26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Makala| Hatari inayowanyemelea wajawazito Lindi, ni wanaotumia tiba asili kujifungua

*Katika kila wajawazito 10 basi 6 wanatumia dawa hizo

*Inasababisha wengi wao kufika hospitali mfuko wa uzazi ukiwa umechanika

Na Hadija Omary, Lindi

Zaidi ya asilimia 90 ya akinamama wajawazito wilayani Ruangwa mkoani Lindi wanadaiwa kutumia dawa za asili kwa ajili ya kuongeza njia za uzazi na kuongeza kasi ya uchungu jambo ambalo ni hatari kwa afya zao na watoto walio tumboni

Akizungumza na Mtanzania Digital ofisini kwake, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Ruangwa Mjini, Dk. Ezekia Ambikile, ambapo amesema kuwa changamoto hiyo ni kubwa jambo linalohatarisha usalama wa mama na mtoto aliyeko tumboni.

Baadhi ya akina mama wakizubiri huduma katika Kituo cha Afya Ruangwa.

Dk. Ambikile amesema tatizo hilo la matumizi ya dawa za asili kwa akina Mama wanaokwenda kujifungua katika maeneo mbalimbali  ya vituo  vya afya na zahanati ndami ya Halmashauri  hiyo ni kubwa.

“Kati ya akina Mama 10 wanaokwenda kujifungua, 6 hutumia dawa hizo ambapo akinamama 3 kati yao hulazimika kufanyiwa upasuaji kutokana na hali ya uchungu wanaofika nao,” amesema Dk. Ambikile.

Amefafanua zaidi kuwa pamoja na dawa hizo kuonekana kuwa na ufanisi mkubwa kwa kina mama hao, lakini ni jambo la hatari kwani baadhi yao wanapofika kwenye vituo hivyo vya kutolea huduma wanakuwa na uchungu mkali ambo wakati mwingine huhatarisha maisha ya mama na mtoto.

“Kibaya zaidi kuna akina mama wengine ambao wanatumia dawa hizi wakiwa hawana vigezo kiasi kwamba njia inakuwa haitoshi lakini wanakuwa washatumia dawa hizo kwa matumaini kwamba atajifungua kwa njia ya kawaida.

“Katika hili wengine wanakuwa wameshafanyiwa oparesheni za awali, jambo ambalo kwa mama ambae alishafanyiwa upasuaji hatakiwi kutumia dawa yoyote ya uchungu huku njia ambayo ni muafaka kabisa inayoweza  kumsaidia kujifungua ni kufanywa oparesheni nyingine,” amebainisha Dk. Ambikile.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.

Dk. Ambikile anaeleza kuwa jambo lingine la hatari ni akina mama waliowengi kufika hospitalini mfuko wa uzazi ukiwa katika hatua za mwisho za kuchanika na wengine kufikia waka ukiwa umeshachanika tayari hali inayosababisha mtoto aliyetumboni kupoteza maisha.

Mkazi wa Nachingwea Halmashauri ya Ruangwa mkoani Lindi anasema kuwa dawa hizo ni za asili na urithi kutoka kwa Mababu zao nakwamba wamekuwa akizitumia vizazi na vizazi pindi tu wanapokuwa wajawazito.

Anasema kwa kutumia dawa hizo wamekuwa wakipata urahisi wakati wa kujifungua nakwamba huchukua muda mfupi tangu uchungu unapoanza mpaka mtoto kuzaliwa.

Upande wake Muuguzi wa akina mama, Mwanahamisi Ahmad aliefika kujifungua katika kituo hicho cha Afya Ruangwa Mjini ameiambia Mtanzania Digital kuwa wamekuwa wakitumia dawa hizo pindi wanapokuwa na ujauzito kuanzia miezi saba, nane hadi tisa nakwamba matumizi ya dawa hizo yanatofautiana baina ya mtu na mtu

“Dawa hizi tunazitumia pindi ujauzito unapofikisha miezi saba, nane au tisa ila dawa hizi huwa zinatofautiana, kuna zingine za kujifusha au kunawa ukeni kwa ajili ya kuongeza nji na zingine kuoga ama kunywa, zipo nyingi ambazo huwa tunazitumia kupaka kwenye tumbo kuelekea chini, dawa hizi zinatumika mara mbili kwa siku yaani asubuhi na jioni,” anasema Mwanahamisi.

Lovenes Njinjo ni Mama aliejifungua Watoto mapacha katika Kituo cha Afya Ruangwa ambaye anakili kutumia dawa hizo za asili kabla ya kujifungua.

Anasema licha ya watoto wake hao wawili kutanguliza miguu wakati wa kujifungua lakini alijifungua salama.

“Mimi nilivyokuja hapa sijasumbuka sana kivile, nilitumia dawa tu za miti shamba na majani, nilinawa kabla ya kuja hapa, hivyo njia ilikuwa imejionyesha toka jana nilipokuja sema nilichukua muda kidogo kwa kuwa huyu mmoja ndio alikuwa anasumbua sana kumngojea mwenzie na hata alivyokuja huyo walianza kutanguliza miguu siyo kichwa lakini wote walitoka salama,” anasema Lovenes.

Kwa upande wake  Muuguzi Mkunga wa kituo cha Afya Ruangwa, Tusajigwa Mwaisaka anasema kuwa wakati mwingine watoto hupoteza maisha kutokana na kunywa maji hayo ya dawa ambayo hutumika na mama zao kwa ajili ya kuongeza uchungu kabla ya kujifngua.

Takwimu zikoje?

Hata hivyo, Dk. Ambikile anaeleza kuwa pamoja na kuwepo kwa hatari ya mama na mtoto kupoteza maisha kutokana na matumizi ya dawa hizo, kwasasa wao kama Kituo cha Afya bado hawa takwimu maalumu zinazohusisha changamoto hiyo.

“Kama nilivyoeleza jambo hili katika wilaya yetu ni kubwa japo hatujawa na takwimu halisi za vifo vya akina mama na watoto vilivyotokana na matumizi ya dawa hizi lakini hii kwetu bado ni changamoto kubwa,” anasema Dk. Ambikile.

Dawa hizi zinaitwaje?

Amina Selemani (75) ni Mmoja ya Wakunga wa jadi wilayani humo ambaye anasema kuwa dawa hizo za asili amekuwa akizitoa kwa akina mama wajawazito wenye mahitaji ambapo amedai kuwa akiwapa maelekezo ya matumizi kadri mimba inavyozidi kukua.

Hata hivyo, Amina anasema kuwa kwa kuwa yeye alirithi shughuli hiyo kutoka kwa Bibi yake hakuweza kutambua dawa zote zaidi ya ile moja tu ya Mtambatamba ambayo hutumika kwa kunawa sehemu za siri kwa mama mjamzito huku zingine za kufusha, kupaka na kuoga akieleza kuwa huzitambua kwa kuona mti wake tu.

“Mimi ujuzi wa dawa hizi nilirithishwa kutoka kwa bibi yangu na alinionyesha majani na mti huu wa mtambatamba, nimeutambua kwa jina kwa sababu pamoja na matumizi hayo pia ikiwa tupo jangwani, huna maji tukiukuta tunakata na maji yake yanayotoka tulikuwa tunakunywa enzi hizo tukiwa watoto,” anasema Amina.

Kwa mujibu wa Amina, mti huo wa mtamba kwa asili unaota jangwani ambapo ukikatwa hutoa maji kama ilivyo bomba lililokatika, maji yake ni masafi na baridi japo ukiyakinga na kuhifadhi kwenye chupa ama chombo chochote huwa yanabadilika kuwa ya utelezi kama ute wa mayai mabichi au maji ya bamia zilizolowekwa 

Inadaiwa akina mama hao hutumia maji ya mtamba kunawa ama kipande cha mti huo kukiloweza kwenye maji ili kupata angalau utekezi endapo watakosa maji hayo ili kuweka kilainishi kwenye njia ya uzazi.

Usanifu ukionyesha kwanini in ahitajika nguvu kubwa kuwekeza kwa Wakunga ili kuokoa maisha ya akina mama. (Picha kwa hisani ya Mtandao wa Gazetini).

Hii ni bayana kwamba Serikali bado ina kazi kubwa ya kuhakikisha kuwa inatoa elimu juu ya afya ya uzazi ili kuokoa vifo vinavyotokea wakati na baada ya kujifungua.

Hili pia linapaswa kwenda sambamba na kuimarisha uwekezaji kwa Wakunga ili kupunguza hatari ya vifo vinavyotokana na kujifungua.

Takwimu zinaonyesha kuwa maisha ya wanawake 556 kati ya kila wanawake 100,000 hupotea wakati wa kujifungua.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles