29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

RC Songwe awataka wananchi kuchukua tahadhari

Mwandishi Wetu -Songwe

MKUU wa Mkoa wa Songwe, Brigedia Jenerali Nicodemus Mwangela, amewataka wananchi wote wa Mkoa wa Songwe kuchukua tahadhari kwakuwa sasa kumekuwa na wageni wengi wanaoingia katika mkoa huo kutoka katika mikoa mbalimbali hasa yenye wagonjwa wengi wa corona.

Brigedia Jenerali Mwangela, aliyasema hayo jana wakati akipokea mchango wa Sh 280,000 kutoka kwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Jimbo la Magharibi (Songwe) kwa mapambano dhidi ya ugonjwa wa corona.

 “Kwa sasa mkoa wetu umeanza kupokea wageni wengi kutoka mikoa ya Dar es Salaam na hata Zanzibar, hatuwezi kuwazuia kwakuwa nchi yetu ni moja, lakini tusaidiane kutoa elimu ya corona kwa wageni hao na tuchukue tahadhari zote muhimu,” alisema Brigedia Jenerali Mwangela.

Pamoja na hali hiyo, alisema kuwa kila mwananchi akipata mgeni kutoka mikoa hiyo waangalie namna ya kumtengea chumba ili asichangamane na watu wengine au kutoa taarifa kwa uongozi wowote endapo watakuwa na shaka na hali ya afya ya wageni hao ili waweze kujikinga na ugonjwa wa corona.

Aidha amelipongeza Kanisa la KKKT kwa kuwa taasisi ya dini ya kwanza kuchangia mapambano ya corona kwa Mkoa wa Songwe, pia kwa kuchukua tahadhari zote muhimu za kujikinga pamoja na kutoruhusu watoto wahudhurie ibada.

Brigedia Jenerali Mwangela alisema kuwa taasisi za dini ziendelee kuchukua tahadhari na kutoa elimu ya kujikinga na ugonjwa wa virusi vya corona, ikiwa ni pamoja na kuwatembelea waumini majumbani mwao kuwapa elimu hiyo.

Naye Mkuu wa KKKT Jimbo la Magharibi (Songwe), Mchungaji John Mwasakilali, alisema kuwa wanampongeza Rais Dk. John Magufuli kwa kutofunga shughuli za ibada kwa makanisa hayo.

Mchungaji Mwasakilali alisema kuwa wamechukua tahadhari ya kujikinga na ugonjwa wa virusi vya corona kwa kupunguza muda wa ibada hadi kufikia saa moja, kukaa kwa kuachiana nafasi na kunawa kwa maji tiririka na sabuni na kuwa waumini wake wametii maelekezo ya Serikali.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dk. Hamad Nyembea, alisema kuwa fedha hizo zilizotolewa na KKKT zitasaidia kununua baadhi ya vifaa vinavyohitajika katika Kituo cha Afya Nanyala ambacho kimeteuliwa kutoa huduma kwa ngazi ya mkoa endapo atapatikana mgonjwa wa corona.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles