Na BENJAMIN MASESE
MKUU wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, amewaonya na kuwataka watumishi katika mkoa huo kila mmoja abebe msalaba wake.
Amewasisitizia kufanya kazi, kuacha visingizio na kila mtu awajibike kwa nafasi yake kutekeleza mipango na maelekezo ya Serikali.
Mongella alikuwa akizungumzia hatua ya wananchi kujitokeza na mabango wakati wa ziara za viongozi wa taifa katika mkoa huo.
RC alisema hali hiyo haimpendezi na yeyote atakayezembea kuwahudumia wananchi kwa nafasi yake na malalamiko yakajitokeza kwa viongozi wa taifa, atawajibishwa baadaye.
Alitoa angalizo hilo huku kukiwa na taarifa kuwa Rais Dk. Magufuli anatarajiwa kuwasili mkoani Mwanza Mei 11, mwaka huu kutembelea shughuli mbalimbali za miradi ya maendeleo.
Mongella alikuwa akizungumza katika kikao cha kupokea taarifa ya utekelezaji wa hatua ya kuanzishwa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi Tanzania (HPV) kwa wasichana wenye umri wa miaka 14 mkoani Mwanza.
Alisema imekuwapo tabia ya watumishi kupoteza muda kubishania jambo fulani badala ya kutumia nguvu kufanikisha mipango ya Serikali.
Mongella alisema wapo baadhi ya watumishi wanakwamisha mipango ya Serikali kutokana na tabia yao ya visingizio vingi na kutaka wabembelezwe kutimiza wajibu wao hata kupitisha barua wakati wameajiriwa kwa kazi hiyo.
Aliwataka wakuu wa wilaya na wakurugenzi kuwasilisha taarifa kwake ya utekelezaji miradi kila baada ya miezi mitatu.
“Hapa leo tunajadili suala la chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana wenye umri wa miaka 14 lakini tunashuhudia watumishi wanavyotafuta visingizio kibao.
“Wanatumia muda mwingi kubishania jambo lisilo na maana badala ya kutumia nguvu kufanikisha kitu kilicho mbele yao.
“Tambueni hata vitabu vitakatifu vinasema kwamba mtu akibembelezwa kutimiza wajibu wake ni dhambi, sasa mimi sitaki kubeba dhambi ya mtu kisa hataki kutimiza wajibu wake kila mmoja abebe msalaba wake.
“Mnataka kiongozi aje hapa wa taifa wananchi wajitokeze na mabango, sitakubali tutaajibishana.
“Twendeni vijijini tukawahudumie wananchi, mfano katika hili la saratani linakwamisha maendeleo kwa sababu mama mmoja akiwa na saratani lazima familia itayumba hata kama wana uwezo wa fedha.
“Tambueni asilimia 80 ya shughuli za nyumbani zinafanywa na mama, bila kusimamia afya na uhai wa watu tutakuwa tunajidanganya kupata maendeleo,” alisema.