22.2 C
Dar es Salaam
Monday, September 25, 2023

Contact us: [email protected]

CCM wapigilia msumari uamuzi wa RC Kafulila

Na Derick Milton, Simiyu

Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Simiyu kimeunga mkono maamuzi yaliyofanywa na Mkuu wa Mkoa huo, David Kafulila ya kuvunja bodi zote za vyama vya msingi vya ushirika 335 mkoani humo na kuagiza ndani ya wiki moja ufanyike uchaguzi wa kuwapata viongozi wapya.

Wakizungumza na waandishi wa habari leo Mei 12, 2022 mara baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Mkoa, Viongozi wa Chama hicho wamesema kuwa maamuzi ya mkuu huyo wa mkoa yako sahihi na wameunga mkono asilimia 100.

Mweyekiti wa CCM Mkoa, Shemsa Mohamed amesema kuwa licha ya chama hicho kwenye ilani yake kuutambua ushirika kuwa ndiyo mkombozi wa mkulima, changamoto kubwa imekuwa ni viongozi wa ushirika kuendelea kuwaibia wakulima.

Amesema kuwa maamuzi ya mkuu wa mkoa ya kuwaondoa viongozi wote wa vyama vya ushirika yanatokana na maagizo ya chama hicho ambayo waliyatoakwake kuhakikisha anasafisha ushirika katika mkoa huo.

Amesema kuwa bado wakulima wameendelea kuibiwa kupitia mizani, bei halisi ya pamba lakini pia wengine wakitumia vibaya nafasi zao kwa kusababisha hasara kwenye vyama hivyo na kujinufaisha wao wenyewe.

“Ushirika ni Ilani ya CCM, lengo lake kubwa ni kumnufaisha mkulima na siyo kumyonya, kama chama tutaendelea kuusimamia ushirika ambao unanumfaisha mkulima na siyo kumyonya, wale viongozi ambao ni Mungu mtu kwenye ushirika hatutawafumbia macho.

“Kwa kauli moja tunamuunga mkono mkuu wa mkoa, ili tuweze kupata viongozi wengine wapya ambao watakwenda kumsaidia mkulima, na ili haya yaweze kufikiwa ni lazima kama ambavyo mkuu wa mkoa ameagiza, wakulima wote washiriki katika uchaguzi nasi tunaunga mkono, wakulima wote washiriki uchaguzi ili tuwapate viongozi bora,” amesema Shemsa.

Nae Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Gungu Silanga amesema kuwa wakulima kwa muda mrefu wameibiwa sana kupitia kwa viongozi wa ushirika ambao siyo waaminifu hivyo kupitia maamuzi ya mkuu wa mkoa suruhisho litapatikana.

Amesema kuwa kama chama hawako tayari kuona kikundi cha watu wachache (Kikundi cha harusi) wakipinga maamuzi ya mkuu wa mkoa kwa kuendelea kukumbatia wizi kwenye vyama vya msingi vya ushirika.

“Wakulima wameibiwa sana hasa kupitia bei ya pamba lakini pia kupitia mizani, leo wanatokea watu eti wanapinga maamuzi ya mkuu wa mkoa ili wakulima waendelee kuibiwa, kama chama tunamuunga mkono mkuu wa mkoa ili wapatikane viongozi wa Mkoa,” amesema Gungu.

Katika maamuzi hayo ya Mkuu wa mkoa, aliwaagiza pia wakurugenzi wa halmashauri zote 6 mkoani humo kuwaondoa katika nafasi zao maofisa ushirika wote na kuwekwa wapya.

Hata hivyo tangu Kafulila atoe maagizo hayo zikiwa zimepita siku 7, hakuna uchaguzi wowote wa chama cha msingi cha ushirika ambao umefanyika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,717FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles