Na Clara Matimo, Mwanza
Kuendelea kutekelezwa kwa miradi ya barabara chini ya kiwango na baadhi ya Wakandarasi kushinda tenda wakati hawana mitambo ya ujenzi kumemchefua Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, ambaye amelazimika kutoa maagizo mbalimbali ili kukomesha vitendo hivyo.
Amesema ni marufuku wakandarasi hao kupewa miradi katika mkoa huo kwani majina yao anayo huku akiiagiza Wakala wa Barabara Tanzania(Tanroads) Mkoa wa Mwanza kuhakikisha wakandarasi wanaopewa zabuni ni wale ambao wana vifaa vya kufanyia kazi.
Mhandisi Gabriel alitoa agizo hilo hivi karibuni baada ya kufanya ukaguzi wa miradi ya barabara katika wilaya za Magu na Kwimba mkoani humo inayotekelezwa kwa kiwango cha changarawe ambapo alionyesha kusikitishwa na utekelezaji duni , miradi kutelekezwa na wakandarasi na mingine ujenzi wake kusimama kutokana na wakandarasi kukosa vifaa vya kufanyia kazi.
Akizungumzia maagizo hayo ya Mkuu wa Mkoa Mhandisi Gabriel, Meneja wa Tanroads Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Boniface Mkumbo, alisema “Nimechukua maagizo yako mkuu wa mkoa na nitaenda kukaa na wafanyakazi wenzangu ili tukubaliane jinsi ya kutatua changamoto hii, haiwezekani mkandarasi afanye vibaya zaidi ya kilomita 10 hadi 20 hii inadhihirisha na msimamizi wetu naye ana matatizo tutarekebishana ili tuweze kufanya vizuri zaidi,”alisema .
Kwa upande wao Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi(CCM) Wilaya ya Magu, Isack Zabron na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mpandalume Simon, walishangazwa na kitendo cha Tanroads Mkoa wa Mwanza kusubiri maagizo ya mkuu huyo wa mkoa wakati wao ndiyo wanaowapa zabuni (wanaowaajiri)wakandarasi hao hivyo walipaswa kuwachukulia hatua mapema.
“Mimi haininingii akilini kwa kweli Meneja wa Tanroads unaposema kwamba tutachukuliana hatua sisi kwa sisi hii inadhihirisha kwamba muda wote mlikuwa hampiti site kukagua kazi inayofanywa na mkandarasi hadi mkuu wa mkoa anapofanya ziara maana hii ipo chini ya ofisi yako kwa hiyo bila mkuu wa mkoa msinge baini tatizo?, Alihoji Zabron.
Mkuu wa Wilaya ya Magu Salum kalli, alimpongeza mkuu wa mkoa kwa kufanya ziara ya kukagua miradi ya barabara inayosimamiwa na Tanroads maana ameweza kubaini changamoto hizo huku akisisitiza kwamba wasimamizi wa Tanroads ambao wameshindwa kuwasimamia vizuri wakandarasi nao wawajibike.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Johari Samizi, alisema wanashirikiana vizuri na Tanroads kuhakikisha miradi ya barabara wilayani humo inatekelezwa kwa viwango ambavyo vinaendana na thamani halisi ya fedha iliyotolewa na serikali.
“Mimi niliishamuahidi Meneja wa Tanroads Mkoa wa Mwanza nikamwambia utanichoka yaani kama utanichoka utanichoka sana kwa sababu siwezi kuiona tofauti yoyote nikakaa kimya lazima nitatoa taarifa kwa wakati kabla jambo halijaharibika zaidi,”alisema Samizi.
Nao baadhi ya wananchi wa wilaya hizo akiwemo Shija Marco na Matha John walimpongeza mkuu wa mkoa kwa kufanya ziara hiyo na kuwapa elimu ya jinsi ambavyo mkandarasi anatakiwa kutekeleza miradi ya barabara na kuahidi kutoa taarifa endapo watabaini ameruka hatua moja wapo.
“Mkuu wa mkoa wetu ametufundisha kwamba hatua ya kwanza ni kutifua udongo wote na kusawazisha, kisha kumwagia maji huo udongo uliotifuliwa , kushindilia wanaleta udongo wenye kokoto au mawemawe kidogo (molamu)wanaweka karibu sentimita 10 wanaumwagia maji wanaushindilia kabisa inakuwa ni kama lami ya vumbi, elimu hii itatusaidia kuwabaini wakandarasi wasio waadilifu,”alisema Marco.