Na Nathaniel Limu- Singida
WANACHAMA 13 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wamejitokeza kuwania nafasi ya kuteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho, kwenye kinyang’anyiro cha kuwania ubunge Jimbo la Singida Mashariki,baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Tundu Lissu kupoteza sifa.
Waliochuku fomu, ni Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Miraji Mtaturu na Mkuu wa Mkoa Songwe, mstaafu Luteni Chiku Galawa.
Wengine ni Mwanahamisi Mujori, Moris Mukhoty, Shilinde Kasure, Jeremia Ihonde, Lazaro Msaru, Hamisi Maulidi, Mariamu Nkumbi, Martini Lissu, Sylivester Meda, Thomasi Kitima na Emmanuel Hume.
Akitoa taarifa wilayani Ikungi jana, Katibu CCM Wilaya hiyo, Noverty Kibaji alisema leo wanachama hao wataanza kuchuana katika kura za maoni za ndani ya chama na watakaoshinda nafasi tatu za juu, majina yao watawasilishwa vikao vya juu kwa uamuzi.
“Leo (jana), nimekaa nao na kuwasisitiza wahakikishe wanazingatia sheria, kanuni na taratibu za chama. Tofauti na hivyo, watasababisha CCM kichukue maamuzi magumu kwa yule atakayeenda kinyume,”alisema Katibu huyo.