MKUU wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigella, ameiagiza Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Tanga, kusimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri ya Jiji la Tanga.
Shigella alitoa agizo hilo jana kutokana na mgogoro wa madiwani uliopo mjini Tanga uliosababisha kutoundwa kamati za madiwani na kutofanyika kwa vikao vya sheria vya baraza la madiwani.
Alitangaza uamuzi huo wakati wa kikao cha menejimenti ya Halmashauri ya Jiji la Tanga cha kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Shigella alisema kamati hiyo inatakiwa kusimamia miradi hiyo iweze kutekelezwa katika viwango vinavyotakiwa.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa mkoa, hatua hiyo itasaidia kuhakikisha miradi yote inajengwa kwa kuzingatia viwango vyenye ubora na kuzuia ubadhirifu unaofanywa na makandarasi kwenye miradi hiyo.
“Naagiza kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ihakikishe inaongeza ukaribu wa kukagua miradi ya maendeleo kwani najua kwenye migogoro kuna watendaji watakaoweza kutumia fursa hiyo kufanya ubadhirifu kwa manufaa yao.
“Bila kufanya hivyo kuna baadhi ya watendaji watatumia fursa hiyo kufanya ubadhirifu katika miradi na kuisababishia hasara Serikali,” alisema Shigella.
Aliagiza kamati hiyo kuwachukulia hatua za nidhamu watendaji watakaosababisha miradi hiyo kujengwa chini ya viwango na kuitia hasara halmashauri hiyo.
“Mkikuta miradi ipo chini ya viwango anzeni kumshughulikia mtendaji ambaye anapaswa kumsimamia mkandarasi iwe fundisho kwa wengine wenye nia mbaya,” alisisitiza.
Shigella pia alikiri kuwa madiwani wote wa Jiji hilo wamekuwa hawalipwi posho zao hadi watakapomaliza tofauti zao na kuanza vikao vya baraza.
“Hakuna diwani atakayelipwa posho kwa kutumia fedha za umma wakati hana kazi yoyote anayoifanya.
“Lazima tuweke utaratibu mzuri bila kumuonea mtu. Haiwezekani wewe diwani hutekelezi majukumu yako halafu unataka ulipwe posho, nimezuia mpaka hapo watakapoanza kufanya kazi,”alisema.
Hata hivyo, Meya wa Jiji la Tanga, Seleboss Mustafa, alisema licha ya vikao vya madiwani kutofanyika, halmashauri hiyo imekuwa ikiendelea na utekelezaji wa majukumu yake.