Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amefanyiwa dua maalumu ya kumuombea aweze kutimiza majukumu yake aliyokabidhiwa na Rais Dk. John Magufuli ya kuongoza mkoa huo.
Dua hiyo ilifanyika jana katika kituo cha maombi kinachosimamiwa na Sheikh Chifu Msopa maarufu kwa jina la Sharif Majini.
Sheikh Msopa lisema anaamini kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu mkuu huyo wa mkoa ataweza kuhimili majukumu yake aliyopewa akiwa katika umri wa ujana ikiwa ni pamoja na kutenda haki kwa wananchi wote.
Akizungumza kwenye ofisi za Kituo cha Maombi kilichopo Mabibo mwisho, Dar es Salaam, Sheikh Msopa, alisema lengo kuu la dua hiyo ni kuhakikisha Makonda anaendelea kutimiza wajibu wake kwa kumtanguliza Mungu.
“Leo (jana), tumeamua kufanya dua nzito kwa ajili ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na dua hii ni kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ampe afya njema, ampe hekima na busara kwenye kutimiza majukumu yake.
“Hakuna asiyejua changamoto za Mkoa huu wa Dar es Salaam ambao una watu wengi na mambo mengi lakini pia ndiyo kioo cha nchi.
“Kwa hali hiyo na kwa dhati kabisa tumeamua kuendesha dua hii ambayo wananchi mbalimbali wamedhudhuria kama manavyoona,” alisema Sheikh Msopa.
Alisema Makonda amekuwa ni mmoja wa viongozi vijana wenye uwezo tangu alipokuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni ambako amefanya kazi kubwa ikiwamo kuwa mbunifu kwa ajili ya wananchi anaowaongoza.
Sheikh Msopa alisema kwa hali hiyo viongozi wa dini wana nafasi kubwa ya kuendesha maombi kwa viongozi waliopewa nafasi ili Mwenyezi Mungu awafanyie wepesi kwa kutimiza majukumu yao ya utendaji na kwa haki.
“Makonda ni aina ya kiongozi ambaye siku zote anasimama kwenye haki na ndiyo maana ameweza kutatua migogoro mingi iliyokuwa inatokea kwenye Wilaya ya Kinondoni na sasa amekabidhi ukuu wa mkoa tunaamini Mungu atamuongoza zaidi.