24.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, June 26, 2024

Contact us: [email protected]

DC Mapunda atoa wito Viwanda na kampuni kuwezesha matembezi ya hisani ya “TRRH WALKATHON”

Na Mwandishi Wetu

Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mhe. Sixtus Mapunda, ametoa wito kwa viwanda na kampuni jirani kuchangia katika matembezi ya hisani yanayoandaliwa na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke (TRRH). Wito huo umetolewa katika uzinduzi wa matembezi hayo yanayoitwa TRRH Walkathon, ambapo Mhe. Mapunda alikuwa mgeni rasmi.

Matembezi hayo yanayotarajiwa kufanyika tarehe 27 Julai 2024, yanalenga kusaidia idara ya watoto wachanga katika hospitali hiyo kwa kununua vifaa maalumu vya kuhudumia watoto waliozaliwa kabla ya wakati na kuanzisha wodi maalumu ya uangalizi wa hali ya juu (ICU).

Mhe. Mapunda amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kutoka kwa wamiliki wa viwanda na kampuni katika wilaya ya Temeke ili kufanikisha matembezi hayo ambayo yanalenga kuokoa maisha ya watoto wachanga. Ameeleza kuwa hospitali hiyo ina wataalamu na ujuzi wa kutosha, lakini inahitaji vifaa maalumu vya kuhudumia watoto wachanga ili kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke, Dkt. Joseph Kimaro, ameeleza kufurahishwa na ushiriki wa wadau katika uzinduzi huo, kwani inaonyesha utayari wa jamii kusaidia watoto. Dkt. Kimaro ameeleza kuwa TRRH Walkathon itahusisha matukio mbalimbali kama vile uchangiaji wa damu wa hiari, upimaji wa afya wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza, na upimaji wa saratani ya kizazi. Huduma hizi zote zitatolewa bure na wataalamu wa afya kutoka hospitali ya Temeke.

Dkt. Kimaro ametoa mwito kwa wananchi na wadau mbalimbali kuungana na hospitali hiyo katika matembezi ya TRRH Walkathon na kusaidia kufanikisha uanzishwaji wa wodi yenye vifaa maalumu vya kuhudumia watoto wenye uhitaji wa huduma ya uangalizi wa juu (ICU).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles