NA RAYMOND MINJA IRINGA
MKUU wa Mkoa wa Iringa, Amina Msenza, amewataka viongozi wa Serikali za Mitaa kuwa waadilifu na kutojiingiza katika mauzo ya ardhi ili kuepukana na migogoro ya ardhi inayoendelea kila kukicha .
Pia amepiga marufuku ujenzi holela wa kuporomosha mawe na kujenga milimani, mabondeni na katika vyanzo vya maji.
Kutokana na hali hiyo, ameitaka manispaa iweke vibao vitakavyoonyesha maeneo hayo yamehifadhiwa ili kuepuka uvamizi.
Masenza ametoa maagizo hayo wakati akizungumza na viongozi wa Kata ya Kitwiru iliyopo Manispaa ya Iringa jana.
Alisema lengo la ziara hiyo ni kutembelea na kukagua ujenzi
holela katika Mtaa wa Kibwabwa B, kukagua uchimbaji na upondaji wa mawe unaofanywa na baadhi ya wananchi katika eneo la Shule ya Msingi Mnazi Mmoja na kukagua hali ya usafi wa mazingira katika mitaa ya Kitwiru na Uyole.
“Ninatoa agizo kwa wale wote wanaoporomosha mawe na kujenga, naomba wachukuliwe hatua za kinidhamu milimani, mabondeni na katika vyanzo vya uhifadhi hairuhusiwi kujenga, ninaomba manispaa iweke vibao
vitakavyoonyesha maeneo yaliyohifadhiwa ili yasivamiwe na kuanza kuuzwa ovyo na wale wenye tamaa za kujipatia hela kwa njia za mkato,” alisema Masenza.
Aliwataka wananchi kufuata kanuni na taratibu zilizowekwa na Serikali, ikiwa ni pamoja na kupata vibali vya ujenzi na mara wanapotaka kununua viwanja ili kuepukana na migogoro na udanganyifu kutoka kwa viongozi wasio waaminifu.
“Wenyeviti wa mitaa tuendelee kuwadhibiti wananchi wasitende makosa ya kujenga bila kufuata kanuni na taratibu za ujenzi, ikiwa ni pamoja na kufuata michoro iliyopo,” alisema Masenza.
Naye Kaimu Mkurungenzi wa Manispaa ya Iringa, Omary Mkangama, alisema Manispaa ya Iringa ni miongoni mwa halmashauri zinazokua kwa kasi kubwa, jambo linalosababisha kukithiri kwa ujenzi holela.
Alisema hali hiyo inatokana na ongezeko la idadi ya watu, kutanuka kwa mji na ufinyu wa maeneo.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kitwiru, Simba Nyunza, akisoma taarifa ya mikakati ya uboreshaji wa matumizi ya vyoo bora na usafi wa mazingira, alisema majengo 2,255 ndiyo yenye vyoo bora sawa na asilimia 93 ya majengo yote yaliyotambuliwa.