Na Clara Matimo, Mwanza
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, ameiasa jamii kuendelea kuweka msisitizo katika Afya ya Mama na Mtoto kwa kuhakikisha changamoto ya uhaba wa damu kwa mama wajawazito inatatuliwa, huku akisisitiza kampeni ya tohara kwa wanaume isipuuzwe.
Mhandisi Gabriel ametoa wito huo jijini hapa Julai 28, wakati akifunga kikao cha siku mbili kilicholenga kujadili na kuweka mikakati itakayowezesha kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga, kuboresha hali ya lishe katika jamii ili kupunguza udumavu kwa watoto, kupunguza maambukizi  ya virusi  vya ukimwi na maandalizi ya kutoa chanjo mpya ya covid-19 ambacho kiliwakutanisha wataalamu na wadau wa afya ndani ya mkoa huo.
Amesema mkoa wa Mwanza  bado unachangamoto ya vifo vitokanayo na uzazi kwani kwa mujibu wa Takwimu mwaka 2020 kulikuwa na vifo 157 na mwaka huu hadi kufikia Juni vifo 79 vimeishatokea,  miongoni mwa sababu zinazosababisha wanawake kupoteza maisha ni kutoka damu nyingi baada ya kujifungua na kifafa cha mimba ambazo zinaweza kupatiwa ufumbuzi.
“Tutoe elimu na kuwahamasisha wananchi katika maeneo mbalimbali ikiwemo vyuoni, shuleni na kwenye nyumba za ibada ili wachangie damu kwa hiari, tukifanya hivyo tutakuwa na benki ya damu ya kutosha ambayo itasaidia sana kuokoa maisha ya mama endapo atatokwa damu nyingi baada ya kujifungua.
“Lakini pia tumekuwa tukipata vifo vinavyotokana na uzembe kwa kutowajibika kwa baadhi ya watoa huduma za afya, naagiza kila wilaya kutoa taarifa ya kifo cha mama na mtoto iwapo kitatokea, taarifa hiyo iainishe sababu za kifo kama ni uzembe mhusika atajwe  ili tumuwajibishe,” alisema na kuongeza;
“Nanyi waandishi wa habari endeleeni kuihamasisha jamii ili mwanamke anapopata ujauzito azingatie kuwahi kuhudhuria Kliniki kwa kufanya hivyo atakuwa kwenye usalama zaidi maana endapo anachangamoto ya kiafya hata wataalamu wa afya watakuwa na muda wa kuitatu, hivyo wote tuliohudhuria kikao hiki tutoke na kauli mbiu isemayo ‘Mimi na wewe tunawajibika kwa usalama wa afya ya mama na mtoto,” Â amesema Mhandisi Gabriel.
Akizungumzia tohara kwa wanaume aliitaka jamii kutopuuza  maana inasaidia kujikinga na maradhi mbalimbali.
“Wataalamu wa afya wanatwambia mwanaume ambaye hajafanyiwa tohara yuko kwenye hatari ya kupata maambukizi ya VVU endapo atashiriki tendo la ndoa na mwanamke mwenye maambukizi kuliko aliyefanyiwa tohara, wito wangu, kampeni ya tohara inaendelea ndani ya mkoa wetu tuendelee kuihamasisha jamii ili ambao bado wafanyiwe,” amesema.
Naye, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Lutengano Mwalwiba, amesema atahakikisha maazimio yote waliyopitisha katika kikao hicho yanatekelezwa ikiwemo kuwaelimisha wananchi kuhusu faida za chanjo kwa kuwapa elimu sahihi ili wajitokeze kwa wingi kuchanjwa itakapozinduliwa mkoani Mwanza kwa kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakiwapa hofu wakati si wataalamu wa masuala ya afya.
“Tutaendeleza  kwa juhudi kubwa kampeni ya mkoa nilinde nikulinde, tumeishaweka utaratibu asiye na barakoa hakuna kupata huduma,” amesema.