23.6 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

RC Mwanza aonya watumishi wa umma kujilimbikizia vyumba vya Biashara

*Ni katika maeneo ya Soko kuu, Stendi ya mabasi

Na Clara Matimo, Mwanza

Ili kuhakikisha kunakuwa na usawa na kuondoa urasimu katika utoaji wa vyumba vya biashara kwenye miradi mipya ya Soko Kuu la Jiji la Mwanza na Stendi Kuu ya Mabasi yaendayo mikoani ya Nyegezi, watumishi wa umma wametahadharishwa kutojirundikia vyumba kisha kuvipangisha kwa bei ya juu.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, akiwa katika ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa soko kuu la mjini kati linalojengwa wilaya ya Nyamagana mkoani humo.

Onyo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel,  Mei 10, mwaka huu wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miradi hiyo inayojengwa wilaya ya Nyamagana mkoani humo.

Alisema serikali inatekeleza miradi kwa lengo la kuwanufaisha wananchi wake na kuweka bei ya chini ili waweze kumudu gharama za uendeshaji wa biashara zao lakini  baadhi ya watumishi wa umma  wenye tamaa na wanaopenda kujinufaisha wenyewe wanakuwa madalali.

“Mkuu wa wilaya  ya Nyamagana unafahamu,  tulikuwa wote pale makoroboi tulikuta kibanda cha halmashauri cha 200,000 walioko mle ndani wanamlipa tajiri Sh 1,000,000 ina maana anachukua cha juu Sh 800,000, akiwa na  vibanda 10 anaingiza Sh milioni nane kwa mwezi mshahara ambao hata mkuu wa mkoa haupati mtu mmoja ametulia anawanyonya wananchi.

“Kiwango kisiwe kikubwa sana cha kumuumiza mfanyabiashara wala kisiwe kidogo cha kuvutia watu wachache kutumia mwanya huo  kujinufaisha, twende  na bei halisi ya soko, fedha lazima zirudi kwenye baadhi ya maeneo lakini wafanyabiashara wanufaike,”alisema Mhandisi Gabriel.

Mhandisi wa jiji la Mwanza, Tunaye Mahenge, alisema  miradi yote miwili ujenzi wa soko kuu la mjini kati ambao umetekelezwa kwa asilimia 73 na stend kuu ya mabasi nyegezi uliofikia asilimia 85 ilitarajiwa kukamilika Aprili mwaka huu lakini imekwama kutokana na changamoto mbalimbali.

Alizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na eneo kuwa na chem chem ya maji kutoka chini hali iliyosababisha kubadili mchoro wa msingi ili uendane na hali ya eneo katika mradi wa ujenzi wa stendi kuu ya mabasi nyegezi, upandaji horera wa bei za vifaa vya ujenzi unaoweza kuongeza gharama za utekelezaji wa miradi hiyo, vifaa kutopatikana kwa wakati kutokana na ugonjwa wa uviko 19.

“Changamoto hizo zimesababisha mkandarasi Mohammedi Builders Ltd, anaetekeleza mradi wa ujenzi wa soko kuu la mjini kati kwa gharama ya Sh bilioni 20,739,695,080  aombe kuongezewa muda wa miezi mitano huku mkandarasi wa stendi ya nyegezi  anayetekeleza mradi huo kwa gharama ya Sh bilioni 15, 885, 589,063 yeye ameomba  aongezewe muda wa miezi mitatu.

Mradi wa ujenzi wa soko ulianza kutekelezwa Oktoba, 2020 huku wa stend ya mabasi nyegezi ukianza Februari 5, 2019 lengo likiwa ni kuboresha huduma, kuongeza mapato ya halmashauri ya Jiji la Mwanza ili iweze kujitegemea na kupunguza utegemezi kutoka serikali kuu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles