24.7 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

REAL MADRID KUTOA PAUNI MILIONI 270 KWA NEYMAR

MADRID, HISPANIA             |          


KLABU ya Real Madrid inajiandaa kutoa pauni milioni 270 kukamilisha ada ya uhamisho wa mshambuliaji, Neymar Jr, kutoka Paris Saint Germain (PSG).

Rais wa Real Madrid, Florentino Perez, ana matumaini kwamba vikwazo vya usajili kutoka Chama cha Soka barani Ulaya (UEFA), vitaifanya PSG kumuuza Neymar na wapo tayari kutoa euro milioni 300 kufanikisha uhamisho huo.

Madrid bado haijapata mbadala wa Cristiano Ronaldo, ambaye alijiunga na Juventus kwa ada ya uhamisho ya euro milioni 100 msimu huu, lakini baada ya kipigo cha mabao 4-2 kutoka kwa wapinzani wao Atletico Madrid katika mchezo wa UEFA Super Cup, kuna hofu kwamba lazima klabu hiyo isajili nyota mwingine.

Kabla ya kufungwa kwa dirisha la uhamisho, Madrid imeonekana kuwa tayari kusajili mchezaji wa zamani wa Barcelona, Neymar ikiwa PSG itapewa adhabu kali kwa kukiuka kanuni za matumizi ya fedha katika usajili.

Klabu ya PSG inayomilikiwa na matajiri wa visima vya mafuta kutoka ghuba ya Qatar, chini ya mfuko wa uwekezaji katika michezo nchini Qatar, bado ipo katika uchunguzi wa UEFA kuhusu kiasi cha fedha inacholipwa na wadhamini.

Mwaka 2013, UEFA ilitangaza kuwapo kwa matumizi ya fedha ya kistaarabu katika kusajili ikizitaka klabu kutumia fedha kulingana na mapato wanayoingiza.

Ikifafanua kwamba, fedha zinazolipwa ndani ya klabu na mmiliki wake hazizingatiwi kama mapato na thamani ya udhamini wowote ikiwa na lengo la kuhakikisha kuna haki sawa katika bei ya soko.

Inadaiwa kwamba, Mamlaka ya Utalii ya Qatar hutoa euro milioni 120 kila mwaka katika klabu ya PSG.

Mwaka 2017 uwezo wa kifedha wa PSG ulitikisika baada ya klabu hiyo kutumia pauni milioni 198 kumsainisha Neymar kutoka Barcelona ikifuatiwa uhamisho wa mkopo wa Kylian Mbappe kwa pauni milioni 167.

Uamuzi wa kamati ya rufaa ya UEFA, inatarajia kutolewa mwishoni mwa Agosti mwaka huu.

PSG wanaamini kuwa walifanya kila kitu kwa utaratibu, lakini wanafahamu kwamba wanaweza kukabiliana na vikwazo kwani wana kumbukumbu ya kuadhibiwa kwa kuvunja sheria za matumizi ya fedha mwaka 2014.

Kocha wa Real Madrid, Julen Lopetegui, hatarajii tu mshambuliaji mpya kutua katika timu yake bali hata beki wa kushoto ambapo klabu hiyo ipo katika mipango ya kumsajili, Marcos Alonso, kutoka Chelsea.

Madrid pia inaweza kuwa na mpango mbadala kama dili la kumsajili Neymar likishindikana huenda ikatazama uwezekano wa kumpata Mauro Icardi wa Inter Milan, Rodrigo Machado  wa  Valencia na nyota wa RB Leipzig, Timo Werner.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles