mashindano hayo na CAPS Uniyed ya Zimbabwe, baada ya mchezo wa kwanza uliochezwa Congo kupata sare ya bao 1-1 kabla ya kuja kutoka sare ya bila kufungana na wenzao kusonga mbele kwa bao la ugenini.
Simba wakiwa ugenini
Pamoja na rekodi za TP Mazembe wakiwa nyumbani, lakini pia Simba wamekuwa moto pale wanapopambana ugenini.
Ukiondoa michezo ya mwaka huu katika hatua za awali, mwaka 1979 katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, waliwastaajabisha watu pale walipoichapa Mufulira Wanderers ya Zambia mabao 5-0 wakiwa ugenini.
Katika mchezo wao wa kwanza Simba walifungwa mabao 4-0 na kukata tamaa lakini waliwachapa wapinzani wao kwa kuwatandika mabao 5-0 nyumbani kwao mjini Lusaka na hivyo kusonga mbele.
Mwaka 2003 baada ya Simba kuichapa BDF XI mabao 4-1, wakianza kushinda bao 1-0 nyumbani kabla ya ushindi wa mabao 3-1 ugenini katika mchezo wa awali wa ligi ya mabingwa, walikutana na Santos ya Afrika Kusini waliwatoa kwa kuwanyuka kwa mikwaju ya penalti 9-8 wakiwa ugenini michezo yote miwili.
Kwenye mchezo wa raundi ya pili Simba ilifanikiwa kuwatoa mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa, Zamalek ya Misri baada ya kuwafunga kwa penalti 3-2 kutokana na mchezo wa kwanza Wekundu wa Msimbazi kufungwa bao 1-0 wakiwa nyumbani kisha nao kwenda kulipiza kwa kuwafunga bao 1-0 ugenini na hivyo kuamuliwa yapingwe matuta.
Simba kusonga mbele inawezekana
Kuna msemo wa wahenga unaosema ‘jitihada hushinda kudra’, hivyo kama Simba wakicheza kwa malengo, nia na kuweka hesabu zao sawa, basi upo uwezekano wa kupenya hatua ya robo fainali.
Hakuna shaka wachezaji na benchi la ufundi wamejipanga kukabiliana na mikiki mikiki watakayokutana nayo Congo kuanzia ndani hadi nje ya uwanja.
Ndani ya uwanja, wachezaji wanapaswa kucheza kwa ushirikiano na kila mmoja anatakiwa kutumia nguvu, akili na juhudi binafsi ili kutimiza majukumu yake kikamilifu.
Hii itawasaidia Simba kupata matokeo chanya kwenye uwanja wa ugenini na kuwapa furaha mashabiki wao ambao wanaiombea timu yao ipige hatua zaidi kimataifa.
Ushindi wa aina yoyote utakuwa na manufaa kwa Simba, kwani utawawezesha kutinga hatua inayofuata ambayo kila shabiki na mwanachana wa klabu hiyo anaitamani.
Kila kitu kinawezekana chini ya jua, kama Simba iliwahi kuvunja rekodi na kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2013, haitashindwa kufika fainali hii sasa ikiwa ina mahitaji yote muhimu.