28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, December 1, 2024

Contact us: [email protected]

RC Njombe aishauri TRA kuongeza muda kampeni ya mlango kwa mlango

Na Mwandishi Wetu, Njombe

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhandisi Marwa Rubirya, ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kuishauri kuongeza muda wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi ya mlango kwa mlango, inayoendelea mkoani humo na kusema kuwa wiki moja iliyopangwa haitoshi kutokana na umuhimu wa elimu ya kodi kwa wafanyabiashara.

Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhandisi Marwa Rubirya akizungumza na maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) (hawapo pichani) wakati walipomtembelea ofisini kwake kumjulisha kuhusu kuanza kwa kampeni ya elimu kwa mlipakodi mkoani humo

Akizungumza juzi na timu ya maofisa wa TRA wanaofanya kampeni hiyo mkoani humo, Mkuu huyo wa Mkoa amesema, kutembelea wafanyabiashara duka kwa duka siyo kazi rahisi hivyo inahitaji muda wa kutosha ili kuhakikisha kuwa takribani wafanyabiashara wote wanapata elimu hiyo muhimu.

“Nawapongeza sana TRA kwa kuendesha zoezi hili la mlango kwa mlango katika mikoa mbalimbali na hatimaye mmefanikiwa kufika hapa Njombe. Lakini huu muda wa wiki moja hautoshi nashauri siku nyingine mpange siku za kutosha ili kila mfanyabiashara aweze kunufaika na elimu hii,” alisema Mhandisi Rubirya.

Ameongeza kuwa, elimu inayotolewa na TRA itasaidia kuongeza kasi ya ukusanyaji wa kodi kwa manufaa ya nchi na kuchochea maendeleo.

“Kama kuna eneo ambalo linasaidia katika ukusanyaji kodi ni kuhakikisha wafanyabiashara wengi zaidi wanakuwa na elimu ya kodi ambayo itawasaidia kuongeza uelewa na hatimaye kujisikia fahari kwenda kulipa kodi”, alisisitiza Mhandisi Rubirya.

Kwa upande wa baadhi ya wafanyabiashara wa mkoani hapa baada ya kutembelewa na maofisa wa TRA wanaofanya kampeni hiyo akiwemo, Bahati Mtweve, alisema kwamba, utaratibu huo ni mzuri na utasaidia kuwapa elimu ya kutosha wafanyabiashara wengi mkoani hapa na kuacha mazoea ya kuogopa maofisa wa TRA pindi wanapokuwa wanapita kwenye maeneo ya biashara zao.

“Kwa utaratibu huu, nadhani hakuna mfanyabiashara yeyote atakayekuwa anawaogopa TRA kwa kuwa wengi watakuwa na uelewa wa kutosha na watahamasika kulipa kodi kwa wakati,” alisema Mtweve.

Naye, Winifrida Mponela, alisema elimu inayotolewa na TRA katika kampeni hiyo, imewasaidia kufahamu zaidi juu ya utunzaji wa kumbukumbu na kwamba kwa upande wake, kuja kwa maofisa wa TRA mkoani hapa, kutawawezesha wafanyabiashara kujua mambo mengi yanayohusu kodi.

“Kwetu sisi tumeona ni faida sana kutembelewa na maofisa wa TRA kwani wametupatia elimu ya matumizi sahihi ya mashine ya EFD kama sehemu ya utunzaji wa kumbukumbu na hii itatuepusha na faini zisizo za lazima ambazo mtu anapewa kwa kosa la kutokutoa risiti,” alisema Mponela.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara mjini Njombe, Eliud Pangamawe, alitoa ombi kwa maofisa wa TRA akiwemo Meneja wa Mkoa wa Njombe, Shabani Musibu kuendelea kufanya zoezi hilo kila wakati ili kuondoa dhana iliyokuwa imejengeka hapo awali kwamba, TRA ni adui wa wafanyabiashara.

“Mnatakiwa kufanya kampeni hii mara kwa mara ili kuongeza ukaribu na urafiki kati yetu sisi na ninyi na pia kuondoa dhana potofu ya kusema ninyi ni maadui zetu,” alisema.

Kampeni ya elimu kwa mlipakodi mkoani Njombe imelenga kuwajengea uelewa wa kutosha wafanyabiashara na walipakodi kwa ujumla juu ya masuala mbalimbali yanayohusu kodi, kusikiliza maoni yao kwa ajili ya kuboresha huduma za TRA, kuwakumbusha kulipa kodi stahiki na kwa wakati, kusikiliza changamoto za kikodi walizonazo na kuzitafutia ufumbuzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles