26.1 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

RC Mwanri na enzi za Al Sahhaf

Na KULWA KAREDIA-TSJ

MWAKA 2003, wakati Marekani ilipoivamia nchi ya Irak kijeshi, kulikuwa na waziri mmoja mwenye maneno mengi kiasi kwamba aliwaaminisha wananchi wake kuwa hatapata mkong’oto kutoka kwa majeshi ya wavamizi.

Kiongozi huyo alikuwa hodari wa kuzungumza na waandishi wa habari kila siku, kwa nia moja tu ya kuwapasha Wairak juu ya majeshi yao yanavyodhibiti majeshi ya Marekani ili yasiingie katika mji mkuu wa nchi hiyo, Baghdad.

Huyo si mwingine bali ni Waziri wa Habari, Mohammed Saeed al-Sahhaf, ambaye alijitoa ‘mhanga’ kuwahadaa wananchi wake na ulimwengu mzima kwamba endapo majeshi ya Marekani yangejaribu kuvamia uwanja wa ndege wa Baghdad au mji mkuu wao, wangefyekwa vibaya, jambo ambalo watu waliamini, kumbe ilikuwa ni kinyume chake.

Hata alipotiwa mbaroni na majeshi ya wavamizi, Rais wa Marekani wakati huo, George W. Bush, aliagiza aachiwe kwa kile alichodai huyo ni mtu mwema, rafiki ambaye alitimiza majukumu yake kisawasawa.

Akiwa katika majukumu yake ya propaganda hizo, huko nyuma tayari wanajeshi wa Marekani walikuwa wameuteka uwanja wa ndege, huku wengi wakikaribia kabisa kuingia mjini Baghdad kuelekea Ikulu ya Rais Saddam Hussein.

Leo sina nia ya kuelezea kwa kirefu suala hili, lakini nimeanza hivi kutaka kukupa picha msomaji wangu namna ambavyo hivi sasa tumempata ‘Al Sahhaf’ mpya ambaye amekuwa akiwavunja mbavu Watanzania.

Kwa kipindi kirefu nimekuwa nikifuatilia utendaji wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Agrey Mwanri, nimebaini amegeuka kuwa Al-Sahhaf kwa sababu ya kauli ambazo amekuwa akitoa.

Ni kiongozi ambaye anakwenda kwenye majukumu yake akiwa na timu nzima ya ulinzi na usalama ya mkoa, lakini kauli anazotoa wakati mwingine sikubaliani nazo kwa sababu anatumia nguvu kubwa kupita kiasi.

Licha ya kutumia nguvu kubwa, amekuwa akitoa misemo ambayo kwa kweli yeye kama kiongozi wakati mwingine lazima awe anaichuja kwanza. Hivi sasa amekuwa RC anayeongoza kuangaliwa kwenye mitandao ya kijamii kutokana na kila kukicha anakuja na misemo mbalimbali.

Kwa mfano alianza na msemo wa ‘fyekelea mbali’, sukuma ndani’, juzi tena maneno hayo “habari imekwisha, anayebisha anayesema mkuu wa mkoa unachozungumza ni cha kijinga jinga sana, nyosha mkono, jifanye unajikuna, jifanye tu unajikuna, alafu ona, alafu unajikuna, kwamba kitu hiki chote unachotwambia haina maana yoyote”. Haya ni maneno yake.

Lakini pia akiwa ziara ya kukagua ujenzi wa kituo cha Igalula, aliibuka na “ama zangu ama zenu”. Nimekuwa nikipata tabu mno juu ya kauli hizi. Kiongozi makini hawezi kuwa na kauli za aina hii.

Najiuliza mno hivi hii ni aina gani ya uongozi ambao hivi sasa tuna ushuhudia. Namfahamu mno Mwanri tangu akiwa Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), alivyokuwa akijibu maswali pale bungeni kuhusu mashauri mbalimbali.

Namnukuu: “Utasikia anasema mheshimiwa Spika, kabla ya kuingia ndani ya Bunge nimezungumza na mkurugenzi wa mji fulani…. na nimemwambia aniletee jibu kabla ya saa 10 za jioni leo”. Niliamini haya yameishia bungeni kumbe yamekwenda Tabora.

Sina ugomvi na Mwanri hata kidogo, lakini napenda kumsihi na kutambua kuwa yeye ni mkuu wa mkoa anayemwakilisha rais katika mambo yote yanayohusu mkoa wake, hivyo wakati mwingine hapaswi kutunishiana msuli na watu wake kiasi hiki tena mbele ya vyombo vya habari.

Hata kama ndiyo aina yake ya uongozi, namshauri ajaribu kupunguza mambo haya, natambua namna fyekelea mbali ilivyompaisha, sasa si wakati wa kubweteka kwa misemo. Kiongozi makini ni yule anayefanya mambo yake wakati mwingine kimya kimya kushughulikia matatizo ya wananchi wake.

Naamini nguvu kubwa ya misemo hii, kama angekuwa anaielekeza kwenye kuhamasisha kaya masikini kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF), kuanzisha miradi ya kuwakomboa vijana, vyama vya ushirika na mengine mengi, ingekuwa safi sana, kwa sababu natambua jiografia ya Mkoa wa Tabora ilivyo.

Ningependa kuona nguvu ya misemo hii, inatumika kuhimiza wananchi kupata maji, elimu na mambo mengi ambayo yatawakomboa wananchi wa Igunga, Nzega, Sikonge, Uyui, Urambo na Tabora yenyewe. Kuhusu wanafunzi kupata mimba, hili nakuunga mkono ‘fyekelea mbali wote’. Namalizia kwa kusema Mwanri, unanikumbusha enzi za Al-Sahhaf na uvamizi wa Marekani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles