Na Clara Matimo, Mwanza
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Mkoani humo kwa kupunguza hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa asilimia 38 kwa mwaka wa fedha 2019/2020 hadi 2020/2021 pamoja na kupata hati safi kwa iaka sita mfululizo.
Mhandisi Gabriel ametoa pongezi hizo leo Jumatatu Juni 20, 2022 baada ya Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Mhandisi Modest Apolinary, kusoma taarifa ya hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa nje (CAG) kwa mwaka wa fedha 2020/2021 pamoja na utekelezaji wake katika mkutano maalumu wa baraza la madiwani uliolenga kujadili hoja hizo.
Mhandisi Apolinary alisema katika kikao cha kupitia hoja za CAG kwa mwaka wa fedha 2019/2020 halmashauri hiyo ilikuwa na hoja 60 lakini katika kikao cha mwaka huu cha kupitia hoja za mwaka 2020/21 ina hoja 37 huku akifafanua kwamba zimepungua kwa asilimia 38 .
“Upungufu huo umetokana na usimamamizi mzuri wa kamati ya fedha, baraza la madiwani, ofisi ya mkuu wa wilaya na mkoa, haya yote yameiwezesha halmashauri yetu ya manispaa ya Ilemela pia kupata hati safi kwa kipindi cha miaka sita mfululizo kuanzia mwaka wa fedha 2015/16 hadi 2020/2021.
“Sababu ya kupata hati hiyo ni ushirikiano baina ya wataalamu, madiwani, ofisi ya mkuu wa wilaya na mkoa katika kuhakikisha halmashauri inaendeshwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu, mwaka 2019/2020 hoja zilikuwa zimebaki 14, hoja sita zimefungwa, tatu ziko kwenye utekelezaji, tatu ni hoja za kujirudia na mbili zimepitwa na wakati,” ameeleza Mhandisi Apolinary..
Aidha amefafanua kwamba zoezi la uhakiki kwa hoja tatu zilizo kwenye utekelezaji kati ya 14 za miaka ya nyuma, 11 zimefungwa na kwa mwaka wa fedha 2020/2021 hoja ni 23, kati ya hizo 13 zimefungwa, nane ziko kwenye utekelezaji, mbili ni za kujirudia.
“Hivyo, kati ya hoja 37 za miaka ya nyuma na za mwaka 2020/2021, 26 zimefungwa halmashauri imebaki na hoja 11 ambazo zote ziko kwenye hatua ya utekelezaji lengo letu ni kuhakikisha zote zinafungwa,”alisema.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masala, Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli, alisema mwaka wa fedha 2022/2023 hawatakuwa na hoja hata moja ya kujibu kwani watakuwa makini zaidi kwa kufuata maelekezo na ushauri wa madiwani.
Baada ya maelezo hayo Mhandisi Gabriel aliwapongeza na kumuagiza mkurugenzi huyo kukaa na mkaguzi wa ndani wajadiliane ili wafute hoja zote 11 zilizobaki maana nyingi ni dhaifu huku akiwasisitiza kufuata ushauri watakaopewa na CAG.