27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

RC Mwanza aanza kudhibiti upigaji mikopo ya Halmashauri

*Ni ile ambayo Watumishi wa Umma walijikopesha

*Pia baadhi ya vikundi vilipewa mikopo mara mbili

Na Clara Matimo, Mwanza

Siku chache baada ya kubainika uwepo wa upotevu mkubwa wa fedha za mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya ujasiriamali kutoka katika makundi maalum mkoani Mwanza ambapo vikundi hewa 30 vilibainika kukopeshwa fedha huku zaidi ya Sh bilioni 4.9 zilizokopeshwa kuanzia mwaka 2017/18 hadi Februari 2021/22 zikiwa hazijarejeshwa, Mkuu wa Mkoa huo, Mhandisi Robert Gabriel, ameanza kuchukua hatua.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, akitoa elimu ya fedha kwa watendaji wa halmashauri za Wilaya za Nyamagana na Ilemela mkoani humo wanaoratibu mikopo ya asilimia 10 kwa makundi maalum pamoja na viongozi wa vikundi vilivyoomba mikopo hiyo.

Hatua hizo ni kwa ajili ya kuepusha fedha hizo kuendelea kupotea hewani bila kuwanufaisha walengwa ambao ni wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Akitangaza hatua hizo Mei 11, mwaka huu alipokuwa akitoa Semina kwa Watendaji wa Halmashauri za Wilaya za Nyamagana na Ilemela mkoani Mwanza wanaoratibu mikopo hiyo, Mhandisi Gabriel amesema watumishi wa umma walijikopesha fedha kinyume na sheria za mikopo hiyo huku baadhi ya vikundi vikipewa mikopo wakati havijamaliza kulipa ile ya awali.

“Kati ya kipindi cha miaka mitano  2017/18 hadi Februari 2021/22  zaidi ya  ya Sh bilioni 8.9 ambazo zinatokana na mapato ya ndani ya halmashauri zilitolewa kama mkopo kwenye vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kati ya hizo  Sh bilioni 4.4 zilirejeshwa hadi sasa kiasi cha Sh bilioni 4.9 hazijarejeshwa hizi ni pesa nyingi zaidi ya asilimia 50 ya fedha yote iliyokopwa haijarejeshwa.

“Fedha yoyote ile  duniani yenye utaratibu wa kisheria haitoki hadi vigezo vya kisheria vyote vimekidhi ndipo mtu wa mwisho ambaye ni wa fedha atoe fedha hiyo, sasa kuna maswali bado tunaendelea kuyafanyia kazi, pesa ilitokaje wakati kikundi hakijakidhi vigezo? Fedha ilitokaje wakati kamati zinazosimamia na kupitisha mikopo hazijakaa?,”amesema na kuongeza:

“Ukiwa na sheria, taratibu na kanuni hauwezi ukatoa fedha bila kufuata mchakato, yule mtoa fedha hatoi fedha tu kwa sababu kuna kikundi anatoa fedha kwa sababu kikundi kimekithi vigezo vya kukopesheka, sasa mimi kama mkuu wa mkoa najiongeza ingawa kwenye sheria ya mikopo hiyo mwanasheria hajahusishwa lakini mimi nitamuweka ili kabla mtoa fedha hajatoa fedha kwa kikundi chochote kile mwanasheria lazima ajiridhishe naamini njia hii pia itatusaidia kudhibiti upotevu huo wa fedha za umma,”alisema Mhandisi Gabriel.

Aidha, Mhandisi Gabriel aliwata watumishi wa umma na wanavikundi waliokopeshwa fedha hizo lakini bado hawajazirudisha wazirejeshe mapema ili na wengine wanufaike nazo kwani  serikali haikuwapa kama zawadi wala haikutoa sadaka.

“Inaumiza sana hizi Sh bilioni 8.9 ambazo zimeishatolewa na serikali kama mikopo kwa makundi haya hata kama wangejenga viwanda vyenye thamani ya  Sh milioni 100 kila kimoja mkoa huu leo ungekuwa wa mfano  uchumi ungepanda na wanachi maisha yao yangeboreka sana.

Amesema kuanzia sasa wanavikundi watakaopewa mikopo ni wale watakaopewa elimu ya fedha na serikali mkoani humo na watatambuliwa kwa kupewa vyeti maalumu  ili wakichukua mikopo hiyo iwe na tija kwao, binafsi, familia zao na taifa kwa jumla.

“Kumpa mtu fedha ya mkopo bila kumpa elimu ni sawa na kumpa leseni dereva ambaye hajafuzu halafu  unamwambia aendeshe scania au fuso unamuangamiza yeye na mali uliyompa inaangamia hata timiza lengo lake, inatakiwa wajue kanuni taratibu na miongozo sahihi ndipo tuwape mikopo,”amesema Gabriel.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles