26.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 21, 2024

Contact us: [email protected]

Bloomberg Media Initiative Africa yazindua awamu ya pili mafunzo uandishi habari za fedha Tanzania

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

TAASISI ya Bloomberg Media Initiative Africa (BMIA) imetangaza kuanza kwa awamu ya pili ya programu ya mafunzo ya uandishi wa habari za masuala ya fedha (FJT) kwa waandishi nchini Tanzania.

Mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha jumla ya waandishi wa habari 50 wa masuala ya fedha na biashara kuandika habari za kina zinazohusu sekta hizo.

Awamu hiyo ya pili inafanyika baada ya mafunzo hayo kusimama kwa miaka miwili kutokana na changamoto za ugonjwa wa UVIKO-19.

Mafunzo hayo yanaendeshwa kwa ushirikiano kati ya Shule Kuu ya Biashara ya Strathmore ya nchini Kenya, Shule Kuu ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Shule Kuu ya Habari na Mawasiliano ya Umma ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam.

Kurejewa kwa mafunzo hayo kunatokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika awamu ya kwanza iliyofanyika 2019 ambapo waandishi wa habari 40 walipata taaluma mbalimbali kuhusiana na uandishi wa habari za masuala ya fedha na biashara.

Katika awamu ya pili kutakuwa na waandishi wa habari 50 kutoka vyombo vya serikali, sekta binafsi, taasisi zisizokuwa za kiserikali na vyombo vikubwa vya habari.

Pia imeelezwa kuwa mafunzo hayo ya miezi sita yatahusisha mada mbalimbali zikiwamo uchambuzi wa data, masoko ya hisa, uhasibu, sera, uchumi na hivyo kuwezesha mabadiliko ndani ya vyombo vya habari ya namna ya kuandika habari za masuala ya fedha na biashara.

Mafunzo hayo yatatolewa na waandishi wa habari wa Bloomberg News na shule zilizotajwa. Mafunzo hayo yamelenga kuhakikisha kwamba kunakuwa na uwajibikaji, uwazi na utawala bora.

Mafunzo hayo ni sehemu muhimu ya BMIA kuchangia maendeleo katika uandishi wa habari za fedha na biashara barani Afrika, kwa kutambua umuhimu wa vyombo vya habari katika kuleta uwazi, uwajibikaji na utawala bora.

Akizungumzia mafunzo hayo Mkurugenzi  BMIA, Erana Stennett, alisema: “Tumefurahishwa na kurejea tena katika kutoa mafunzo ya programu baada ya miaka miwili. Tunaamini kwa kuwapa waandishi wa habari ujuzi na maarifa ili kuripoti vyema masuala ya biashara na fedha tunachangia ukuaji wa uchumi na maendeleo ya Tanzania,” amesema.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Gavana wa Benki Kuu (BoT) Profesa Florens Luoga alisema: “Katika kipindi hiki kigumu baada ya janga la corona, uandishi thabiti wa habari za kibiashara na kiuchumi ni msingi mkubwa wa kuweza kuwafahamisha wadau ili kuweza kuwa na msukumo mkubwa wa ukuaji wa uchumi.

“Kwa kutoa mafunzo kwa wanahabari zaidi, BMIA inachangia maendeleo ya kiuchumi ya Tanzania.”

Kuzinduliwa kwa awamu ya pili nchini kunafuatia kuwapo kwa mafanikio makubwa ya programu hiyo kwa nchi za Kenya, Nigeria, Afrika Kusini, Ghana, Zambia, Ivory Coast na Senegali, ambapo zaidi ya waandishi 600 wamepatiwa mafunzo hayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles