33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

KAGERE, DILUNGA WAIPA SIMBA NGAO YA JAMII

NA DAMIAN MASYENENE-MWANZA                |          


SIMBA imetwaa Ngao ya Jamii, baada ya jana kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mtibwa Sugar katika mchezo uliochezwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Mabao ya Simba yalipachikwa na Meddie Kagere dakika ya 29 na Hassan Dilunga dakika ya 45, huku Kelvin Sabato akifunga bao pekee la Mtibwa Sugar dakika ya 33.

Mchezo huo ulikuwa maalumu kwa ajili ya kuashiria ufunguzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaoanza kutimua vumbi Agosti 22, mwaka huu.

Simba iliuanza mchezo kwa kasi, dakika ya saba, Okwi alimchungulia kipa wa Mtibwa Sugar, Benedicto Tinoco na kutandika shuti kali akiwa nje ya 18, lakini mpira uligonga mwamba wa juu na kutoka nje.

Dakika ya 23, kipa wa Simba, Aishi Manula, alipangua kiki kali ya Awadh Juma wa Mtibwa Sugar.

Dakika ya 29, pasi maridadi ya kiungo Dilunga, ilimkuta Kagere ambaye awalizidi maarifa beki Hassan  Isihaka na kipa  wake  Tinoco na kuiandikia Simba  bao la kuongoza.

Bao hilo liliishtua Mtibwa Sugar ambayo ilizidisha kasi ya mashambulizi kwenye lango la Simba.

Mashambulizi ya Mtibwa Sugar yalizaa  matunda dakika ya 34 pale mshambuliaji Sabato alipoisawazishia bao kwa mkwaju wa mbali uliogonga mwamba wa pembeni na kujaa wavuni.

Baada ya bao hilo, kila upande  uliendelea kupanga mikakati ya kuongeza mabao zaidi.

Dakika ya 45, Dilunga aliifungia bao la pili Simba kwa kiki ya chini, baada ya kutengewa pande la kifua na Okwi.

Hata hivyo, Dilunga hakuonyesha mbwembwe nyingi baada ya kufunga bao hilo, badala yake alinyoosha mikono yake miwili juu, kitendo kilichotafsiriwa  bado anaiheshimu Mtibwa Sugar  alikotokea kabla ya kujiunga na Simba katika  dirisha la msimu ujao.

Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa Simba kwenda mapumziko, ikiwa mbele kwa mabao 2-1.

Kipindi cha pili, Simba ilizidisha kasi ya mashambulizi kwa lengo la kupata mabao zaidi.

Dakika ya 53, mwamuzi Elly Sasii, alimlima kadi ya njano, Rogers Gabriel wa Mtibwa Sugar baada ya kumfanyia madhambi Okwi.

Dakika ya 63, Kocha wa Mtibwa, Zubery Katwila, alifanya mabadiliko alitoka Awadh Juma na kuingia Juma Luizio, kabla ya kocha wa Simba, Patrick Aussems, alimtoa Okwi na kumwingiza John Bocco na kufanya mabadiliko mengine dakika ya 73 kwa kumtoa Shiza Kichuya na kumwingiza Shomari Kapombe.

Aussems alifanya mabadiliko ya mwisho dakika ya 74, alimtoa Dilunga na kumwingiza Mzamiru Yassin, huku Katwila akifanya mabadiliko dakika ya 83 kwa kumtoa Salehe Khamis na kumwingiza Ally Makalani.

Pamoja na mabadiliko yaliyofanywa na kila upande, dakika 90 za pambano hilo zilimalizika kwa Simba kutwaa Ngao ya Jamii kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Kikosi Simba:
Aishi Manula, Nicolaus Gyan, Asante Kwasi, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Jonas Mkude, James Kotei, Hassan Dilunga/ Mzamiru Yassin, Meddie Kagere, Emmanuel Okwi/ John Bocco, Shiza Kichuya/ Shomari Kapombe.

Kikosi Mtibwa Sugar:
Benedict Tinoco, Rodgers Gabriel, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Hassan Isihaka, Cassian Mponera, Shaban Nditi, Ismail Mhesa, Saleh Khamis/Ally Makalani, Kelvin Sabato, Awadhi Juma/Juma Luizio, Salum Kihimbwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles