NA TIMOTHY ITEMBE
MKUU wa Mkoa wa Mara, Adam Malima amezitaka halmashauri zinazojishugulisha na kilimo cha kahawa kuhakikisha kilimo hicho kinapanda kutoka tani 2000 hadi tani 3200 kwa mwaka ifikapo mwaka 2022.
Malima alisema mkakati mwingine wa mkoa huo katika kahawa ni kuhakikisha Mara inalima kahawa kwa wingi na yenye ubora ili kuwavutia wanunuzi na kuongeza kipato.
“Tunahitaji kilimo cha kisasa chenye tija kuongeza wingi na ubora wa kahawa.
“Kwa hali hiyo tunatarajia kuwa na soko la kahawa hapa hapa Tarime badala ya kusumbuka kwenda kutafuta masoko nje ya Tarime.
“…Tutakuwa tumepunguza gharama za usafirishaji ambazo zinatutesa huku tukipata fedha kidogo ya kuendeshea shughuli za maendeleo ikiwamo ya familia,”alisema Malima.
Alizitaka halimashauri za Tarime, Butiama, Bunda, Serengeti na Rorya kuandika andiko la kuomba mkopo wa fedha ifikapo Aprili 30 kutoka benki ili kuongeza jitihada za kilimo cha kahawa ndani ya miaka mitano.
Mmoja wa wajumbe wa Bodi ya kahawa, Melkiad Masawe alisema kazi ya bodi ni kutafuta masoko.
Alisema ili wakulima waweze kunufaika na kilimo cha kahawa ni sharti walime kwa kuzingatia kanuni za kilimo na kujiandikisha katika daftari la kilimo hai.
Kikao hicho cha wadau wa wakahawa kilifanyika Nyamwaga wilayani Tarime kujadili mkakati wa kufikia lengo la tani 5000 ifikapo mwaka 2022.
Ofisa kilimo na Umwagiliaji Wilaya Tarime,Sluvanus Gwiboha alisema kuhakikisha kuwa lengo linafikiwa sharti wakulima wapande kahawa ya vikonyo.
Mkakati uliopo kwa halmashauri ya Tarime ni kulima kahawa kwa njia ya vikonyo na mbegu ili kuongeza uzalishaji kwa eneo kutoka tani 0.8 hadi tani 1.5 kwa hektaa.
Mwingine ni kuongeza kilimo cha kahawa kutoka tani 2000 hadi tani 3200 kwa mwaka na kuandaa vitalu vitatu vitakavyozalisha miche 1,005,000 ifikapo 2021/2022.